Mhe. Samia Hassan, Makamu wa Rais;
Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu;
Ndugu Gratian Mukoba, Rais wa Shirikisho la Vyama
vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA);
Mama Nortubunga Maskini, Makamu wa Rais wa TUCTA;
Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu;
Mhe. Tulia Ackson, Naibu Spika;
Balozi Injinia John Kijazi, Katibu Mkuu Kiongozi;
Mheshimiwa Jordan Rugimbana, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;
Waheshimiwa Mawaziri wote, na Waheshimiwa Wabunge
mliopo;
Bi. Mary Kawar, Mkurugenzi wa Shirika la Kazi
Duniani (ILO), Ofisi ya Nchi za Afrika Mashariki;
Waheshimiwa Mabalozi mliopo;
Waheshimiwa Majaji,
Mheshimiwa Almas Maige, Mwenyekiti wa Chama cha
Waajiri Tanzania;
Dr. Aggrey Mlimuka, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama
cha Waajiri Tanzania (ATE);
Ndugu Nicholaus Mgaya, Katibu Mkuu wa Shirikisho la
Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA);
Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi;
Viongozi na Maafisa wa Serikali mliopo;
Wawakilishi wa Vyama vya Siasa mliopo; Mzee
Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM
Bwana Kimbisa (Mb), Mwenyekiti wa CCM Mkoa;
Wanahabari;
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Dodoma;
Ndugu Wananchi;
Ndugu Wafanyakazi;
Mabibi na Mabwana.
Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa
kutupa uhai na afya njema na kuweza kukutana hapa. Leo ni siku muhimu sana.
Tupo hapa kwa ajili ya kuenzi na kuthamini mchango wa wafanyakazi wa Tanzania,
wake kwa waume, walioko sekta binafsi na ya umma, na ambao kila siku tangu asubuhi hadi jioni
wamekuwa wakivuja jasho kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu.
Hii si mara yangu ya kwanza nashiriki Sherehe ya
Siku ya Wafanyakazi, maarufu kama Mei
Mosi. Nimeshiriki kwenye sherehe hizi mara kadhaa. Lakini leo nashiriki
kipekee kabisa. Nashiriki kwa mara ya kwanza tangu nichaguliwe kuwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Oktoba 2015. Hivyo, napenda kuchukua nafasi
hii kuwashukuru Viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) na
Vyama vyote vya Wafanyakazi nchini kwa kunialika ili nijumuike nanyi kwenye
Sherehe hizi za Siku ya Wafanyakazi Duniani mwaka huu. Aidha, napenda
kuwashukuru wafanyakazi wote wa Tanzania kwa kunipa kura nyingi
zilizoniwezesha kuchaguliwa kuwa Rais wa
nchi hii. Naahidi kwenu kuwa sitawaangusha.
Nitumie fursa hii pia kuwapongeza sana wananchi
wa Mkoa Dodoma chini ya Uongozi wa Mkuu
wa Mkoa, Mheshimiwa Jordan Rugimbana kwa kukubali kuwa wenyeji wa Sherehe hizi pamoja na maandalizi mazuri
mliyofanya kufanikisha sherehe hizi. Sherehe zimefana, hongereni sana!
Nawashukuru pia wananchi wa Dodoma kwa kunipa kura nyingi wakati wa uchaguzi
Mkuu wa mwaka jana.
Aidha, ninawashukuru sana Wafanyakazi na Wananchi
wote mliojitokeza hapa leo kwa wingi ili kujiunga na wenzetu duniani kote
kusherehekea siku hii muhimu ya Wafanyakazi Duniani.
Ndugu Wafanyakazi na Wananchi kwa ujumla;
Duniani kote wafanyakazi ni nguzo muhimu ya
maendeleo. Hakuna taifa lolote duniani ambalo limeweza kuendelea bila kutegemea
wafanyakazi wake. Hapa nchini, wafanyakazi wametoa mchango mkubwa kwa maendeleo
ya taifa letu tangu kipindi cha ukoloni hadi sasa. Bila shaka wengi wetu hapa
tunafahamu namna wafanyakazi na vyama vya wafanyakazi vilivyoshiriki kikamilifu
katika harakati za ukombozi wa nchi yetu. Baada ya nchi yetu kupata uhuru,
wafanyakazi wameendelea kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi yetu.
