October 27, 2016

MTENDAJI WA TEMESA AAGIZA WATUMISHI TEMESA DODOMA KUJIANDAA NA SERIKALI KUAHAMIA MAKAO MAKUU

Mtendaji Mkuu wa TEMESA Dkt Mussa Mgwatu (kushoto) akizungumza  na Meneja wa TEMESA Dodoma, Mhandisi Bikulamchi (kulia) alipomtembelea ofisini kwake.


Na Theresia Mwami, TEMESA-Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu amewataka watumishi kuanza kujiandaa kwa kupokea kazi nyingi kwani hadi sasa Serikali na Taasisi zake tayari zimeanza kuhamia Dodoma.

Alisema kuwa kuhamia Dodoma kutaleta changamoto mbali mbali katika utoaji huduma za matengenezo ya magari, umeme, elektroniki na viyoyozi kwani mahitaji ya wateja yatakuwa ni mengi mno kuliko ilivyo sasa. 

Dkt. Mgwatu alizungumza hayo alipotembelea kituo cha TEMESA mkoani  Dodoma kuona changamoto na utendaji kazi na kuzungumza na  watumishi wa kituo hicho.

“Tuanze kujiandaa kwa ajili ya changamoto  hizo, tusingoje kuulizwa kwanini hatukujiandaa wakati tunafahamu kuwa serikali inahamia Dodoma na naomba mjipange kutoa huduma ipasavyo” Alisema Dkt. Mgwatu.

Aidha Dkt. Mgwatu amemuagiza Meneja wa TEMESA  Dodoma Mhandisi Bikulamchi kuanza kuandaa utaratibu wa namna ya kuendeleza kiwanja cha TEMESA Dodoma kilichopo eneo la Kizota  ili kuweza kukabiliana na changamoto ya mahitaji ya mji wa Dodoma yanayozidi kukua siku hadi siku.

“Ni mategemeo yangu kuwa katika kiwanja hicho tutaweza kujenga karakana kubwa tena ya kisasa ambayo itakuwa mfano mkoani hapa, ambayo itaweza kukidhi mahitaji yote ya soko la mkoa huu na hata nje ya mkoa, sambamba na ujenzi wa ofisi mpya ya TEMESA Makao Makuu” alisistiza Dkt Mgwatu.

Kwa mujibu wa Dkt. Mgwatu karakana hiyo ya kisasa ikijengwa itakuwa na watumishi wa ufundi na utawala kwa uwiano mzuri wenye kuzingatia taaluma husika ili kutoa huduma zenye ubora wa hali ya juu. Aliongeza kuwa itatakiwa kufanyika mabadiliko makubwa  ili kuweza kuwapata watumishi watakaoweza kuendana na kasi ya mabadiliko hayo katika kituo hicho.

Pia Dkt. Mgwatu aliwataka watumishi wa TEMESA Dodoma  kufanya kazi kwa kuzingatia taaluma walizo nazo, kuheshimu taaluma za wengine pamoja na kuzingatia maadili ya kazi, kufanya  kazi zenye ubora ili kuhakikisha wateja wanaridhika na kazi za TEMESA  na hivyo kuvutia wateja zaidi hata kutoka nje ya Taasisi za Serikali.

 Kwa upande wao wafanyakazi wa TEMESA Dodoma wamemuahidi Dkt. Mgwatu kufanya  kazi kwa bidii zaidi ili kuongeza mapato ya kituo na kwa ubora wa kazi ingawa bado kuna  changamoto ya kupatikana vitendea kazi vya kisasa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Mtendaji Mkuu wa TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu yuko katika ziara ya kikazi kutembelea vituo vilivyopo kanda ya Kati kuangalia utendaji kazi wake na kuona changamoto zilizopo ili ziweze kupatiwa ufumbuzi kwa maendeleo ya Wakala huo. 

No comments:

Post a Comment

Pages