WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa wilaya
ya Tanganyika mkoani Katavi kuhakikisha unawaondoa watu wote wanaoishi katika
maeneo ya hifadhi na ushoroba wa
wanyama wa Lyamgoroka.
Agizo hilo limetolewa jana jioni (Jumatatu, Agosti 22,
2016) na Waziri Mkuu wakati akizungumza
na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kiwanja cha Majalila wilayani Tanganyika.
Waziri Mkuu alisema
wilaya hiyo inatakiwa kuendelea kuwaondoa watu wote waliovamia na kujenga
makazi ndani ya Hifadhi ya Taifa ya
Katavi ili kuepuka uharibifu wa mazingira.
“Hakikisheni mnatunza
mazingira. Msiache wakate miti hovyo kwa sababu wanakausha vyanzo vya maji na
kusababisha eneo kuwa hatarini kukumbwa na ukame, hivyo ni vyema wakaondolewa
mapema,” alisema.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amewataka Maofisa Ushirika na Kilimo
katika mkoa wa Katavi kuwasaidia wakulima wa tumbaku kwa kuhakikisha wanapata
soko la uhakika na kulipwa kwa wakati.
Waziri Mkuu alitoa agizo
hilo baada ya kupokea malalamiko ya wananchi kupitia mabango waliyokuwa wameyabeba
ambayo yalikuwa yakiwalalamikia maofisa hao kwa kushindwa kuwatafutia masoko na
badala yake wanawakumbatia wabadhilifu
wa fedha za ushirika.
"Hatuwezi kuwa na
Ofisa Kilimo ambaye hajui masoko ya mazao ya wakulima wake.Mnakaa ofisini tu!
Hamfanyi kazi. Lazima mfuatilie masuala ya kilimo katika maeneo yenu, sasa
chukua mabango yote yanayohusu zao la tumbaku na ukalete majibu kwa wakulima,”
alisema.
Awali Waziri Mkuu
alitembelea eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za halmashauri na
wilaya Tanganyika ambapo aliwapongeza wakazi wa kijiji cha Majalila kwa kutoa
bure ardhi yenye ukubwa wa ekari 500 ili Serikali iweze kujenga ofisi hizo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, AGOSTI 23, 2016.


No comments:
Post a Comment