Nitumie fursa hii kuwapongeza wafanyakazi kote nchini
kwa kazi kubwa na nzuri mnayoifanya kwa maendeleo ya taifa letu. Ninyi ndio
mmejenga miundombinu mbalimbali tunayoitumia hivi sasa, ninyi ndio
mnahakakikisha Watanzania wanapata huduma bora za elimu na afya lakini hata
ulinzi na usalama wa taifa letu kwa kiwango kikubwa unategemea ninyi
wafanyakazi. Hongereni sana wafanyakazi!
Ndugu Wafanyakazi na Wananchi kwa ujumla;
Kama nilivyotangulia kusema, hii ni sherehe yangu
ya kwanza ya Mei Mosi tangu nimechaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa nchi
yetu. Hivyo, napenda kutumia fursa hii adimu kuzungumza na wafanyakazi pamoja
na wananchi kwa ujumla kuhusu masuala na mipango mbalimbali ambayo Serikali ya
Awamu ya Tano ninayoingoza imepanga kutekeleza katika kipindi cha miaka mitano
ijayo.
Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuona nchi
yetu inapata maendeleo kwa manufaa ya Watanzania wote. Tumejipanga kufanikisha
utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 pamoja na Ilani ya Uchaguzi
ya Chama Tawala. Sote tunafahamu kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo inalenga kuiwezesha
nchi yetu kuwa ya uchumi wa kati unaongozwa na viwanda. Ili kutekeleza Dira ya
Maendeleo na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala, tayari tumekamilisha Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano
utakaotekelezwa katika kipindi cha mwaka 2016/17 hadi mwaka 2020/21.
Mpango huu
unadhima ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na
maendeleo ya watu. Lengo kuu la Mpango huu ni kuhakikisha rasilimali na fursa
za nchi zinatumika vizuri ili kujenga uchumi wa viwanda na kupunguza umasikini.
Baadhi ya malengo mahsusi ni kuimarisha kasi ya ukuaji mpana wa uchumi kwa
manufaa walio wengi, kuongeza kasi ya kupunguza umaskini, kuongeza fursa ya
ajira kwa wote, kuongeza upatikanaji na ubora wa huduma za jamii na kuongeza
mauzo nje kwa bidhaa za viwandani.
Ndugu Wafanyakazi na Wananchi;
Baadhi ya
masuala muhimu yaliyomo kwenye Mpango wa Maendeleo ambayo tutayatekeleza katika
kipindi cha miaka mitano ijayo ni pamoja na kufufua viwanda na kujenga vipya,
hususan vinavyotumia malighafi zinazopatikana kwa wingi hapa nchini, teknolojia
ya kati, nguvu kazi na ambavyo bidhaa zake zitatumika zaidi hapa nchini,
ikiwemo viwanda vya nguo na bidhaa za ngozi. Aidha, tunakusudia mazingira ya
uzalishaji na uendeshaji biashara kwa kuhakikisha tunajenga miundombinu ya nishati
ya umeme, reli, barabara, maji, madaraja, vivuko, bandari, viwanja vya ndege na
TEHAMA. Tunalenga pia kuhakikisha kuwa panakuwepo ardhi kwa ajili ya uwekezaji
na upatikanaji wa rasilimali-watu yenye ujuzi. Halikadhalika, tutaboresha sera,
sheria, taratibu, uratibu na ushirikiano wa kitaasisi.
Maendeleo ya
uchumi ni lazima yaende sambamba na maendeleo ya watu. Ili kuhakikisha hilo,
vipaumbele vitakuwa ni kuhakikisha watu wanaondokana na umaskini, njaa na
ukosefu wa ajira. Aidha, tutaboresha huduma za jamii, hususan afya na elimu, kwa
kuhakikisha zinapatikana kwa uhakika na ubora unaostahili. Tutahakikisha watu
wengi wanajiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii na pia panakuwepo na usawa wa
jinsia na watu wenye ulemavu, utawala bora, mipango miji na kuogeza juhudi za
kukabiliana na athari za tabianchi.
