January 17, 2017

DKT. MGWATU AWATAKA WATENDAJI TEMESA KUEPUKA WAZABUNI WANAOUZA VIPURI NA VILAINISHI KWA BEI ISIYO YA SOKO

Na Theresia Mwami, TEMESA
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Dkt. Mussa Iddi Mgwatu leo amefungua mafunzo elekezi kwa mameneja wa mikoa na vituo vya TEMESA juu ya tozo za matengenezo ya magari, pikipiki na mitambo pamoja na uaandaji wa taarifa za uzalishaji za mwezi kwa watumishi wa TEMESA kutoka katika mikoa na vituo mbali mbali vilivyopo nchini.
Katika hotuba yake Dkt. Mgwatu amewataka watumishi hao kuhakikisha kuwa wanashiriki mafunzo hayo kwa umakini mkubwa ili kuleta mabadiliko chanya kwa TEMESA na kuondoa kero mbalimbali zilizopo sasa, ikiwemo kero ya gharama kubwa za matengenezo ya magari, pikipiki na mitambo ya serikali na kuwataka watumishi hao kuondokana na wazabuni wanaouza vipuri na vilainishi vya magari kwa bei ghali isiyo ya soko.
“Mafunzo haya ni gharama na kwa hiyo haitakuwa jambo jema tukarudi katika vituo vyetu na kuendeleza mambo yale yale kwa mazoea. Tutakuwa hatujatenda haki kwa wananchi na kwa taifa kwa ujumla. Niwe mkweli kuwa nitachukua hatua kali pale nitakapoona mkoa au kituo hakifanyi vyema katika utendaji kazi wake” alisema Dr. Mgwatu.
Nae Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Matengenezo Mhandisi Sylvester Semfukwe amesema kuwa idara yake imeandaa mada mbali mbali kwa ajili ya mafunzo hayo zikiwemo: Tozo ya matengenezo ya magari, pikipiki na mitambo kwa kuzingatia muda halisi wa matengenezo, Mfumo mpya wa kuandaa taarifa za uzalishaji za kila mwezi, Namna ya kubaini vipuri bandia kwa njia ya kielektroniki, Masuala ya masoko na huduma kwa mteja pamoja na mwongozo wa uwandaaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2017/18.
Mafunzo hayo ya siku tano yaliyoanza jana katika Ukumbi wa TBA mkoani Dodoma, yanashirikisha jumla ya mikoa 19 yenye vituo vya TEMESA, yanatarajia kukamilika Ijumaa tarehe 20/01/2017. Aidha mafunzo hayo ni muendelezo wa mafunzo kama hayo yaliyofanyika mwezi Desemba, 2016 mkoani Dar es Salaam na yalishirikisha mikoa sita.

Ã¥ 

No comments:

Post a Comment

Pages