Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, itakutana tena kwa dharura siku ya Jumanne Julai 04, 2017 kwenye ofisi za TFF, Dar es Salaam ambako pamoja na ajenda nyingine, itatathmini mwenendo wa kazi za Kamati ya Uchaguzi ya shirikisho.
Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Salum Madadi amesema kwamba kamati hiyo ya utendaji inakutana kwa dharura kwa mujibu wa Ibara ya 35 (1) ya Katiba ya TFF inayosomwa pamoja na Ibara ya 35 (6).
Kamati hiyo inakutana baada ya barua ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Wakili Revocatus Kuuli kudai kwamba kuna mitazamo tofauti inayosababisha kutokamilisha majukumu yao kwa asilimia 100 kutoka hatua moja hadi nyingine wakati huu wa mchakato wa uchaguzi.
Kutokana na tofauti hizo, Wakili Kuuli kwa kutumia nafasi ya kofia ya uenyekiti, amesitisha kwa muda mchakato wa uchaguzi hadi hapo hali ya mambo itakapowekwa sawa na Kamati ya Utendaji inayotarajiwa kukutana Jumanne wiki inayoanza kesho.
Hii ni mara ya pili kwa kamati kukutana ndani ya wiki moja kwani Jumamosi Julai 01, 2017 kamati hiyo ya utendaji ilikutana na kufanya uamuzi wa kumpitisha Wallace Karia kuwa Kaimu Rais wa shirikisho.
Kadhalika, Kamati hiyo ya Utendaji ya TFF, ilimpitisha Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi kuwa Kaimu Katibu Mkuu wa TFF.
Viongozi hao watakaimu nafasi hizo tajwa hadi hapo mahakama itakavyoamua kuhusu kesi zinazowakabili kwa sasa Rais wa TFF, Jamal Malinzi na Katibu Mkuu, Mwesigwa Selestine.
………………………………………………………………………………………….
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA
No comments:
Post a Comment