January 27, 2017

Madiwani waungana kudai posho mbili

NA MWANDISHI WETU, KIBONDO

MADIWANI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wa upinzani katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, juzi waliungana kumshinikiza Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo kuwalipa posho ya ziada iliyotokana na mchango wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).

UNHCR kupitia Shirika linalosimamia shughuli za mazingira kambi za Nduta na Mtendeli na vijiji vinavyozunguka kambi (REDESO) ilitoa fedha hizo kwa lengo la  kufanikisha uwasilishaji wa bajeti ya halmashauri hiyo  kwa mwaka wa fedha 2017/2018.

Hali hiyo ilisababisha kikao cha baraza la madiwani kuingia dosari na hatimaye kuvunjika kabla hakijaitimisha ajenda ya ziada ambayo awali  madiwani  waliafiki ijadiliwe  baada ya kupitisha makadirio ya bajeti kwa mwaka 2017/2018.

Baada ya kupitisha kwa  mapendekezo ya bajeti chini ya usimamizi wa Mkurugenzi Mtendaji,  Juma Mnwele, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri,  Phares Mzobona ambaye aliendesha kikao hicho aliwaeleza  wajumbe kuwa  ameombwa na asasi isiyo ya kiserikali kupata  fursa ya kukabidhi msaada huo kwa ajili ya kuhifadhi mazingira wilayani humo  pamoja na kusikiliza matokeo ya utafiti  wa hali ya misitu wilayani Kibondo tangu  mwaka 1974 hadi  sasa. Utafiti huo uliofanywa na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA).

Baada ya makabidhiano ya hundi ya Sh. Milioni 30 kwa Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Louis  Bura ambayo ilishuhudiwa  na wafadhili  kutoka UNHCR na Ofisa wa Idara ya Wakimbizi, Mkuu huyo wa Wilaya aliwaomba fedha hizo zitumike kwa malengo yaliyokubaliwa ambayo ni  kuhakikisha mazingira ya  Kibondo yanahifadhiwa na kutunzwa.

Fedha hizo ni kwa ajili ya kununua mizinga ya Nyuki kwa jamii zilizo kandokando ya Kambi ya Wakimbizi, Pikipiki nne  pamoja na  kompyuta moja kwa ajili ya shughuli za kiofisi kwa idara ya Maliasili.

Hali ilianza kubadilika baada ya mwakilishi kutoka REDESO kutangaza mbele ya wajumbe kwamba pamoja na msaada huo, wameleta pia hundi ya Shilingi Milioni 5.3 ikiwa ni sehemu ya mchango wao kwa baraza hilo maalumu la bajeti.

Madiwani hao walisema hawawezi kupolea taarifa ya utafiti huo hadi  watapogawana kwanza nyongeza ya fedha iliyoletwa na wafadhili hao.

Hoja hiyo ilitolewa na Diwani wa  Rugongwe, Evaristo Masigo (CCM) ambaye alimuomba Mwenyekiti kusimamisha kikao hicho hadi hapo watakapomaliza kugawana fedha hizo.

Misago aliungwa  mkono na Diwani wa Bitare, Julius Kihuna (ACT Wazalendo) ambaye alieleza  kutokuwa na imani na  watendaji wa halmashauri hiyo, hivyo ni vema fedha hiyo wagawiwe ndipo semina hiyo ianze vinginevyo  ni bora semina ifutwe.

Wakitolea ufafanuzi suala hilo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji,  Seif Salum na Mweka Hazina wa Halmashauri, Itendele Maduhu, walieleza  taratibu za kupokea fedha na namna zinavyotolewa,  hivyo kuwaeleza suala hilo sio la haraka na linahitaji muda.

Walisema pamoja na kwamba wafadhili hao wametoa fedha hizo, halmashauri  ilishatenga  pesa ya posho kwa mkutano huo na kwamba madiwani  watapewa posho zao kwa mujibu wa taratibu za vikao na kwamba hawataweza kupewa posho mbili kwa kikao kimoja kama wanavyoshinikiza.

Hata hivyo, ufafanuzi huo haukuzaa matunda na  kikao kilivunjika baada ya   madiwani wa CCM kuungana na wa upinzani  kuanza kupiga kelele na fujo, hali iliyosababisha  wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya kumshauri Mwenyekiti  kufunga kikao.

Alipotafutwa kutoa ufafanuzi kuhusu sakata hilo, Mkurugenzi Mtendaji Mnwele ambaye alikuwa safarini kuelekea Mwanza, alisema kitendo kilichotokea ni cha fedheha na aibu kwa madiwani ambao wamechaguliwa  kuwatetea na kuwawakilisha wananchi, ili kuondoa kero zinazowakabili.

“Sitasaini ama  ama kuruhusu kulipwa kwa posho hiyo kwani tayari halmashauri ilishatenga karibu Sh. Milioni 12 kwa ajili ya malipo ya posho ya wajumbe wote,” alisema Mnwele na kuongeza katika kuonyesha utawala bora na uwazi  fedha hizo zilizoletwa na wafadhili zitarejeshwa  kwa barua maalum, ili iwe fundisho kwa  madiwani ambao kila kukicha wamekuwa na ajenda ya kudai posho.

Naye  Mkuu wa Wilaya ya Kibondo,  Bura, alieleza kusikitishwa na  namna Mwenyekiti wa kikao hicho  alivyoshindwa kuendesha kikao na yeye kuungana na wajumbe kudai posho mara mbili.

Alisema huo ni mwendelezo wa tabia iliyoanza kuonyeshwa na baadhi ya madiwani chini ya Mwenyekiti wa Halmashauri, Saimon Kanguye hasa baada ya wiki iliyopita  wajumbe wa kamati ya Fedha, Uongozi na Mpango kugomea na kutoka nje ya kikao cha kujadili makisio ya bajeti ya Halmashauri  na kuwaacha wakuu wa Idara na Mkurugenzi  kushinikiza kulipwa posho  ya  Novemba, licha ya  Mkurugenzi kuwaeleza  malipo yao yako katika utaratibu wa mwisho kulipwa.

Hata hivyo,  Halmashauri ya Kibondo imepitisha  makisio ya bajeti kwa mwaka 2017/2018 ya Sh.Bilioni  29.4 ikijumuisha ruzuku kutoka Serikali Kuu, mapato ya ndani na michango ya wahisani.
Awali, Mnwele aliwaeleza wajumbe wa baraza hilo kwamba bajeti hiyo imejikita katika kuboresha maisha ya wananchi kwa kuangalia sekta ya elimu, afya, barabara, kilimo, maji na maendeleo ya vijana na wanawake.

No comments:

Post a Comment

Pages