Awali ya yote, tunapenda kuchukua fursa hii kuwashukuru sana kwa kuitikia wito wa kuja kutusikiliza. Karibuni sana!
Ndugu Waandishi wa Habari
Leo tumewaiteni ili kuwaeleza msimamo wa Chama chetu cha ACT Wazalendo juu ya uamuzi uliofanywa na Kamati ya Bunge ya Maadili na Madaraka ya Bunge kuwasimamisha wabunge saba wa upinzani akiwemo Mbunge wa ACT Wazalendo Ndugu Zitto Kabwe.
Ikumbukwe kuwa uamuzi huu wa Kamati ya Maadili ambayo sehemu kubwa ya wajumbe wake ni wabunge wa Chama cha Mapinduzi(CCM) unafuatia msimamo wa wabunge wa upinzani wakiongozwa na Mbunge wa Chama chetu kupigania maslahi ya wananchi kupata habari za bunge.
ACT tunaamini Wabunge hawa wametolewa kafara kwa kupinga vikali uamuzi wa Serikali kuzuia matangazo ya Bunge kurushwa moja kwa moja.
Ndugu waandishi wa Habari
Chama chetu kimeandaa mapokezi haya yaliyopewa jina maalum la “Opereshen” Linda Demokrasia, lengo likiwa ni kuwapa nafasi mashujaa hawa waliofukuzwa bungeni kwa ajili ya kusimamia maslahi ya umma, kuelezea kilichotokea na kinachoendelea bungeni ambacho watawala hawataki kijulikane.
Pia katika mkutano wa hadhara Kiongozi wa Chama ndugu Zitto Kabwe atafafanua kwa kina muktadha wa siasa za sasa na hatari ya kuua vita dhidi ya ufisadi kutokana na namna demokrasia inavyofifishwa
Ndugu waandishi wa Habari
Kwa kutambua umuhimu wa utetezi wa maslahi ya wananchi na kuisimamia serikali kupitia Bunge Chama chetu baada ya mkutano wa Dar esSalaam utakaofanyika Jumapili ya Juni 5 mwaka huu katika viwanja vya Mbagala Zakiem, pia Chama kitafanya mikutano mingine mikubwa ya hadhara katika mikoa ya Mwanza ( 11 Juni, 2016), Kigoma (12 Juni, 2016), Mbeya (18 Juni, 2016) na Morogoro (19 Juni, 2016).
Chama chetu kimeviandikia barua vyama vya CUF, CHADEMA na NCCR-Mageuzi kuviomba kushiriki kwenye mapokezi hayo.Tunasubiri majibu ya vyama tulivyowaalika kwa kuwaandikia barua kwa kuwa mpaka sasa hawajatujibu rasmi kama watashiriki ama la zaidi ya kutufahamisha kuwa wamepokea barua zetu
Ndugu Waandishi wa Habari
Sisi ACT-Wazalendo,tunaamini “Operesheni Linda Demokrasia” ni muhimu ikapiganwa na vyama vyote pasipo kujali itakadi ya vyama kwa kuwa hoja hiyo ya kutaka Bunge lioneshwe moja kwa moja ilipoibuliwa na Mbunge Ndugu Zitto Kabwe kuhoji hatua ya serikali kubana uwazi Bungeni,wabunge wote wa upinzani walisimama na kuiunga mkono hoja na kuitetea
Ndugu Waandishi wa Habari
Tunawashukuru tena kwa kuitikia kwenu wito wa kufika na tunawatakia majukumu mema ya ujenzi wa Taifa.
Ahsanteni sana!
Ndugu Ado Shaibu Ado
Katibu, Itikadi Uenezi na Mawasiliano ya Umma,
ACT Wazalendo
No comments:
Post a Comment