Matumaini yetu ni kwamba utekelezaji wa Mpango huu
utaleta matokeo chanya kwa nchi yetu kwa kukuza uchumi kutoka asilimia 7 mwaka 2015 hadi asilimia 10 mwaka 2020; kuongeza mapato
ya yatokanayo na kodi kutoka asilimia
12.1 ya pato la taifa mwaka 2014/15 hadi asilimia 17.1 mwaka 2020; kuongezeka kwa kasi ya kupunguza umaskini
ambapo pato la wastani kwa kila mwananchi litaongezeka kutoka wastani wa dola
za Marekani 1,006 mwaka 2015 hadi 1,500 mwaka 2020; umaskini wa mahitaji
ya msingi kupungua kutoka asilimia 28.2 mwaka 2011/12 hadi asilimia 16.7 mwaka 2020/21; huduma za msingi za afya na elimu
zitaimarika; kuongezeka kwa mauzo nje ya nchi ya bidhaa za viwandani; kuongeza
idadi ya watalii na kuongeza uwekezaji wa moja kwa moja kutoka dola la
kimarekani bilioni 2.14 mwaka
2014/15 hadi bilioni 5 mwaka 2021. Hayo
ndiyo malengo yetu.
Ndugu Wafanyakazi na Ndugu Wananchi
Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Taifa utagharimu
takriban shilingi trilioni 107, zikiwemo
trilioni 59 kutoka Serikalini.Kwa
kuanza, kwenye bajeti ijayo, Serikali
imetenga kiasi cha jumla ya shilingi trilioni
11.82 kwa ajili ya bajeti ya maendeleo sawa na asilimia 40 ya bajeti yote kutoka asilimia 26 mwaka uliopita. Kati
ya fedha za bajeti ya maendeleo, shilingi 8.702
trilioni sawa na asilimia 74 ya
bajeti ni fedha za ndani na fedha za nje ni shilingi 3.117 trilioni sawa na asilimia 26.
Kama mnavyoona, sehemu kubwa ya ugharamiaji wa
mpango huu itafanyika kwa kutumia fedha za ndani. Hii ishara tosha kuwa
tumedhamiria kufanikisha azma yetu ya kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya
mwaka 2025 ili kuleta maendeleo nchini mwetu na kuwaondolea wananchi kero
mbalimbali.
Ndugu Wafanyakazi na Ndugu Wananchi;
Bila shaka baadhi yenu mtashangaa kwa nini nimetumia
Sherehe hii ya Wafanyakazi kuongelea malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano
katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Jibu ni moja tu. Imenilazimu kueleza
hayo yote ili sisi wafanyakazi wote hapa nchini tufahamu kazi kubwa iliyopo
mbele yetu. Sisi ndio tunategemewa kuwaongoza Watanzania katika kutekeleza na
kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025. Hivyo, tunaposherehekea
sikukuu hii ya wafanyakazi duniani hatuna budi kila mmoja wetu kujiuliza ni kwa
namna gani tutachangia katika kufanikisha utekelezaji wa Mpango huu wa
Maendeleo kwa nchi yetu. Kwa kifupi, naweza kusema kuwa mipango yote mizuri niliyoieleza
hapo juu haiwezi kufanikiwa kama wafanyakazi hawatashiriki kikamilifu.
Hivyo basi, nitoe wito kwa wafanyakazi kote nchi
kila mmoja kwa nafasi yake kujipanga vizuri katika kutekeleza Mpango huu. Ni
lazima tufanye kazi kwa bidii na kujituma, ueledi mkubwa na uadilifu. Nchi yetu
haitaweza kufikia uchumi wa kati unaoendeshwa kwa viwanda kama tutaendelea kulea
uvivu, uzembe, ubadhirifu, rushwa, ukwepaji kodi, kutotimiza wajibu wetu na wafanyakazi hewa. Kwa kutambua hilo, Serikali yenu imeanza
kuchukua hatua za kuimarisha nidhamu na uwajibikaji kwa watumishi Serikalini. Tayari
tumeanza kuwashughulikia watumishi wachache ambao ni wazembe, wavivu, wala
rushwa, wabadhirifu na wasio na maadili.
