August 02, 2016

PONDAMALI, MANYIKA DARASANI TFF

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limefanikiwa tena. Safari FIFA - Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu limeipa nafasi Tanzania kuwapa mafunzo ya juu ya ukocha wa makipa (Advanced Goalkeeping Coach Course) ikiandika historia kuwa nchi ya pili barani Afrika kwa makocha wa nafasi hiyo baada ya Botswana.
 
Makocha wa makipa 25 hususani wa wa timu za taifa, timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, wanahudhuria kozi hiyo inayoongozwa na Alejandro Heredia ambaye ni Mkufunzi kutoka FIFA.
 
Makocha hao ni Peter Manyika (Taifa Stars ya Tanzania), Saleh Ahmed (Zanzibar Heroes); Muharami Mohammed (Timu ya Taifa ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 - Serengeti Boys); Mohammed Silima (Timu ya Taifa ya Vijana Zanzibar) na Elyutery Mhoery (Timu ya Taifa ya Wanawake - Twiga Stars) na msaidizi wake ambaye pia anachezea JKT Queens, Fatuma Omary.
 
Wengine ni makocha maarufu wa makipa wakiwamo Juma Pondamali (Young Africans); John Bosco (Majimaji ya Songea); Salimu Tupa (Tanga); Bakari Ali Hamadi (Wete Pemba – Zanzibar); Hafidh Muhidin Mcha (Mkoani Pemba – Zanzibar); Mussa Wanena (Kagera Sugar); Juma Bomba (African Lyon), Adam Abdallah Moshi (Simba SC), Idd Mwinchumu (Azam FC) na Hussein Tade (Seeb Club-Oman/Toto African).
 
Pia wamo Khalid Adams (Mwadui FC); Josia Steven (Mbeya City); Herry Boymanda (Tanzania Prisons); Emmanuel Mwansile (Polisi Morogoro); Ben Kalama (Stand United); Abdallah Said (JKT Ruvu); Patrick Mwangata (Mtibwa Sugar); Augustin Malindi (Mkoa wa Kigoma); Raphael Mpangala (Ndanda FC); Salimu Tupa (Tanga) na nAbdul Mgude (Coastal Union ya Tanga).
 
“Mjione kwamba mmepewa kipaumbele,” alisema Heredia akiwanoa makocha hao na kuongeza: “Kinachohitajika sasa ni juhudi tu. Kozi hii haijafanyika pengine hapa barani Afrika zaidi ya Botswana. Mjue kuwa mna bahati.”
 
Akitoa nasaha wakati wa ufunguzi wa kozi hiyo, Makamu Rais wa TFF, Wallace Karia aliishukuru FIFA na CAF kwa namna inavyoshirikiana na TFF katika kuwapa kozio nyingi za makocha wa timu kwa wachezaji wa mbele, makocha wa makipa na waamuzi wa madaraja tofauti.
 
“Hakuna kipindi TFF imepata kozi za makocha nyingi za makocha kama kipindi hiki cha uongozi wa Jamal Malinzi,” anasema Karia na kuongeza: “Tumetoka kwenye kozi ya makocha wa Daraja A sasa tuko kwenu. Lengo ni Tanzania kuwe na makipa wazuri. Ninyi mtaleta makipa wazuri. Na hii ni kwa manufaa ya sasa na baadaye kwa upende wetu, timu zetu na taifa kwa ujumla.”
 
Karia aliwatia hamasa makocha hao wanaoshiriki kozi hiyo kuwa, mara baada ya kozi hiyo ipo siku watakwenda kuwa wakufunzi nje ya mipaka ya nchi kadhalika makocha ambao wanaweza kupata kazi mahala popote duniani hasa ukizingatia walimu wa daraja lao wako Tanzania na Botswana tu.
 
Kadhalika, Makamu huyo wa Rais wa TFF alielezea kuwa mpira wa miguu una changamoto nyingi na nyingine husababishwa na watalaamu hao kubweteka kwa mafanikio. “Hili ni tatizo. Tubadilike kifikra na kivitendo. Msilaze damu, kuweni active (mahiri).”
 
 
MIKATABA YA WACHEZAJI VPL, FDL
 
Shirikisho la Mpira wa MiguuTanzania (TFF) linapenda kuzikumbusha timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwamba hatutatoa leseni ya mchezaji yeyote ambaye timu haikuleta mkataba wakati wa maombi ya usajili, hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 68 vipengele vya 1, 2, 3 na 8 ya Ligi Kuu ya Tanzania toleo la 2016/2017.
 
Kila timu inatakiwa kuleta nakala tatu za mkataba wa mchezaji, ili kamati ya katiba, sheria na hadhi za wachezaji iweze kupitia na TFF iweze kuidhinisha mikataba hiyo. Baada ya hapo timu na mchezaji, watakuja kuchukulia mikataba hiyo hapa TFF. Na kumbuka kanuni ya 68(8) inataka kulipia kiasi cha sh 50,000 kwa kila mkataba wa mchezaji.
 
Ni matarajio yetu kuwa kila klabu itatimiza wajibu wake ili kuondoa migogoro kati ya timu na mchezaji na mchezaji na timu. Tunategemea kupata ushirikiano.
 
Kadhalika, kwa mujibu wa kanuni 67 vipengele vya 1, 2, 3 na 8 ya Ligi Daraja la Kwanza Tanzania ya StarTimes, Shirikisho la Mpira wa MiguuTanzania (TFF) linakumbusha kwamba halitatoa leseni ya mchezaji yeyote ambaye timu haikuleta mkataba wakati wa maombi ya usajili.
 
Kila timu inatakiwa kuleta nakala tatu za mkataba wa mchezaji, ili kamati ya katiba, sheria na hadhi za wachezaji iweze kupitia na TFF iweze kuidhinisha mikataba hiyo. Baada ya hapo timu na mchezaji mtakuja kuchukulia mikataba hiyo hapa TFF. Na kumbuka kanuni ya 67(8) inataka kulipia kiasi cha sh 25,000 kwa kila mkataba wa mchezaji.
 
Pia katika hili tunategemea kila timu itatimiza wajibu wake ili kuondoa migogoro kati ya timu na mchezaji na mchezaji na timu.

No comments:

Post a Comment

Pages