Na Nuru Juma - MAELEZO
Shirika la Mkulima Market linatarajia kufanya soko la wazi (Mkulima soko) Jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es salaam(UDSM) Aprili 12 mpaka 15 mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Mratibu wa Mkulima Market Bi Vicensia Shule wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu soko hilo la wazi leo, jijini Dar es salaam.
Vicensia Shule amesema kwamba, maonesho hayo yatahusisha mauzo ya bidhaa mbalimbali za kilimo, uvuvi na ufugaji. Aidha amekaribisha wadau mbalimbali kutoka katika taasisi za umma, sekta binafsi, wafanyabiashara na makundi mbalimbali kushiriki kuuza, kuonesha, kutoa huduma na elimu kuhusu ukulima.
Hata hivyo alitoa gharama kwa watakaohitaji kushiriki kwa siku zote nne kama ifuatavyo, banda la pamoja (meza 1 na kiti 1) Sh. 50,000, robo banda (meza 2 na viti 2) Sh. 100,000, nusu banda (meza 4 na viti 8) Sh.175000, banda zima Sh. 350000 na kutumia eneo la wazi Sh. 125,000, aidha kwa wale watakaotoa huduma za chakula, vinywaji, michezo ya watoto watalipia gharama ya kutumia eneo la wazi.
Nae, Mratibu Msaidizi wa shirika hilo Bw Vicent Mirumbe ametoa wito kwa vijana kushiriki maonyesho hayo ambayo yatawasaidia kuwainua kiuchumi na kutowategemea wazazi au walezi.
“Vijana wengi wapo majumbani wakitegemea wazazi au walezi wao kuwawezesha katika mahitaji yao ya kila siku. Mkulima Market ni fursa nzuri itakayowawezesha vijana wasio na ajira kujiajiri kupitia soko hilo la wazi.” Alifafanua Mirumbe.
Mkulima Market pia imeandaa masoko mengine ya wazi katika kipindi cha sikukuu kubwa tatu ambazo ni Eid al Fitr Juni 21 hadi 24 mwaka huu, Eid al Hadj Agosti 29 hadi Septemba 1 mwaka huu na Krismasi Desemba 20 hadi 24 mwaka huu, ambapo katika soko la wazi la Desemba kutakua na Tamasha la Maembe (Mango Festival).
No comments:
Post a Comment