WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa ameuagiza uongozi Wazara wa Elimu Sayansi na Telnolojia pamoja na
Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwenda mkoani
Mtwara kufanya uchunguzi ili kubaini sababu zilizosababisha shule tisa za
mwisho katika matokeo ya kidato cha pili kutoka mkoani humo.
Pia ameziagiza
halmashauri nchini kushirikiana na Idara ya Ukaguzi ili kuhakikisha
wanawasimamia vizuri walimu jambo litakalowezesha kuboresha ufundishaji na
hatimaye kupata matokeo mazuri.
Waziri Mkuu ametoa
agizo hilo leo (Jumanne, Januari 17, 2017) wakati akizungumza na watumishi na
wananchi wa mkoa wa Katavi alipowasili Ikulu ndogo ya Mpanda kwa ajili ya
kufungua duka la dawa la Bohari Kuu ya Dawa (MSD) katika hospitali ya Manispaa
ya Mpanda.
Kwa mujibu wa matokeo
hayo kati ya shule 10 za sekondari zilizofanya vibaya kwenye mtihani huo, tisa
zinatoka katika Mkoa wa Mtwara na moja Tanga. Shule za Mtwara zilizofanya
vibaya ni Chingungwe, Malocho, Naputa, Chanikanguo, Mtiniko, Michiga, Msimbati,
Salama na Lukodoka huku ya Tanga ikiwa ni Nywelo.
“Viongozi wa Wizara ya
Elimu Sayansi na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (TAMISEMI) waende Mtwara wakafuatilie kwa kina wajue kuna nini hadi
shule tisa kati ya 10 zilizofanya vibaya katika matokeo ya mitihani ya kidato
cha pili mwaka jana zitoke huko,” amesisitiza.
Mbali na kuuagiza
huongozi wa wizara hizo kwenda mkoani Mtwara pia Waziri Mkuu amewataka
wasimamie vizuri mikoa ambayo awali ilikuwa na matokeo mabaya na sasa inafanya
vizuri na wahakikishe shule za mikoa hiyo hazishuki na badala yake ziendelee
kupata matokeo mazuri zaidi.
Awali, akisoma taarifa
ya mkoa huo, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali Mstaafu, Raphael Muhuga
alisema katika matokeo ya mtihani kidato cha pili ya mwaka jana mkoa wake
ulishika nafasi ya pili kitaifa ukiongozwa na mkoa wa Geita.
Alisema kwa sasa
wanajipanga kuhakikisha katika mitihani ya mwaka huu wanashika nafasi ya kwanza
kitaifa, hivyo alitoa wito kwa watendaji wa Idara ya Elimu, wakuu wa shule,
wazazi na walezi kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha malengo hayo yanafanikiwa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, JANUARI 17,
2017.
No comments:
Post a Comment