June 30, 2017

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam yapongezwa kwa kufungua kituo cha Urithi wa Ubunifu Majengo na Utalii

Na Lorietha Laurence- WHUSM.

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bibi. Nuru Millao  ameupongeza Uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kulifanya jengo la Old Boma kuwa Kituo cha Urithi wa Ubunifu wa Majengo na Utalii (DARCHI).

Akizungumza katika hafla ya kufungua  kituo  hicho leo Jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt.Harrison Mwakyembe, Millao alisema hatua hiyo inadhihirisha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kuwa utamaduni wa Mtanzania unadumishwa na kukuzwa. 

“Ni dhahiri kuwa wananchi  wataweza kufahamu umuhimu wa kutunza na kuhifadhi majengo ya kale kutokana na elimu watakayoipata kupitia kituo hiki katika kukuza utamaduni ” alisema Millao.

Aidha alitoa wito kwa kwa Jumuiya ya Wasanifu Majengo Tanzania kuendelea kushirikiana na Taasisi za ndani na nje ya nchi katika kutekeleza mipango ya kutunza majengo na sehemu za kale ili kuhifadhi historia na utamaduni wa Mtanzania.

Pia amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa katika Jiji la Dar es Salaam kusimamia sheria kwa  kushughulia kero mbalimbali zinazotokana na udhaifu wa sheria za kuendeleza majengo ya kale.

Naye  Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Bw.Isaya Mwita ameeleza kuwa kufunguliwa kwa  kituo hiko ni fursa ya kukuza pato la uchumi wa nchi kupitia mapato ya watalii watakaokitembelea.

 “Tayari tumeweka mipango mbalimbali ya kuhakikisha Jiji letu la Dar es Salaam linakuwa sehemu ya Utalii kwa kutoa mafunzo kwa madereva Taxii ambao wanahusika katika kuwasafirisha  watalii ili wawe na uelewa zaidi kuhusu kituo hiki ” alisema Mstahiki Meya Bw.Mwita.

Kwa Upande wake Balozi wa Umoja wa Ulaya Nchini Mhe.Roeland Van De Geer amesema ofisi yake iko tayari kushirikiana kwa karibu na Jiji la Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla katika kuleta maendeleo.

No comments:

Post a Comment

Pages