WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mataifa ya
Afrika yanatakiwa yaandae maarifa, vitendea kazi na rasilimali watu watakaoweza
kusimamia na kuendeleza ipasavyo sekta ya madini na kuleta tija kwa Taifa
husika na wananchi kwa ujumla.
Amesema taarifa za kijiolojia zinaonesha kuwa Afrika
ni Bara lenye utajiri mkubwa wa rasilimali madini huku sehemu kubwa ya madini
hayo yakiwa bado hayajaanza au yako kwenye hatua mbalimbali za uendelezaji.
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Septemba 14, 2017)
alipofungua mkutano wa 37 wa Baraza la Uongozi wa Kituo cha Madini na
Jiosayansi cha Afrika (AMGC) uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa kituo
hicho mkoani Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amesema rasilimali za madini ilizopo Barani
Afrika inaweza kuwa ni chanzo kikubwa cha kusukuma maendeleo ya kiuchumi na
kijamii katika nchi nyingi iwapo itasimamiwa vizuri.
Ametolea mfano Tanzania ambayo licha ya kuwa na
utajiri mkubwa wa madini ya dhahabu, almasi, chuma, madini ya vito kama
tanzanite lakini mchango wa sekta ya madini ni asilimia 4.8 ya pato ghafi la
Taifa.
“Changamoto kuu kwa sasa ni kwa jinsi gani tunaweza
kuwa na sekta ya madini inayotoa mchango stahiki katika nchi husika pamoja na kusimamia
sekta hii kwa kuwafanya wananchi wetu hususan katika maeneo yenye rasilimali
wakanufaika na kuona fahari badala ya kuacha mashimo, umasikini na mateso kwa
wananchi.”
Amesema lengo la kuanzishwa kwa kituo hicho ambacho
leo kimetimiza miaka 40 ni kuhakikisha sekta ya madini inawajibika kuleta
maendeleo ya kijamii na uchumi pia ikijali masuala ya mazingira, hivyo ni vema
kikatumika kama ilivyokusudiwa.
Waziri Mkuu amesema kituo hicho kikitumika vema kwa
mujibu wa kusudia la uanzishwaji wake kinaweza kuleta tija kubwa kwenye sekta
ya uchumbaji wa madini, uongezaji wa thamani na usimamizi wa sekta.
Amesema kituo hicho ni moja kati ya taasisi chache
duniani yenye teknolojia za kisasa ambazo zinaweza kusaidia kufanya uchambuzi
wa miamba na madini yaliyimo. “Pia ni sehemu ambayo unaweza kupata huduma za
ushauri na kusaidia teknolojia utakayoweza kutumia ili kufanya uzalishaji wa
madini mbalimbali.”
Hivyo amewakumbusha wajumbe na wanachama wa AMGC kuwa
kituo hicho hawajakitumia ipasavyo ni vema kikatumika ili kupata tija kwenye
uendelezaji na usimamizi wa madini, ambapo ameiagiza Bodi iandae mpango
utakaoziwezesha nchi wasnachama kukitumia.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati na Madini,
Dkt. Medard Kalemani amesema kwa sasa kituo hicho kinakabiliwa na changamoto
mbalimbali ya kwanza ni kwa wanachama kutolipa ada kwa wakati.
Dkt. Kalemani ambaye ni Mwenyekiti wa
Baraza la Uongozi wa Kituo cha AMGC amesema changamoto ya pili ni wanachama wa
kituo hicho kutokitafutia wateja na masoko. Pia miundombinu mingi ya kutuo ni
chakavu.
Akizungumzia changamoto hizo Waziri
Mkuu ameziagiza nchi zote zinazodaiwa ada ikiwemo Tanzania zilipe ada stahiki
kwa wakati na kuweka mkakati wa kukitangaza kituo hicho ili kukiwezesha kupata
wateja kwa ajili ya kutumia huduma zitolewazo.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, SEPTEMBA 14, 2017.
No comments:
Post a Comment