July 05, 2017

WAZIRI MKUU MHE.MAJALIWA AELEKEZA BARAZA LA MICHEZO TANZANIA(BMT) LIVUNJWE

Na Daudi Manongi, MAELEZO,DODOMA

Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa ameelekeza  Baraza la Michezo Tanzania(BMT) livunjwe na shughuli zake kufanywa na Sekretarieti hadi hapo Baraza jipya litakapoundwa tena.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo Bungeni Mjini Dodoma wakati akisoma hotuba ya  kuhairisha mkutano wa saba wa Bunge la kumi na moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Serikali ya awamu ya tano haitafumbia macho usimamizi mbovu na utawala wa michezo usiojali  maslahi ya Taifa,Serikali imeazimia kuimarisha utendaji kwa vyombo vya michezo nchini ili kila mwenye dhamana awajibike ipasavyo”,Aliongeza Mhe.Majaliwa.

Aidha katika hotuba yake amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dk John Pombe Magufuli kwa kuunga mkono jitihada za michezo nchini kwa dhamira yake ya kujenga Uwanja mkubwa wa Michezo hapa mjini  Dodoma kwa kushawishi mataifa rafiki kama vile Moroco ambao wanajenga uwanja huo.

Pia amesema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa michezo kwa Afya,umoja wa kitaifa na kama fursa ya ajira kwa vijana wetu ambapo ivi karibuni  mkoani Mwanza yamehitimishwa mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA  yaliyoibua vipaji na   hamasa kubwa iliyo miongoni mwa vijana nchini.

“Tutaendelea kuratibu  michezo shuleni,ikiwa ni pamoja na kusimamia ufundishaji wa michezo kama somo,maelekezo yetu ni kwamba kila mkoa uwe na shule angalau mbili zenye mchepuo wa michezo na walimu wenye sifa stahiki za kufundisha michezo,Ameeleza Mhe.Majaliwa.

Waziri Mkuu Majaliwa pia ameipongeza kwa dhati timu ya Serengeti Boys kwa kutoa upinzani mkubwa kwenye mashindano ya shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika na kuweka msisitizo kwa Chama cha Mpira nchini(TFF) kuendelea kuwatunza vijana hao.

“Msisitizo wangu kwa TFF ni kuendelea kuwatunza vijana hao na kusimamia vilabu vya michezo nchini, kuwekeza kwenye soka la vijana ili kujenga timu imara kwa miaka michache ijayo”,Aliongeza Mhe.Majaliwa.

No comments:

Post a Comment

Pages