February 01, 2017

Serikali Yaendelea na Usitisha wa Shughuli za Uvuvi Ndani Ya Pori la Akiba la Selous

Na Lilian Lundo, MAELEZO–Dodoma

Serikali itaendelea kutoruhusu uvuvi kufanyika ndani ya Pori la Akiba la Selous kutokana na ukiukwaji wa taratibu zilizokuwa zimewekwa wa kuingia ndani ya  hifadhi hiyo.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhandisi Ramo Makani ameyasema hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Rufiji Mohamed Mchengerwa juu ya hatua ambazo Serikali inazichukua kutoa ridhaa kwa wananchi waishio maeneo ya hifadhi kupata ruhusa kisheria kuweza kuvua samaki.

“Mwaka 1994, wananchi wa Kata ya Mwaseni, Mloka, Ngoroka na Kipungila Wilaya ya Rufiji waliruhusiwa kuingia ndani ya Pori la Akiba Selous na kuvua Samaki. Hata hivyo, baadhi ya wanavijiji walikiuka taratibu zilizokuwa zimewekwa kwa kuingia ndani ya hifadhi bila kujiandikisha na kuvua samaki kinyume cha sheria,” alifafanua Mhandisi Makani.

Aliendelea kwa kusema kuwa baadhi ya wavuvi walibainika kujihusisha na vitendo vya ujangili wa wanyamapori, uvuvi haramu wa kutumia sumu, ukataji miti ovyo kwa ajili ya kukausha samaki na kutengeneza mitumbwi pamoja na uharibifu wa mazingira uliotokana na uchomaji wa moto ovyo kinyume cha sheria.

Mhandisi Makani amesema kuwa kwa kuzingatia hali ya usalama katika maeneo ya uhifadhi wa wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kutoruhusu uvuvi kufanyika ndani ya Pori la Akiba Selous.

Aidha Wizara inawashauri wananchi wa Kata za Mwaseni, Mloka na nyinginezo zilizo jirani kutumia mabwawa mengine yaliyoko nje ya Pori hilo yenye fursa kubwa kwa kufanya shughuli za uvuvi.

Mabwawa ambayo wananchi wameshauriwa kuyatumia ni Bwawa la Zumbi lililoko vijiji vya Nyaminywili, Kipugira na Kipo, Bwawa la Ruwe lililopo Mkongo, Lugongo lililopo kijiji cha Mtanza na Bwawa la Zimbwini lililopo Mji wa Kibiti.

Mabwawa hayo ya Mto Rufiji yatatoa fursa ya shughuli za uvuvi hivyo kusaidia kuinua kipato cha wananchi.

Vile vile Mhandisi Makani amesema kuwa, Wizara hiyo kwa kutambua mahitaji ya wananchi katika maeneo hayo ya kufanyia kazi na kujiletea maendeleo kiuchumi na kijamii. Wizara hiyo inaendelea kushauriana na Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji kuhusu namna ya kutekeleza mpango wa kuwajengea mabwawa ya samaki ili pamoja na mabwawa ya asili yaliyopo yawawezeshe kufanya shughuli za uvuvi endelevu.

No comments:

Post a Comment

Pages