June 24, 2017

Idara ya Habar Yapokea Kamusi Kuu Kuenzi Kiswahili

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Dk. Hassan Abbasi (kushoto) na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara hiyo Sehemu ya Huduma za Habari na Picha, Rodney Thadeus, wakionyesha nakala za Kamusi Kuu ya Kiswahili toleo la pili kwa Maofisa Habari wa Idara hiyo (hawapo pichani) baada ya makabidhiano ya kamusi hizo jijini Dar es Salaam jana. (Picha na Frank Shija, Maelezo).

Na Lilian Lundo, MAELEZO

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Dkt. Hassan Abbasi leo amekabidhi Kamusi Kuu ya Kiswahili kwa watumishi wa Idara ya Habari (MAELEZO) katika ofisi za Idara hiyo zilizopo Jijini, Dar es Salaam.

Dkt. Abbasi amesema mojawapo ya jukumu la idara hiyo ni kuhabarisha Umma, hivyo kamusi hiyo itakuwa msaada mkubwa katika uandishi wa habari za kila siku. 

“Kamusi hii ina maneno mpaka yaliyoaanza kutumika hivi karibuni, kama vile bajaji. Pia ina misamiati mingi ambayo haitumiki, hivyo kwa kuitumia kamusi hii kutaongeza idadi ya misamiati ya Kiswahili kwa watumiaji wa lugha ya Kiswahili,” amesema Dkt. Abbasi.

Ameitaka Idara ya Habari kuitumia Kamusi hiyo kama nyenzo muhimu katika kutangaza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi pamoja na kutumia misamiati mipya.

Hata hivyo, Dkt. Abbasi alitoa ufafanuzi wa neno Mbashara kuwa ndio neno sahihi lenye maana ya inayorushwa hewani moja kwa moja au kuonwa kwa wakati huohuo kupitia redio na televisheni na sio Mubashara kama ambavyo limekuwa likitumika na vyombo vingi vya habari.

Aidha alitoa mfano wa misamiati mingine iliyopo katika kamusi hiyo kuwa ni neno sharubati linalomaanisha kinywaji laini ambacho hutengenezwa kwa maji ya matunda au sukari na kisha kutiwa rangi. Neno lingine ni mnyange ambalo linamaana ya mtu mwenye mwonekano mzuri, maridadi, mtanashati, mrembo, mlimbwende. 

Dkt. Abbas amewataka watumishi wa idara hiyo kuwa chemchem ya kutumia misamiati iliyoko katika kamusi hiyo ili kukuza lugha ya Kiswahili.

Kamusi Kuu ya Kiswahili ilizinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Juni 19, mwaka huu, Bungeni Mjini Dodoma.

No comments:

Post a Comment

Pages