Nafahamu, watumishi wazembe na wabadhirifu ni wachache.
Lakini watumishi hao ndio wamekuwa wakiharibu sifa nzuri ya watumishi wa umma.
Hawa ndio wamekuwa wakirudisha nyuma gurudumu la maendeleo la nchi yetu. Hawa
ndio wamekuwa wakinufaika na kunyonya jasho la wafanyakazi walio wengi wa
Tanzania. Sasa mwisho wao umefika.
Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuwashugulikia popote walipo. Hatutawaonea
aibu au huruma watumishi wa aina hii. Nimefurahi kusikia Vyama vya Wafanyakazi
viko pamoja na Serikali na havitaunga mkono mtumishi mzembe, legelege na
fisadi. Mmezidi kutupa nguvu zaidi ya kuendelea na jitihada tulizozianzisha za
kurejesha nidhamu ya kazi kwenye utumishi wa umma. Niwaombe pia tushirikiane
katika kushughulikia wafanyakazi hewa. Wafanyakazi hewa wameigharimu Serikali
fedha nyingi ambazo zingeweza kuboresha maslahi ya wafanyakazi halali na
kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Hadi leo
idadi ya wafanyakazi hewa waliopatikana ni 10,295.
Kati ya wafanyakazi hao 8,373 ni
kutoka Serikali za Mitaa na 1,922 ni
wa Serikali Kuu. Kutokana na wafanyakazi hao hewa Serikali imekuwa ikilipa
kiasa cha shilingi 11,603,273,799.41
kila mwezi sawa na shilingi
139,239,285,592.92 kwa mwaka sawa na shilingi
696,196,427,964.6 kwa miaka mitano. Fedha hizi zingeweza kujenga barabara
za juu (flyovers) tano au kuboresha maslahi ya watumishi halali ama kuboresha
huduma mbalimbali za jamii. Aidha, nafasi hizo hewa zingeweza kutoa ajira kwa
wahitimu wa vyuo vikuu mbalimbali ambao wanatafuta kazi na hivyo kuleta manufaa
kwa taifa.
Ndugu Wafanyakazi;
Wakati nikitoa rai kwa watumishi legelege,
wabadhirifu na wala rushwa kubadilika, napenda pia kutumia fursa hii kuwapa
moyo wafanyakazi wote ambao ni wachapakazi na ambao wanatekeleza majukumu yao
kwa ueledi na uadilifu. Endeleeni kufanya kazi kwa kujiamini, kujituma bila ya
kuwa wasiwasi wowote. Nafahamu wapo
baadhi ya watu wamekuwa wakiwatisha na kuwaeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano
haijali wafanyakazi. Wapuuzeni watu hao. Hao ndio wale waliokuwa wakinufaika au
kushirikiana na watumishi mafisadi, wala rushwa na wabadhirifu. Sasa
wanatapatapa baada ya kuona Serikali inachukua hatua mahsusi kwa watumishi wa
namna hiyo. Serikali ya Awamu ya Tano haitambuguzi mfanyakazi yeyote ambaye
anajituma na kufanya kazi kwa ueledi na uadilifu. Nipende kusema tu Serikali
yangu itawalinda na kuwatetea wafanyakazi waadilifu na wachapakazi.
Ndugu Wafanyakazi;
Wakati wa Kampeni na hata nikifungua
Bunge niliwaahidi wafanyakazi wote wa umma na sekta binafsi kuwa ningeboresha
maslahi na mazingira yenu ya kufanya
kazi, ikiwemo kuongeza mishahara, kuwapatia vitendea kazi, pamoja na kulinda na haki za msingi za hifadhi ya jamii kama huduma
za afya na malipo ya pensheni baada ya kustaafu kazi. Ahadi yangu
hii bado ipo pale pale na nawaahidi tena sitawaangusha. Kwa bahati nzuri hata kaulimbiu
ya Mei Mosi mwaka huu ambayo; “Dhana ya Mabadiliko Ilenge Kuinua Hali ya
Wafanyakazi” inasisitiza umuhimu wa kuboresha maslahi na mazingira ya
kazi ya wafanyakazi.
