October 27, 2016

UBALOZI WA PAPA, MAKANISA YAAMUA KUJENGA OFISI DODOMA

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dodoma, Beatus Kinyaiya kabala ya mazungumzo yao, Ofisini kwa Waziri Mkuu mjini Dodoma Oktoba 27, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri  Mkuu, Kassim Majaliwa  akizungumza na Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dodoma, Beatus Kinyaiya  (katikati) na Mkurugenzi Mtendaji wa  Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii, Peter Maduki (kushoto), Ofisini kwake jijini Dar es salaam.

* Yaomba kupatiwa viwanja, Waziri Mkuu awahakikishia vipo

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema amefurahishwa na uamuzi wa Kanisa Katoliki na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) wa kutafuta viwanja Dodoma ili wajenge ofisi za makao yao makuu pamoja na makazi ya viongozi wao wakuu.

Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Oktoba 27, 2016) wakati akizungumza na Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo Katoliki la Dodoma pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kikristo ya Huduma za Kijamii (CSSC), Bw. Peter Maduki ofisini kwake mtaa wa Railway, mjini Dodoma.

“Sina shaka juu ya maombi yenu ya kupatiwa viwanja kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu pamoja na makazi ya viongozi wakuu. Sasa hivi Master Plan ya Dodoma kama Makao Makuu ya nchi inapitiwa upya ili izingatie mahitaji ya msingi sababu zamani ilikuwa haijapangwa kwa mazingira ya sasa ya ujio wa Serikali,” amesema Waziri Mkuu.

Amesema wiki tatu zilizopita alimwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) ili atafute makampuni yenye uwezo wa kupima viwanja kwa haraka. “Hii itatusaidia kutambua tuna eneo kiasi gani na mahitaji halisi ni yapi na nani akija apewe eneo lipi kulingana na mahitaji yake,” ameongeza.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameyashukuru makanisa kwa huduma za kijamii zitolewazo katika sekta za elimu, afya na kilimo kama ambavyo ameshuhudia katika baadhi ya maeneo alikopita hapa nchini.

Pia amewakubalia ombi lao la kuwa na kikao cha pamoja baina ya watendaji wa Serikali na makanisa ambacho kitajadili namna ya kuimarisha ubia katika utoaji wa huduma za kijamii hususan za afya na elimu.

“Kikao hiki kitalenga kufanya mapitio ya huduma zinazotolewa baina ya Serikali na Makanisa lakini pia kitatusaidia kupata mrejesho wa mambo yanayofanyika kwenye hospitali na shule mnazomiliki katika maeneo mbalimbali hapa nchini,” aliongeza.

Amesema waharakishe kuleta mapendekezo yao ili kikao hicho kifanyike kabla ya Desemba, mwaka huu kwani kitaisaidia Serikali kupata mrejesho wa kuboresha baadhi ya maeneo katika mwaka mpya wa kielimu unaoanza Januari kila mwaka.

MapemaBaba Askofu Mkuu Kinyaiya alimweleza Waziri Mkuu kwamba wanahitaji eneo la kujenga ofisi za makao makuu na makazi kwa ajili ya kanisa hilo pamoja na makanisa yaliyo chini ya CCT ambayo kwa pamoja yanaunda Tume ya Kikristo ya Huduma za Kijamii (CSSC). Alisema wanahitaji eneo kwa ajili ya ujenzi wa ofisi na makazi ya Balozi wa Baba Mtakatifu.

Alisema walipowasilisha maombi yao CDA, waliahidiwa kupatiwa eneo la makazi tu lakini bado wanahitaji eneo la ofisi. Pia alitumia fursa hiyo kumshukuru Waziri Mkuu kwa jinsi alivyoiwakilisha Serikali kwenye mazishi ya Mhashamu Askofu Mstaafu, Mathias Isuja wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dodoma ambaye alifariki Aprili 13 na kuzikwa Aprili 20, mwaka huu.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa CSSC, Bw. Maduki alisema katika sekta ya afya hadi kufikia Juni 2016, makanisa yalikuwa yanamiliki na kuendesha hospitali 102, vituo vya afya 102 na zahanati 696. “Kati ya hospitali 102, mbili ni za rufaa za kanda na 38 ni za hospitali teule za Halmashauri za Wilaya na hospitali nyingine 62 zinatoa huduma halmashauri mbalimbali,” alisema.

Alisema karibu asilimia 38 ya hospitali hapa nchini zinamilikiwa na makanisa na nyingi ziko maeneo ya vijijini. Pia alisema kuna chuo kikuu kimoja, vyuo vikuu vishiriki vitatu, na vyuo vya mafunzo ya kati 62 ambavyo vinatoa kozi za uuguzi, maabara na ufamasia.

Kuhusu sekta ya elimu, Bw. Maduki alisema makanisa yanatoa elimu kuanzia elimu ya awali hadi chuo kikuu na kwamba hadi kufikia Juni, 2016, makanisa yalikuwa na shuke za msingi 161, za sekondari 369, na vyuo vya ufundi stadi 126. “Pia tuna vyuo vya ualimu 14, vyuo vikuu tisa, vyuo vikuu vishiriki 17 na vituo vya vyuo vikuu saba,” alisema.

                            
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
ALHAMISI, OKTOBA 27, 2016.

No comments:

Post a Comment

Pages