October 19, 2016

WAZIRI MKUU AMSIMAMISHA KAZI MHANDISI WA MAJI LINDI

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza wakati wa ziara yake Mkoani Lindi pamoja na mambo mengine Waziri Mkuu alimsimamisha kazi Mkurugenzi  wa Mamlaka ya Maji Lindi,  Mhandisi Adam Alexander kwa kushindwa kusimamimia ujenzi kituo cha kuzalisha maji katika Manispaa ya Lindi pamoja na matumizi mabaya ya ofisi. (Picha na Chris Mfinanga).
Mhandisi aliyesimamishwa kazi Adam Alexander.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Lindi (LUWASA), Mhandisi Adam Alexander kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi pamoja na kushindwa kusimamia ujenzi wa kituo cha kuzalisha maji katika Manispaa ya Lindi.

Waziri Mkuu amemkabidhi Mhandisi huyo kwa Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Lindi, Bw. Stephen Chami na kumuelekeza afanye uchunguzi zaidi juu ya suala hilo.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Oktoba 19, 2016) wakati alipotembelea mradi wa maji wa Ng'apa ambapo ameagiza nafasi hiyo ikaimiwe na Mkurugenzi Msaidizi wa mamlaka hiyo, Mhandisi Idrisa Sengulo.

"Kamanda wa TAKUKURU fanya mapitio ya kina ya mshahara wake. Yeye anasema analipwa Wizarani, mimi najua analipwa na LUWASA. Angalia kazi aliyokwenda kuifanya Dar es Salaam kama inalingana na siku alizokaa,” amesisitiza Waziri Mkuu.

Mhandisi hiyo anakabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya fedha za ofisi pamoja na kupokea mshahara bila la kulipa kodi ya mapato ya mshahara (PAYE), kujilipa kiwango kikubwa cha posho pamoja na kusafiri kwa muda mrefu.

Waziri Mkuu amesema Serikali haiwezi kuvumilia kuona wananchi wanapata shida huku watendaji waliopewa dhamana ya kuwatumikia hawaonekani kwenye vituo vyao vya kazi. "Huyu nimemuita mimi aje huku, hadi jana alikuwa Dar es Salaam."

Alipoulizwa sababu za kutokuwepo ofisini kwake kwa muda mrefu, Mkurugenzi huyo alisema kwamba alikuwa Dar es Salaam akiandika maombi ya fedha kwa ajili ya kutatulia changamoto mbalimbali zinazoikabili mamlaka hiyo.

"Unatumia siku ngapi kuandika proposal, msomi unatumia mwezi mzima kuandika proposal na unakaa Dar es Salaam hata Katibu Mkuu wako hajui na huko unajilipa posho tu! Tena baada ya kulipwa sh.120,000 kwa siku wewe unajilipa sh.150,000. Hatuwezi kuvumilia hali hii,” amesema.

Waziri Mkuu amemaliza ziara yake siku tatu mkoani Lindi na amerejea jijini Dar es Salaam.
                      
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 - DAR ES SALAAM
JUMATANO, OKTOBA 19, 2016.

No comments:

Post a Comment

Pages