Kama alivyosema Katibu Mkuu wa TUCTA kuwa tangu
tumeingia madarakani, tumeweza kuongeza ukusanyaji wa mapato kutokana na kuziba
mianya mingi ya ukwepaji kodi na kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima. Hata hivyo, sio dhamira yetu na bila shaka sio
dhamira ya Watanzania walio wengi kuona fedha zote tunazokusanya tunazitumia
kwa ajili ya kulipia mishahara watumishi tu. Nasema hivi ili mfahamu kwamba mapato haya yanawahitaji wengi sana.
Wananchi walio wengi wamepata matumaini kuwa kutokana na kuongeza kwa mapato
sasa huduma mbalimbali zitapatikana kwa ubora na uhakika. Hivyo, niwajibu wetu
sisi mliotukabidhi kuongoza Serikali kuhakikisha tunatumia vizuri rasilimali za
nchi kwa manufaa ya Watanzania wote. Na ninapenda kutumia fursa hii
kuwahakikishia kuwa tutaelekeza fedha tunazozipata katika maeneo muhimu ambayo
yanamgusa kila Mtanzania, wakiwemo wafanyakazi.
Ndugu Mwenyekiti wa TUCTA;
Ndugu Katibu Mkuu wa TUCTA;
Ndugu Wafanyakazi;
Hivi punde
nimetoka kusikia risala yenu nzuri iliyosomwa na Katibu Mkuu wa TUCTA, Bwana
Nicholas Mgaya. Sitaweza kujibu hoja zote zilizotajwa kwenye risala yenu.
Lakini napenda kuwahakikishia kuwa Serikali imezipokea hoja zenu zote na
tutazifanyia kazi. Hata hivyo, naomba mniruhusu nieleze japo kwa uchache baadhi
ya hoja mliyotaja kwenye risala yenu:
Kwanza, kuhusu suala la kupunguza kodi ya mapato ya mshahara (PAYE) kwa
wafanyakazi. Napenda kuwaarifu kuwa Serikali
yangu kama nilivyoahidi wakati wa kampeni zangu nimeamua kuwapunguzia Wafanyakazi
kodi ya Mapato ya Mishahara kutoka asilimia
11 ya sasa hadi asilimia 9
kuanzia mwaka wa fedha wa 2016/17 kutegemea Wabunge watakavyopitisha bajeti
yetu. Tuna uhakika kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumewapunguzia wafanyakzi mzigo
mkubwa wa makato katika mishahara yao. Nimeamua kuanza na hili kwanza ili
changamoto zilizopo sasa za kiuchumi tuweze kuzivuka na baadaye mambo yakiwa
mazuri tutaangalia suala la kupandisha mishahara.
Pili, suala la tofauti ya mishahara. Tayari tumeanza kuchukua hatua kuhakikisha
tunakuwa na mfumo wa mishahara ambao unazingatia vigezo vya uzito wa kazi na
kupunguza tofauti kubwa ya malipo ya mshahara kwa kuoanisha mishahara ya
watumishi wa Umma walioajiriwa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Taasisi na
Mashirika ya Umma. Tunataka Watumishi wa Umma wafaidi matunda ya kazi kwa kuzingatia
uzito wa kazi wanazozifanya kwa misingi ya haki na usawa.
Aidha, kufuatia marekebisho ya Sheria ya Taasisi za
Kazi Na.7 ya Mwaka 2004, tumeunda Bodi mbili za mishahara. Bodi ya mshahara
katika Sekta Binafsi inayosimamiwa na Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Kazi
na Ajira, na Bodi ya Mshahara katika Utumishi wa Umma inayosimamiwa na Waziri
mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma. Majukumu ya Bodi hizi ni kufanya uchunguzi
na kupendekeza kima cha chini cha mshahara katika sekta husika. Ni matarajio yetu
kwamba bodi hizi zitatekeleza majukumu yake kwa weledi kwa kupendekeza viwango
vinavyozingatia hali halisi ya uzalishaji, tija na uchumi wetu. Nilikwisha
tamka sitarajii kuwa na mfanyakazi anayelipwa zaidi ya milioni 15 wakati wengine wanalipwa laki tatu kwa mwezi.
