Na Bryceson Mathias, Kilosa
HATIMAYE wakulima wenye hasira wa
Kijiji cha Mbigiri, Kilosa Morogoro, wameruhusu maiti ya Maiko Ngorongoro(40),
aliyeuawa na vijana zaidi ya 40 wa jamii ya Kimasai (morani) kwenye mashamba ya
wakulima, ichukuliwe na polisi, baada ya jana kumzuia asichukuliwe hadi Mkuu wa
Mkoa wa Morogoro, Dk. Rajabu Rutengwe, afike.
Tukio la mauaji ya Ngorongoro yalitokea
huku kukiwa na sintofahamu ya viongozi wa kijiji hicho, Hamad Ibrahim (Mwenyekiti),
Jacob Mvungi (Mtendaji wa Kijiji) na Maftaha Hamis (Mwenyekiti wa Tawi la
Chadema-Mbigiri), wakiwa bado wako mahabusu Kilosa, wakitakiwa kueleza ni nani
waliosababisha kuuawa kwa ng’ombe takriban 300 kwa kukatwa miguu na majereha
mengine, Machi mwaka huu.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Tuwatugawe,
Daniel Shabani, alsema wakulima wameiruhusu maiti hiyo ichukuliwe na polisi,
baada ya kuwa na maridhiano baina ya uongozi wa Wilaya ya Kilosa na mwakilishi
wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro aliyemwakilisha, Dk. Rutengwe.
Hata hivyo wakati wakulima hao
wakiridhia maiti hiyo kuchukuliwa na Polisi baada ya maridhiano na uongozi wa serikali
ya Wilaya ya Kilosa na Mkoa wa Morogoro, Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha wafugaji
cha Mabwegere, Mika Kashu, amekamatwa na polisi kufuatia tukio hilo.
Kukamatwa kwake kunatokana na vijana
zaidi ya 40 (Morani) wa kifugaji, ambao jana waliwashambulia wakulima waliokuwa
mashambani wakilima na wakamuua, Ngorogoro, kwa kumchoma mikuki ubavuni na
kumpasua kichwa.
Toka jana baada ya mauaji hayo, wakulima
walisikika wakiilalamikia Serikali Kuu kwamba, vyombo vyake vya usalama
wilayani Kilosa na mkoani Morogoro, vimekuwa vikiwapendelea na kuwabeba wafugaji
kila yanapotokea majanga baina yao, wakidai kuna kiashiria cha rushwa
kinawabeba.
“Wafugaji wakipata janga, japo ng'ombe
mmoja kukamatwa anapokula mazao yetu, viongozi wa serikali, polisi ya wilaya na
mkoa, wanahamia eneo la tukio haraka wakiwa na magari, silaha na kila kifaa cha
ulinzi, lakini mkulima akifa, polisi wanakuja kwa kusuasua,” alisema Shabani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro,
Leonard Paul, alipopigiwa simu jana kwenye simu yake ya kiganjani atoe
ufafanuzi, simu yake ilipokewa na mlinzi wake, na alipoelezwa juu ya tukio hilo
alisema sawa bila kutoa ushirikiano.
No comments:
Post a Comment