July 16, 2015

TTCL YATOA MSAADA WA VIFAA VYA UJENZI KATIKA SHULE YA SEKONDARI LUSWISWI ILEJE MBEYA


 Meneja wa TTCL Mkoa wa Mbeya, James Mlaguzi akisoma taarifa ya msaada uliotolewa na kampuni hiyo katika shule ya Sekondari Luswisi.
 Mbunge wa Ileje aliyemaliza muda wake,Aliko Kibona akitoa shukrani kwa niaba ya  wananchi wa Kata ya Luswisi kwa kampuni ya TTCL kutokana na msaada waliopokea.
 Mbunge Aliko Kibona pamoja na Meneja wa TTCL wakikabidhiana mifuko ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu.
 Mbunge na Meneja wakipongezana baada ya kukabidhiana Saruji na Mbao.
 Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Luswisi wakifurahia msaada uliotolewa na TTCL.
 Wanafunzi wakisaidia kushusha mifuko ya saruji iliyotolewa na kampuni ya TTCL.
 Watumishi wa TTCL Mbeya wakijadiliana jambo kabla ya kuanza makabidhiano ya msaada wa saruji na mbao katika shule ya sekondari Luswisi.
 Baadhi ya wanakijiji waliojitokeza kupokea msaada huo.
 Watumishi wa TTCL Mbeya wakimsikiliza Mbunge alipokuwa akitoa shukrani kwa  niaba ya wananchi.

  Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Luswisi, Mseven Ndangalaakielezea furaha yake baada ya kupokea msaada wa saruji na mbao kutoka TTCL.
 Ngoma za asili zikiendelea kutoa burudani katika hafla ya kukabidhiana msaada wa saruji na Mbao. 

*************
KAMPUNI ya simu ya TTCL imetoa msaada wa saruji na mbao katika Shule ya Sekondari ya Luswisi iliyopo Kata ya Luswisi Wilaya ya Ileje mkoani Mbeya kwa ajili ya ujenzi wa nyumba mbili za Walimu na chumba kimoja cha darasa.
Kampuni hiyo ilitoa msaada wa mifuko 100 ya saruji na mbao vyenye thamani ya shilingi Milioni tatu ikiwa ni kupunguza changamoto inayowakabili Walimu wa Shule hiyo ambayo inawalimu 22 huku ikiwa na Nyumba moja iliyokamilika ambayo anaishi Mkuu wa Shule.
Wakizungumza baada ya kupokea msaada huo baadhi ya Walimu hao wakiongozwa na Makamu Mkuu wa Shule, Mseven Ndangala, alisema Walimu wanaishi katika wakati mgumu kwani asilimia kubwa wamepangishwa na wanakijiji sehemu ambayo ni mbali na eneo la shule.
Alisema Walimu wengi wamepanga umbali wa kilomita 7 kutoka shuleni hivyo hulazimika kukodi pikipiki kuwapeleka na kuwarudisha shule kwa gharama ya shilingi 6000 kwa siku hali inayowarudisha kwenye umaskini na kupunguza ari ya kufundisha kutokana na kutumia gharama kubwa kwenye usafiri.
Aliongeza kuwa hivi sasa kuna walimu wapya watano ambao kwa mazingira yalivyo hawataweza kupanga kutokana na ukosefu wa fedha na kuwalazimu kuishi walimu wote watano kwenye chumba kimoja hali inayoonesha kuwakatisha tama kuendelea kufundisha shuleni hapo.
Awali akikabidhi msaada huo, Meneja wa TTCL Mkoa wa Mbeya, James Mlaguzi, alisema Kampuni ilipata maombi kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Ileje, Aliko Kibona kwa ajili ya kusaidia kupunguza adha hiyo jambo ambalo lilikubaliwa na hatimaye kuwafikishia.
Alisema kampuni imejipanga kuhakikisha mwishoni mwa mwaka huu inapeleka huduma za mawasiliano vijijini ili kuwawezesha wakulima kutafuta masoko ya mazao yao kwa njia za mtandao.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ileje aliyemaliza muda wake, Aliko Kibona aliwashukuru kampuni ya TTCL Hususani Afisa mtendaji Mkuu Dk. Kazaula Kamugisha kwa kumkubalia ombi lake ili kuhakikisha walimu wanakuwa na mazingira mazuri ya kufundishia kwa kuwajengea nyumba nzuri.
 
Aidha alitoa wito kwa Watendaji wa vijijini na Kata kuhakikisha wanasimamia vizuri msaada huo kwa kuhakikisha unafanya kazi zilizokusudiwa ili kuwaridhisha waliotoa misaada na hivyo kuwafanya wawe na moyo wa kujitolea katika kipindi kingine.
Aliongeza kuwa ni wajibu wa Wabunge, wadau na wananchi kuhakikisha wanatumia kila njia wanatengeneza mazingira mazuri ya Walimu kuwa na ari kubwa ya kufundisha kuliko kuitegemea Serikali kwa kila kitu.

No comments:

Post a Comment

Pages