Timu ya soka ya Taifa ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ leo Mei 17, 2016 imechanua vema baada ya kuilaza India mabao 3-1 katika mchezo wake wa pili wa michuano maalumu ya kimataifa iliyoandaliwa na Shirikisho la Soka India katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Tilak, Maidan mjini Goa, India.
Mabao ya Serengeti Boys yalifungwa na Maziku Amani katika dakika ya 21 wakati lile la pili India walijifunga baada ya beki wake kuhangaika kuokoa krosi ya Nickson Kibabage katika dakika ya 28 wakati lile la tatu lilifungwa na Asad Juma katika dakika ya 48 huku lile la India likifungwa na Komal Thatal katika dakika ya 38.
Kwa ushindi huo, Serengeti Boys sasa wanasubiri angalau sare au ushindi wa mchezo mmoja kati ya miwili, dhidi ya Korea Kusini utakaopigwa Alhamisi Mei 19, 2016 na Malaysia Mei 21, 2016 ili icheze nusu fainali ya michuano hiyo iliyoanza Mei 12 kabla ya kufikia fainali zake Mei 26, mwaka huu. Katika mchezo wa kwanza, Serengeti Boys ilitoka sare ya Marekani ya bao 1-1.
Katika mchezo huo, Serengeti Boys iliwakilishwa na Ramadhani Kabwili, Ally Nganzi, Ally Msengi, Asad Juma, Dickson Job, Issa Makamba, Maziku Amani, Nickson Kibabage, Shaaban Ada, Syprian Mtesigwa na Mohammed Abdallah.
India: Mohammed Nawaz, Reamsochung Aimol, Boris Singh, Mohammed Khan, Juendra Singh, Suresh Wangjam, Amarjit Kiyam, Khumanthem Meetei, Sandjev Staldi, Aniket Jadhav na Komal Thatal.
No comments:
Post a Comment