January 17, 2017

MAMLAKA YA BANDARI YASHAURIWA KUFANYA TARATIBU ZA KURASIMISHA BANDARI BUBU NCHINI

Na Adili Mhina, Tanga

Mamlaka ya Bandari nchini imeshauriwa kuangalia taratibu za kurasimisha bandari bubu ili kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali pamoja na kuhakikisha bidhaa zinazopitishwa katika maeneo hayo zinakubalika kisheria. 

Ushauri huo umetolewa hivi karibuni na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri wakati  timu ya ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Tume ya Mipango ilipofanya ziara katika Bandari ya Tanga kwa lengo la kufanya ufuatiliaji na tahmnini ya shughuli zinazotekelezwa bandarini hapo. 

Mwanri alieleza umuhimu wa kurasimisha bandari bubu baada ya kupata taarifa kuwa katika Mkoa wa Tanga pekee kuna bandari bubu takriban 42 ambazo zinaendesha shughuli mbalimbali bila  ya usimamizi wa Mamlaka ya Bandari. 

Mwanri alieleza kuwa kwa sasa Serikali haiwezi kuendelea kufumbia macho suala hilo kwani licha ya Serikali kupoteza mapato yake wapo baadhi ya watu wanaotumia njia hizo nyakati za usiku kuendesha shughuli zinazoenda kinyume na kisheria na taratibu za nchi, hivyo kuchochea uhalifu.

“Kuna umuhimu mkubwa kuangalia shughuli zinazoendelea katika bandari bubu kwa kuwa wakati mwingine wafanya biashara wanaopaswa kulipa kodi wanatumia maeneo hayo kupitisha bidhaa bila kulipa kodi na wengine wanatumia bandari bubu kuendesha biashara haramu. Ni lazima kuanza kufanya utaratibu wa kurasimisha bandari hizo ili kuharakisha maendeleo ya nchi yetu,” alisema Mwanri.

Pamoja na hayo, Mwari alitembelea maeneo ya Bandari ya Tanga na kushuhudia shughuli mbalimbali zikiendelea ikiwa ni pamoja na ujenzi wa gati namba 2 ikiwa ni moja ya malengo katika kuimarisha huduma za upakiaji na upakuaji wa mizigo bandarini hapo. 

Awali, Mhandasi wa Bandari hiyo Bw. Saleh Sapi alieleza kuwa Bandari ya Tanga inapokea tani laki mbili za mizigo kwa mwezi ambapo  bidhaa kubwa zinazoingizwa kutoka nje ni malighafi ya kutengenezea saruji wakati bidhaa zinazosafirishwa kwenda nje ni kahawa, mkonge, pamoja na mbao ambazo kwa sasa kibali chake kimesitishwa kwa muda. 

Mhandisi huyo alieleza kuwa  Bandari ya Tanga haina eneo lenye ukubwa wa kutosha kwa ajili ya kutekeleza huduma zake kwa ufanisi huku kina cha maji kikiwa ni mita nne kitu kinachopelekea meli kubwa kushindwa kufika kwenye gati za bandari na badala yake matishari hutumika kubeba mizigo hiyo. 

Mhandisi Sapi alifafanua kuwa kutokana na changamoto hiyo nguvu kubwa inaelekezwa katika kuangalia namna ya kujenga bandari kubwa ya kisasa katika eneo la Mwambani ambapo kuna kina cha maji kinatosha kuhudumia meli kubwa na pia kuna eneo la kutosha shughuli mbalimbali za bandarini.

No comments:

Post a Comment

Pages