Tatu, suala la hifadhi ya jamii. Serikali ya Awamu ya tano inalenga katika
kuhakikisha kwamba wananchi wengi zaidi watafaidika na mfumo wa hifadhi ya
Jamii nchini kuliko ilivyo sasa. Kwa
mfano tunataka wananchi wengi zaidi wajiunge na Bima ya Afya ili wawe na
uhakika wa matibabu. Tunaendelea na juhudi ya kupanua wigo wa Mfuko wa Bima ya
Afya vijijini (Community Health Fund) na
pia kuwezesha wafanyakazi wengi wa sekta binafsi kujiunga na Mfuko wa Taifa wa
Bima ya Afya (National Health Insurance Fund). Aidha, Mifuko ya Hifadhi ya
Jamii imeanza kusajili wananchama toka sekta isiyo rasmi. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba
wananchi wengi wanapata huduma za msingi za hifadhi ya jamii.
Kwa upande wa kuimarisha Mifuko ya hifadhi ya jamii
pamoja nakuboresha malipo ya Pensheni, Serikali imekwishaelekeza Mifuko ya
Hifadhi ya jamii kuachana na uwekezaji kwenye miradi isiyokuwa na tija.
Wawekeze kwenye maeneo kama viwanda ili kuzalisha fursa za ajira na kujipatia
wanachama zaidi. Aidha, ushauri wenu wafanyakazi kupitia shirikisho lenu la
TUCTA kwa Serikali kuhusu kupunguza idadi ya Mifuko ya Pensheni nchini na
matumizi yasiyo ya lazima umepokelewa na kukubalika. Lakini ni vyema mfahamu
kwamba kutokana na historia tofauti ya kuanzishwa kwa mifuko ya hifadhi ya
jamii iliyopo sasa, hatua zozote za marekebisho zinahitaji umakini mkubwa.
Napenda niwahakikishie kwamba kazi ya kurekebisha mifuko ya Pensheni nchi
tutaikamilisha ndani ya mwaka 2016/2017.
Nne,
suala la Vyama vya Wafanyakazi. Napenda kutoa rai kwa waajiri kote nchini kutambua kwamba suala hili sio la hiari bali
ni wajibu wao kuwaruhusu wafanyakazi kuanzisha na kujiunga kwenye vyama vya
wafanyakazi sehemu za kazi bila ya kushurutishwa au kuchaguliwa chama cha
kujiunga. Hivyo, waajiri wote wanaovunja
takwa hili la sheria watachukuliwa hatua kali. Lakini pia nitoe wito kwenu Viongozi
na wafanyakazi vyama hivyo visitumike kuchocheo migogoro ya kikazi, uzembe na
uvivu kazini na wala visiwe vyama vya kisiasa kazini. Vyama hivyo vinapaswa
kutumika kuimarisha uhusiano kati ya waajiri na waajiriwa, kuhamasisha utendaji
kazi na kuleta utulivu sehemu za kazi.
Tano,
suala la mikataba ya ajira. Waajiri wengi wamekuwa hawatekelezi matakwa sheria
kama yalivyobainishwa katika Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka
2004 pamoja na marekebisho yake ambayo tumeyafanya mwaka 2015. Bado yapo malalamiko mengi ya wafanyakazi
kutokuwa na mikataba ya kazi, kufanya kazi bila vifaa kinga, michango ya
pensheni kuchelewa kuwasilishwa au kutowasilishwa kabisa kwenye mifuko ya
hifadhi ya jamii. Serikali ya Awamu ya Tano ninayoongoza haitavumilia ukiukwaji
huu wa sheria.
