HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 28, 2015

ASKOFU AISHAURI TUME YA UCHAGUZI ZANZIBAR

DODOMA, Tanzania

ASKOFU wa Kanisa la Methodist Jimbo la Dodoma, Juliasi Bundara ameishauri Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kuachana na mpango wake wa kurudiwa uchaguzi, baadala yake kura zihesabiwe upya.

Kurudiwa kwa uchaguzi huo kumetokana na uwamuzi wa kutatanisha, wa Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, wa kufuta matokeo ya uchaguzi huo Mkuu wa Zanzibar baada ya kuona CCM inashindwa.

Kufutwa kwa matokeo hayo kumeiingiza nchi katika giza la kisiasa, na mkwamo kutokana na kambi ya Upinzani kudai Chama cha Wananchi CUF kitangazwe kuwa ndiyo kimeshinda uchaguzi huo.

Kambi hiyo ya Upinzani inayoundwa na vyama Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), imeweka wazi hivi karibuni wakati wa Bunge la 11, kuwa uhalali wa Rais John Magufuli unategemea kutangazwa kwa Rais mshindi halali ambaye ni Maalim Shariff Hamad.

Askofu Bundara, alitoa misimamo wake huo wakati alipozungumza na Tanzania Daima, mjini Dodoma jana juu mkwamo huo wa kisiasa nchini.

Alisema kwa vile Zanzibar kama nchi inayo matatizo mbalimbali katika jamii hivyo ni vema fedha zinazo kusudiwa kutumika katika kurudia uchaguzi huo, zikaelekezwa katika mambo ya msingi kama vile miradi ya kilimo, Maji, umeme, na mawasiliano.

"Ni jambo la ajabu sana kuona uchaguzi ukirudiwa na fedha hizo kwa nini zisingetumika katika kuboresha hata elimu ikiwa ni pamoja na kuboresha masilahi ya watumishi ambao wanalipwa kipato ambacho hakikidhi katika maisha yao, "alisema Askofu Bundara.

Askofu Bundara, alisema kuna haja ya pandezote kukutana mezani kwa ajili ya kujadiliana juu ya kuhesabu upya kura zilizopigwa na iwapo itabainika chama kimojawapo kimeshinda au kimeshindwa ni vyema kikakubali matokeo.

"Nibora Rais Magufuli awakutanishe wagombea hao wa Zanzibar ili waweze kutatua migogoro iliyopo kwa sasa jambo pekee ni kukubaliana na matokeo"alisema.

Mbali na hilo aliwakemea wanasiasa ambao hawapendi kukubaliana katika maamuzi ya wananchi na baadala yake kulazimisha yale wanayoyataka kwa ajili ya masilahi yao binafsi pamoja na wapambe wao jambo ambalo ni la hatari kwa nchi.

"Watanzania tumeiombea sana nchi yetu iendelee kuwa na Amani hivyo ni tatizo kubwa kwa baadhi ya wanasiasa kuchochea vurugu na kukataa ukweli pale inapoonekana kuna ukweli.

"Ni lazima ufike wakati wanasiasa watambue kwamba uongozi ni sawa na mbio za vijiti kwa hiyo kuna kupokezana na pale mtu anaposhindwa huna budi ya kukubali matokeo.

"Wenye maamuzi ni wapiga kura na hao wana maamuzi yao na mapenzi yao na itambuliwe kuwa wao ndiyo wanakaa na wale wanao wataka kutokana na uwezo wao wa kusimamia haki katika jamii, "alisema Askofu Bundara. 

Askofu Bundara ni jambo la hatari kwa wananchi kulazimishwa katika kuchaguliwa viongozi wasiowataka kwani wakichochoshwa na uwamuzi huo, matokeo yake ni mwanzo wa machafuko ambayo yanaweza kusababisha kuvurugika kwa amani na tunu nyingine za Taifa.

No comments:

Post a Comment

Pages