July 28, 2015

Morani waua mkulima

 *Wamchoma mkuki, wampasua kichwa

Na Bryceson Mathias, Mbigiri

VIJANA zaidi ya 40 wa jamii ya Kimasai (Morani) wamemuua mkulima, Maiko Ngorongoro (40), baada ya kumchoma mikuki ubavuni na kumpasua kichwa.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Tuwatugawe Mbigiri, Daniel Shabani, amedai mkulima huyo akiwa shambani, ghafla walitokea morani hao wakiwa na mikuki, visu na marurungu, wakamshambulia na kumchoma mkuki marehemu na kumuua baada ya kumpasua kichwa.

Imeelezwa kwamba, wafugaji hao (morani) walikuwa wakitembeatembea mashambani wakiangalia wakulima wanaolima mashambani, ambapo walipowaona walianza kuwashambulia na kumuua marehemu.

“Wafugaji wakipata janga japo ng’ombe wao kukamatwa, polisi yote ya wilaya na mkoa inafika haraka na magari, silaha na kila kitu, lakini mkulima akifa, ni polisi na gari, kwa nini?” alihoji Shabani.

Wananchi hao kwa hasira, walizuia mwili wa marehemu Ngorongoro usichukuliwe na Jeshi la Polisi  hadi afike Mkuu wa Mkoa,  Dk. Rajabu Rutengwe, atoe uamuzi kwa nini wanaonewa na kuuawa ovyo na wafugaji hao kama kuku.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul, alipopigiwa simu yake ya Kiganjani atoe ufafanuzi alipokea mlinzi wake, na alipoelezwa juu ya tukio hilo alisema sawa bila kutoa ushirikiano.

Wananchi kwa upande wao wameilalamikia Serikali Kuu wakisema, Serikali iache mzaha na maisha ya watu, itatue mgogoro huo haraka maana utapoteza watu wengi.

No comments:

Post a Comment

Pages