Na:
Mwandishi Wetu- MAELEZO
Kasi ya ukuaji wa uchumi nchini
imeendelea kuimarika ambapo Tanzania imetajwa kuwa ni miongoni mwa nchi tano
barani Afrika zilizoongoza
kwa kuwa na kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi.
Akiwasilisha hotuba ya bajeti kwa
mwaka 2017/2018 bungeni leo, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango
amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Tanzania inashika nafasi ya pili kwa ukuaji
wa uchumi ambapo uchumi wake unakuwa kwa asilimia 7.1 nyuma ya Ivory Coast
ambayo yenyewe uchumi wake unakuwa kwa asilimia 7.9.
Nchi zingine zilizokuwa na kasi nzuri ya ukuaji wa
uchumi ni Senegal (asilimia 6.6), Djibouti (asilimia 6.5) na Ethiopia (asilimia
6.5).
“Jarida la Benki ya Dunia (Tanzania Economic
Update) lililochapishwa Aprili 2017 linabainisha waziwazi kuwa uchumi wa Taifa
ni imara kwa kuangalia viashiria mbalimbali kama ukuaji wa uchumi, mfumuko wa
bei, urari wa biashara, akiba katika fedha za kigeni na thamani ya shilingi”.
Alieleza Waziri Mpango kwa kunukuu takwimu za Benki ya Dunia juu ya ukuaji wa
uchumi nchini.
Alisema kuwa pamoja na mafanikio yaliyoelezwa
lakini bado kumekuwa na mijadala kuhusu afya ya uchumi wa Taifa hususan ukwasi
katika uchumi, kufungwa kwa biashara, na madai kwamba sekta binafsi imepoteza
matumaini na kujiamini (private sector confidence) na kwamba hali hiyo imesababishwa na mambo
mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa mikopo chefuchefu katika mabenki.
“Takwimu pia
zinaonesha kuwa ukwasi wa mabenki ulianza kutetereka kutokana na kuongezeka kwa
mikopo chefuchefu kutoka asilimia 8.3 mwezi Machi 2016 hadi asilimia 10.9 Machi
2017 ikilinganishwa na kiwango kinachohitajika cha asilimia 5.
Alifafanua
kuwa Mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka kidogo kwa asilimia 3.7 katika kipindi
cha mwaka ulioishia Machi 2017 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 23.6
katika kipindi kama hicho mwaka 2016.
“Kupungua kwa
kiwango cha ukuaji huo kulitokana kwa kiasi kikubwa na kuyumba kwa biashara
duniani ambako kuliathiri nchi nyingi duniani ikiwemo Tanzania”. Alifafanua
Dkt. Mpango.
Aidha katika
bajeti hiyo, aliyataka mabenki yote nchini kusimamia kwa makini taratibu za
kibenki katika utoaji wa mikopo.
Alieleza kuwa
ili kuimarisha ukwasi, Serikali kupitia Benki Kuu imechukua hatua mbalimbali
ikiwa ni pamoja na kupunguza riba ambazo benki za biashara hukopa kutoka Benki
Kuu (Discount Rate) ili kuongeza ukwasi katika benki za biashara na hivyo kuziwezesha kukopa kwa gharama nafuu
zaidi.
Kwa mujibu wa
Waziri Mpango, riba hiyo imepunguzwa kutoka asilimia 16.0 iliyokuwa ikitumika
tangu mwezi Novemba 2013 hadi asilimia 12.0 ambayo imeanza kutumika rasmi
tarehe 6 Machi 2017.
Aidha, ameeleza
kuwa katika kuimarisha zaidi soko la fedha nchini, Benki Kuu ilipunguza kiwango
cha amana ambacho benki za biashara zinatakiwa kuhifadhi Benki kuu kama dhamana
(Statutory Minimum Reserve Requirement – SMR) kutoka asilimia 10.0 hadi
asilimia 8.0 ili kuziwezesha benki za biashara kuwa na ukwasi zaidi kwa ajili
ya kukopesha sekta binafsi na kwamba hatua hiyo imeanza kutumika rasmi mwezi
Aprili 2017..
“Ni matumaini
ya Serikali kuwa hatua hizi zitaziwezesha benki za biashara nchini kuongeza
ukwasi wa kutosha kuwakopesha wananchi kwa riba nafuu”. Alieleza.
Katika eneo la mazingira ya
kufanya biashara, Waziri mpango alieleza kuwa Serikali imeanza kuona viashiria bora zaidi katika eneo la
kuboresha mazingira ya biashara.
Amesema kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia ya
mwaka 2017 ilionesha kuwa, Tanzania ilikuwa nchi ya 132 kwa urahisi wa kufanya
biashara ikiwa imepiga hatua kwa nafasi 12 kutoka nafasi ya 144 mwaka 2016.
Aidha, kwa mujibu wa taarifa ya “Fahirisi ya Uwekezaji
Afrika ya mwaka 2016” (Africa Investment Index, 2016) iliyotolewa na taasisi ya
“Quantum Global Research Lab” ya
Uingereza, Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza miongoni mwa nchi za Afrika
Mashariki kwa kuvutia uwekezaji na ya nane kwa Afrika, ikiwa imepiga hatua
kutoka nafasi ya 19 mwaka 2015.
No comments:
Post a Comment