Ili
kuhakikisha waajiri wanatekeleza kwa hiari bila shurti sheria za kazi, tuanza
kurekebisha tena Sheri ya Ajira na mahusiano kazini kwa kuanzisha adhabu za
papo kwa papo ambapo waajiri watalazimika kulipa faini kwa kila kosa la
kutotekeleza sheria za kazi. Pia, katika mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga
fedha kuajiri maofisa kazi zaidi wapatao 21 ili kuimarisha huduma za ukaguzi
sehemu za kazi. Nitoe wito kwa Vyama vya wafanyakazi, kushirikiana kwa karibu
na Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu). Aidha,
ninaziagiza Mamlaka zinazohusika kusimamia utekelezaji wa Sheria za kazi
kusimamia sheria husika bila woga kwa lengo la kuwalinda wafanyakazi
wasiendelee kutumikishwa na kunyonywa.
Aidha,
naziagiza mamlaka husika kushughulikia suala la ajira za wageni ambazo zinaweza
kufanywa na wazawa. Hakuna nchi yoyote duniani ambayo jukumu lake kubwa ni
kuwatafutia ajira wageni kazi ambazo ingeweza kufanywa na wazawa. Naagiza
Wizara zote zisimamie hili suala kwa nguvu zote ili wazawa wapate ajira kwanza.
Sambamba na hilo, wahusika wote mshirikiane pia kuwafichua wale wote
watakaofanya kazi bila vibali. Nakumbuka zoezi hili lilianza sitaki kuamini
kuwa ilikuwa ni nguvu za soda. Mheshimiwa Waziri tafadhali simamia hili.
Suala jingine ambalo nalo limekuwa ni
tatizo sugu ni baadhi ya waajiri kushindwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi
wao kwenye mifuko ya hifadhi kwa wakati.
Ingawa wafanyakzi wamekuwa wakikatwa kila mwezi lakini fedha hizo
hazifiki kunakohusika. Tatizo hili pia linaihusu Serikali kutokana na Hazina
kutopeleka michango. Hivyo, natoa wito kwa waajiri wote nchini kuwasilisha
michango ya wafanyakazi wao kila mwezi bila kukosa. Hivyo, natoa wito kwa
waajiri wote nchini kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kila mwezi bila
kukosa.
Kwa
upande wa Serikali tayari tumeanza kulishughulikia suala hili la michango kwa
kutambua wafanyakazi wote halali ili michango yao iwasilishwe. Mathalan, kwenye
Mfuko wa PSPF Serikali ilikuwa ikidaiwa shilingi takriban bilioni 710 bilioni lakini hadi sasa tumelipa
takriban shilingi 500. Ni imani yangu kuwa michango ya inayotakiwa kulipwa na Serikali
kwenye Mifuko ya Hifadhi itapungua kutokana na zoezi la kuwaondoa wafanyakazi
hewa. Tunaomba Vyama vya Wafanyakazi vishirikiane na Serikali kufichua
watumishi hewa.
Ndugu Mwenyekiti wa TUCTA;
Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,
Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu
Waheshimiwa Mawaziri na Waheshimiwa Wabunge mliopo;
Ndugu Katibu Mkuu wa TUCTA;
Wageni Waalikwa;
Ndugu Wafanyakazi;
Mabibi na Mabwana:
Napenda
kuhitimisha hotuba yangu kwa kuwashukuru tena Viongozi wa TUCTA na Vyama vya
Wafanyakazi nchini kwa heshima mliyonipa ya kushiriki kwenye Sherehe hizi. Aidha,
napenda kurudia tena wito wangu kwa Wafanyakazi
na wananchi wote kwa ujumla, tuendelee kufanya kazi kwa bidii, kwa nguvu zetu zote, kwa maarifa yetu yote na kwa
kuzingatia misingi ya uwajibikaji na uadilifu ili tuweze kusukuma gurudumu la
maendeleo ya nchi yenu. Tuachane na mazoea ya watu kuingia kazini asubuhi na
kuondoka saa nne.
Tukumbuke
ya kuwa kazi ni utu, kazi sio fursa ya kupata mshahara kwa manufaa ya familia zetu
tu bali ni fursa nzuri ya kutoa mchago kwa taifa lako kwa manufaa ya kizazi cha
sasa na kijacho.
Mungu
Wabariki Wafanyakazi Watanzania!
Mungu
Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni
kwa Kunisikiliza”.
No comments:
Post a Comment