·
Kamba wanaume watwaa ubingwa
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
TIMU ya soka ya Uchukuzi SC jana ilitwaa ushindi wa
tatu wa mashindano ya Mei Mosi, baada ya kuwashinda Tanesco magoli 3-2 kwa
mikwaju ya penati, katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani
hapa.
Ushindi wa Uchukuzi SC ulichagizwa na kipa wao
mahiri William Barton aliyeweza kudaka penati tatu kati ya tano zilizopigwa na
Tanesco.
Baada ya ushindi huo, Barton alimwaga machozi ya
furaha, kwani alidaka penati zilizopigwa na kipa mwenzake Hashim Yahya, Khalifa
Shekuwe na Abdallah Magubile.
Penati za Uchukuzi SC zilifungwa kwa ufundi stadi na
Fidelis Kyangu, Masoud Masoud na Kado Nyoni, wakati waliokosa ni Omary Said
‘Chidi’ na Seleman Kaitaba.
Hatua ya penati ilifuatiwa baada ya timu hizo kutoka
suluhu katika dakika 90 za kawaida na kwa mujibu wa sheria za mashindano hayo
hakina nyongeza ya dakika 30 na inapigwa mikwaju ya penati moja kwa moja.
Kocha wa Uchukuzi SC, Elutery Muholeli alisema kuwa
mchezo ulikuwa na ushindani mkubwa, na wachezaji wake walicheza kwa kujituma,
na dhamira yao ilikuwa ni kutwaa ubingwa, lakini bahati haikuwa yao na
wamebahatika kutwaa ushindi wa tatu.
Naye kocha wa Tanesco, James Washokera alikiri
wachezaji wake kukosa umakini kutokana na kikosi chake kukosa wafungaji, na
aliamua kuwatumia viungo zaidi, ili kufunga magoli lakini walishindwa kutokana
na kucheza nafasi sio yao.
“Unajua hii timu yetu ilitakiwa kuwa ni kombaini ya
Tanesco Tanzania nzima, lakini haikuwa hivyo na badala yake wametoka sehemu
chache na nilitarajia ningechagua wafungaji kutoka mikoani, lakini sikupata
nafasi hiyo, ila hili tatizo huu ndio mwisho wake na mwakani tutakuja kamili
kwani nitahakikisha ninazunguka na kupata wachezaji sehemu zote,” alisema Washokera.
Pia Uchukuzi wanaume wameibuka mabingwa wa mchezo wa
kamba baada ya kumaliza ikiwa imejikusanyia pointi 10, na haikuwahi kuvutwa na
timu yeyote tangu michuano hiyo ianze.
Nayo CDA ‘Watoto wa nyumbani’ wameshika nafasi ya
tatu katika mchezo wa netiboli wakiwa na pointi tatu sawa na Tanesco iliyoshika
nafasi ya nne , lakini wanatofautiana kwa magoli ya kufunga na kufungwa, huku
TPDC ikiburuza mkia ikiwa haijapata pointi yeyote.
Abubakar Mwamachi (9) wa Uchukuzi SC akikokota mpira huku mlinzi wa Tanesco Juma Rajabu akiwa ameshika ardhini.
Omary Kitambo (4) wa Uchukuzi SC akiwania mpira uliopigwa na Stanley Uhagile wa Tanesco. Uchukuzi ilitwaa ushindi wa tatu kwa penati 3-2.
Kipa Willium Barton wa Uchukuzi SC akikaa tayari kupangua penati ya kipa mwenzake wa Tanesco Hashim Yahya. Uchukuzi ilitwaa ushindi wa tatu kwa penati 3-2.
Wachezaji wa michezo mbalimbali wa timu ya Uchukuzi SC wakishangilia baada ya timu ya soka kutwaa ushindi wa tatu kwa penati 3-2 dhidi ya Tanesco.
No comments:
Post a Comment