January 27, 2017

RC RUKWA AWACHARUKIA WAKURUGENZI KUHUSUTASAF

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen, akizungumza na mkazi  wa Nkasi Mkoani Rukwa alipozitembelea kaya za walionufaika na mpango wa TASAF.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amewaagiza wakurugenzi, waratibu wa Tasaf, watendaji wa kata, watendaji wa vijiji na wenyeviti wa vijiji Mkoani humo kuhakikisha kwamba haki inapatikana katika kufanya mchujo kwa zile kaya ambazo hazistahili kuingizwa katika mpango wa kuzinusuru kaya masikini (TASAF)

Ametoa agizo hilo baada ya kufanya ziara yake ya siku ya nne katika wilaya za kalambo na Nkasi Mkoani humo kwa kuzitembelea kaya za walionufaika na mpango wa TASAF ambao bado wanaendelea kunufaika na wale ambao waliondolewa katika mpango huo baada ya kukosa vigezo na hatimae kutakiwa kurudisha pesa hizo.

“nimezunguka nimebaini kuwa zoezi hili limekuwa likifanyika hovyo hovyo, hakuna umakini, hakuna usimamizi, hakuna ufuatiliaji, matokeo yake kwenye mradi wameingizwa watu wenye sifa na wasio na sifa, Wakurugenzi na waratibu wasimamie zoezi hili, wasiwaachie wenyeviti na watendaji wa vijiji peke yao katika hili,”

Zelote Stephen alifanya ziara hiyo ili kujiridhisha kuwa kaya ambazo hazistahili kuingizwa katika mpango wa TASAF wanatendewa haki katika kuondolewa kwenye mpango huo lakini pia kujua sababu zilizopelekea kaya hizo kuingizwa kwenye mpango bila ya kuwa na vigezo na kuachwa kaya zenye vigezo.

“Wale wote ambao hawana vigezo na kweli ionekane kwamba hawana vigezo vya kuwepo basi watolewe kwasababau sehemu zingine utakuta kwenye mpango huo wameingizwa wastaafu, mke wa mwalimu, mjumbe wa smc yumo humo humo, hii haifai,” Zelote alifafanua.

Katika ziara yake hiyo iliyolenga kufuatilia mchujo wa kaya hizo, Zelote Stephen alibaini kuwa wakurugenzi pamoja na waratibu wa TASAF wilaya wanakosa umakini katika kuzifanya shughuli zao na hatimae kubaki maofisini kusubiri ripoti zitokazo vijijini bila ya kufuatilia kwa kina kwa kufika katika maeneo husika ili kujua hali halisi.

“Mimi nina taarifa kwamba fedha za ufuatiliaji wa TASAF zikifika tu katika Ofisi ya Mkurugenzi, kama zimefika asubuhi basi mchana tu hakuna senti tano, zote zimeshanyanganyiwa na hatimae makusudio ya fedha zile hayatimii na ufuatiliaji haufanywi,” Alisisitiza.

Nae mratibu wa TASAF Mkoa wa Rukwa, James Kapenulo aliongeza kuwa kaya zote ambazo zilinufaika na TASAF kwa kuwa na mashamba na nyumba nzuri ambazo kabla ya TASAF hawakuwa nazo, familia hizo ndio ziwe za mfano na ziendelee kuwezeshwa ili tathmini itakapokuja kufanywa ioneshe hali halisi ya mafanikio ya mpango huo.

“Hatuwezi tukaendelea kuwaweka wale ambao wakipewa pesa za TASAF wanaishia kwenye vilabu vya pombe na kumuacha yule ambae akipewa pesa hizi ananunua kuku au mbuzi au bati na kuwapeleka watoto shuleni, hayo sio madhumuni ya mpango huu, huyu aliyefanikiwa baada ya TASAF ndiye ametoka weye umaskini.

Naye mnufaika wa TASAF aliyetolewa kwenye mpango huo Mathias Mwanakatwe alimshukuru Mkuu wa wa Mkoa kwa kuweza kuliona hilo na kulishughulikia kabla hali haijawa mbaya zaidi kwa wale wananchi wenye wivu na chuki kwa wale waliofanikiwa kutokana na kuwepo kwa mpango huo wa TASAF.

Kaya a 550 mbazo hazistahili kuwepo katika mpango huo kwa Mkoa wa Rukwa.

No comments:

Post a Comment

Pages