February 01, 2017

Vyuo Vikuu Vyaaagizwa Kutotoza Ada kwa Fedha za Kigeni kwa Watanzania

Na: Lilian Lundo, MAELEZO-Dodoma

Vyuo Vikuu hapa Nchini vimeagizwa kuacha mara moja kutoza ada kwa fedha za kigeni kwa wanafunzi ambao ni watanzania.

Agizo hilo limetolewa leo Bungeni, Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhandisi Stella Manyanya alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge Jaku Hashimu Ayoub kwamba kumekuwa na malalamiko ya wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania ambao ni wazawa kulipishwa ada ya masomo yao kwa fedha za kigeni badala ya fedha za Kitanzania.

“Sarafu inayotakiwa kutumika Tanzania ni shilingi ya Kitanzania kwa mujibu wa kifungu cha 25 na 26 cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ya mwaka 2006. Aidha, kwa Tanzania malipo ya kitu au huduma yoyote inapaswa kulipwa kwa shilingi ya Kitanzania kama ilivyoainishwa kwenye kifungu cha 28 cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, 2006,” alifafanua Mhandisi Manyanya.

Aliendelea kwa kusema kuwa japo Wizara haijapokea malalamiko yoyote ya kutozwa fedha za kigeni kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu tangu itoe agizo kama hilo kwa wamiliki wa vyuo Septemba 07, 2016.

Hivyo basi kwa mara nyingine Mhandisi Manyanya ameviagiza vyuo ambavyo bado vinatoza wanafunzi Watanzania fedha za kigeni kuacha mara moja kwani vyuo hivyo vimeelekezwa kutoza wananchi wa Kitanzania kwa pesa ya Kitanzania.

Aidha Mhandisi Manyanya  amewataka watanzania kutoa taarifa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ikiwa kuna Chuo chochote kinachotoza ada kwa Watanzania kwa fedha za Kigeni ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika.

No comments:

Post a Comment

Pages