October 15, 2016

'Oktoba 14 kwangu ina maana zaidi ya moja' Dk. Kigwangalla

Mtoto Sheila akimlisha keki baba yake Dk. Kigwangalla

Na Dk. Hamisi Kigwangalla.

Tarehe ya leo, miaka minane iliyopita alizaliwa binti yangu Sheila. Ni Mtoto wangu wa kwanza. Unaweza kukadiria mshawasha na mcheche niliokuwa nao siku hiyo. 

Kila mwaka tunapomkumbuka baba wa Taifa letu, basi mimi hukumbuka kuwa ni siku ya kuzaliwa mwanangu pia. Mwaka juzi niliandika makala. Nimeitafuta siioni. Nitajaribu hapa leo kurejea, Kwa ufupi, maudhui ya makala ile. 

Wakati naandika makala ile nilikuwa nimetoka kutangaza nia ya kuchukua fomu ya kuwania Urais. Nilitafakari sana mustakabali wa maisha yangu. Nilipotoka na nilipofikia. Nikahusianisha Tanzania ile na Tanzania ya akina Sheila. Mustakabali umebadilika kabisa! 

Mwanangu Sheila amezaliwa kwenye zama za utandawazi, elimu yake, Kwa mimi mzazi mwenye kuelewa dunia ya sasa na ushindani atakaopaswa kuukabili, naliona jukumu langu la kumuandaa vema. 

Mimi, hadithi yangu, ni tofauti sana na hadithi ya mwanangu. Siyo lazima na yeye apitie madhila yangu. Yeye ninamuandaa. Namuandaa ajue wajibu wake wa kujiandaa kupambana na ushindani. Mimi niliandaliwa na nchi. Hii ni tofauti kubwa ya kwanza. 

Mimi na Ndg. Bashe tulipoingia shule mwaka 1984, pale Shule ya Msingi Kitongo, na kufundishwa kusoma na kuandika na Mwl. Malunde, tulipelekwa kutimiza majukumu ya wazazi kama ambavyo Serikali ilikuwa ikielekeza. Watoto tulikuwa ni hazina nyeti ya Taifa, mali ya jamii nzima. Leo kila mtu na wanaye. Kila mtu na wa kwao. 

Darasa letu lilikuwa na watoto wa kila mtu, bila tofauti ya kipato ama cheo. Tulisoma na watoto wa Mkuu wa Wilaya, Watoto wa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Wilaya, Bwana Tawala, Meneja wa Benki, matajiri wa kiarabu na kihindi nk. Shule zilikuwa ndiyo hizo tu. Sote tulipata fursa sawa na kwa maana hiyo tulikuwa na mustakabali sawa wa maisha yetu ya baadaye. 

Mimi nilipelekwa shule na mama yangu mzazi, bi Bagaile Lumola. Hii ilikuwa ni siku ya kumbukumbu ya kipekee kwenye maisha yangu. Nilifurahia sana shule, japokuwa mara nyingi nilienda shule bila kula, na sare zangu za wasiwasi, miguu peku, lakini sikuwahi kuona tofauti yoyote ile kati yangu na watoto wa Mkuu wa Wilaya. Hata wao mara nyingine walikuja shuleni bila viatu. Sote tuliona sawa tu, kwamba ni 'kawaida' tu. Pengine hayo yalikuwa ndiyo maisha ya nyakati zile. 

Utandawazi umeibadilisha kabisa jamii yetu. Udugu wetu mpana unaanza kupotea. Zamani tatizo la mmoja wetu mtaani lilikuwa letu sote. Furaha yake ilikuwa yetu sote. Nakumbuka jirani na nyumbani kwa bibi yangu Mama Bagaile, aliyenilea, kulikuwa na familia ya Mzee mmoja mkatoliki mwenye kushika dini yake sana, Mzee Kidola, kila akitaka kuchinja, iwe kuku iwe mbuzi, atanoa kisu chake vizuri, atamfuata babu yangu, ambaye alikuwa muislamu. Na kila akichinja sisi ni lazima tuchekelee maana lazima agawe nyama kwa babu yangu. Hivyo hivyo, siku za Eid, ni lazima tuwapelekee sufuria la pilau na nyama. 

Mzee Kidola alipenda kufuturu nasi uji wa pilipili manga na chai ya viungo, enzi hizo tukifuturu nje ya nyumba barazani, na wapita njia wakikaribishwa! 

Upendo na mshkamano uko hatarini kupotea. Leo Ndg. Saidi anatolewa macho mchana kweupe, hadharani, anafanyiwa unyama watu wanatazama tu. Udugu wetu, upendo na mshkamano wetu umeenda wapi? 

Hii ni tofauti ya pili ya maisha ya makuzi yangu na makuzi ya mwanangu Sheila. 

Tanzania yangu mimi ni Tanzania iliyojengwa na baba wa Taifa, Mwl. Nyerere. Ni Tanzania iliyotoa fursa kwa mtoto aliyelelewa na mama ntilie kuota ndoto ya kuwa Daktari na kuitimiza. Ni Tanzania iliyotoa fursa sawa kwa mtoto wa  mama ntilie na mtoto wa Mkuu wa Wilaya kuwa Mbunge. 

Tanzania ya Sheila, mwanangu, ni Tanzania ninayowajibika kuijenga. Kila kukicha natafakari, Je ni Taifa gani ninaloandaa kwa ajili ya mwanangu na wajukuu zangu? 

Kila nikiangalia nyuma ninakotoka. Najiuliza nimefikaje hapa. Ni muujiza. Nikitazama tulipo na nikitafakari tunapokwenda, nabaki na maswali magumu sana kichwani! 

Hivi, Tanzania ninayoijenga mimi leo, itatoa fursa Sawa Kwa Sheila, mtoto wa Mbunge, na kwa mtoto mwingine wa mama ntilie kama mimi? 

Ninapokukumbuka baba wa Taifa moyo wangu unavuja damu kwa uchungu; machozi ya furaha na upendo yananitoka, ndoto zako zimegusa maisha yangu. Naahidi kufanya kila niwezalo kuishi falsafa yako, siyo kwa kutembea na 'kifimbo' tu na kuvaa suti za Mao, bali kwa kutoa uongozi madhubuti wakati wa kutunga sera ili kulinda misingi ya taifa tulilorithi kutoka kwa babu zetu. 

Viongozi wa zama zetu tuna kazi ya ziada ya kufanya. Ni lazima tuweke ubunifu kwenye malengo ya mbali ya Taifa letu, sera zetu na mikakati yetu. Zama zimebadilika, utandawazi umetamalaki, lakini kuna mambo ya msingi tuna wajibu wa kuyalinda kwa nguvu zetu zote kwa kuwa ni tunu za Taifa letu. 

No comments:

Post a Comment

Pages