Mgeni
Rasmi Bw. Maduka Paul Kessy, Kaimu Katibu Mtendaji, Tume ya Mipango
(aliyesimama) akitoa hotuba ya ufunguzi wa mafunzo kuhusu Mwongozo wa Usimamizi
wa Uwekezaji wa Umma kwa washiriki kutoka Idara za Sera na Mipango za Wizara, Idara zinazojitegemea na Wakala za
Serikali.
Wengine ni Bi. Lorah Madete, Kaimu Naibu Katibu Mtendaji, Klasta ya Uchumi
Jumla, Tume ya Mipango (kulia) na Bw. John Mduma, Mhadhiri Mwandamizi, Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (kushoto).
Washiriki wa Mafunzo wakimsikiliza kwa makini Mgeni Rasmi (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Dkt. Lorah Madete, Kaimu Naibu Katibu Mtendaji, Klasta ya Uchumi Jumla, Tume ya Mipango (aliyesimama), akitoa neno kwa washiriki wa mafunzo kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi ili afungue mafunzo hayo ya siku tano. Waliokaa ni Bw. Maduka Paul Kessy, Kaimu Katibu Mtendaji, Tume ya Mipango (katikati) na Bw. John Mduma, Mhadhiri Mwanamizi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Dkt. John Mduma, Mhadhiri Mwandamizi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (aliyesimama), akitoa neno kwa washiriki wa mafunzo mara baada ya mafunzo hayo kufunguliwa rasmi.
Washiriki wa mafunzo kuhusu Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma kutoka Idara za Sera na Mipango za Wizara, Idara zinazojitegemea na Wakala za Serikali pamoja na wawezeshaji wa mafunzo wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni Rasmi mara baada ya ufunguzi wa mafunzo hayo.
Na Thomas Nyindo.
Maofisa wa Idara za Sera na Mipango kutoka Wizara, Idara na Wakala za
Serikali wametakiwa kuongeza ufanisi na ubunifu katika kuandaa na kusimamia
miradi ya maendeleo ili kuharakisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.
Kauli hiyo imetolewa leo na Kaimu Katibu Mtendaji
wa Tume ya Mipango, Bw. Maduka Kessy wakati akifungua mafunzo ya Mwongozo wa
Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma yanayoendelea katika ukumbi wa Chuo cha Mipango
Dodoma.
Kessy alieleza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea
uwezo maofisa wanaosimamia masuala ya Sera na Mipango katika kuibua na
kutekeleza miradi ya maendeleo, hususan, ile inayogharamiwa kwa fedha za
Serikali ili kufanya Tanzania kuingia kwenye nchi za kipato cha kati kama
ilivyoaninishwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo.
“Mipango ya maendeleo tunayojiwekea, kama taifa, inapaswa
kutafsiriwa katika miradi na programu za utekelezaji, hivyo mafunzo haya
yatatusaidia kuongeza ufanisi, ubunifu na uwajibikaji katika kuandaa miradi na
kusimamia miradi yenye tija kwa wananchi,” alisema Kessy.
Aliwasisitiza washiriki wa mafunzo hayo kuwa wao ni
miongoni mwa wadau muhimu katika kuifanya Tanzania ipige hatua za maendeleo kwa
kuwa ndio wanaohusika katika kupanga na kusimamia utekelezaji wa miradi ya
maendeleo.
Aidha, Kessy alieleza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia
washiriki kuongeza ufanisi na ubunifu katika kuchagua miradi, kutafuta fedha za
ugharamiaji na kuboresha uratibu wa kufungamanisha uwekezaji wa umma kwa
kubainisha hatua za kufuata katika kujumuisha miradi ya maendeleo katika bajeti
za maendeleo.
“Mwongozo huu utawasaidia kufanya maamuzi katika kuchagua
miradi sahihi ya uwekezaji katika sekta ya umma na kuhakikisha ufanisi katika
utekelezaji wake. Sote tunafahamu kuwa azma yetu ya maendeleo kitaifa ni
kufikia uchumi wa kipato cha kati ifikapo 2025,” alisema.
Kaimu Katibu Mtendaji huyo alieleza kuwa zipo changamoto
zinazokabili usimamizi wa miradi ya maendeleo, kuanzia hatua ya kubuni,
kutekeleza hadi kukamilisha miradi hiyo. Kwa hiyo Mwongozo wa Usimamizi wa
Uwekezaji waRasilimali za Umma ni mojawapo ya maandiko muhimu ambayo yamebuniwa
kukabiliana na changamoto hizo.
No comments:
Post a Comment