Kaimu Katibu Mtendaji, Wizara ya Fedha na
Mipango - Tume ya Mipango Bw. Maduka Kessy (wa tatu kutoka kushoto, mwenye tai
nyekundu) na kiongozi wa ujumbe kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Kupunguza
Umaskini China, Bw. Xia Gengsheng (wanne kutoka kushoto) wakiwa katika picha ya
pamoja na wataalamu kutoka China na viongozi wa Tume ya Mipango.
Na Adili Mhina
Na Adili Mhina
Taasisi ya Kimataifa ya
Kupunguza Umaskini China (IPRCC) imeahidi kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano
baina yake na Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Tume ya Mipango kwa lengo la
kuongeza kasi ya maendeleo na kupunguza umaskini nchini.
Uamuzi huo umefikiwa katika
kikao cha wataalamu kutoka Wiraza ya Fedha na Mipango kupitia Tume ya Mipango
wakiongozwa na Kaimu Katibu Mtendaji Bw. Maduka Kessy na ujumbe kutoka taasisi
hiyo kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika kikao
hicho kiongozi wa ujumbe kutoka China Bw. Xia Gengsheng alieleza kuwa maeneo
mapya yanayotarajiwa ni pamoja na kuanzisha vituo vingingine vya mfano vya kilimo
katika vijiji mbalimbali hapa nchini.
Bw. Xia alieleza kuwa wameamua
kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano kutokana na mafanikio yaliyojitokeza
katika juhudi za kupambana na umaskini nchini hususan katika kutoa elimu ya
kilimo kwa wakulima kupitia kuanzishwa kwa Kijiji cha mfano cha Peapea Wilayani
Kilosa Mkoani Morogoro.
“Ndugu Kaimu Katibu Mtendaji
naomba nikuhakikishie kwamba tutaanzisha vijiji vingine vya mfano kama kile cha
Peapea na kutoa fursa kwa wananchi wengi zaidi kujifunza mbinu bora za kilimo
ili waweze kuendesha kilimo chenye tija na waondokane na umaskini,” alieleza Bw.
Xia.
Eneo jingine la ushirikiano
litakalo anzishwa ni masuala ya utafiti ambapo IPRCC kwa kushirikiana na Wizara
ya Fedha na Mipango kupitia Tume ya Mipango na taasisi zingine itawezesha
kufanyika kwa tafifi katika kuchochea maendeleo na kutafuta mbinu mbalimbali za
kupunguza kasi ya umaskini.
Kwa upande wake Kaimu
Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Bw. Maduka Kessy alieleza kuwa ushirikiano
kati ya Tume ya Mipango na Taasisi ya IPRCC ambao umedumu kwa zaidi ya miaka
sita umekuwa na faida kubwa katika kukabiliana na umaskini kwa watanzania.
Alielezea kuwa kwa kipindi
hicho Tume ya Mipango na IPRCC wamefanikiwa kuendesha programu mbalimbali ikiwa
ni pamoja na kuratibu mazungumzo ya kisera juu ya mageuzi ya kilimo vijijini na
kupunguza umaskini, kuanzishwa kwa kituo cha mfano katika kupunguza umaskini
kwa wakulima wadogo Kilosa Mkoani morogoro.
Aliongeza kuwa ushirikiano
kati ya Tume ya Mipango na IPRCC umefanikisha
uratibu wa programu za kuwajengea uwezo watanzania kwa kutoa udhamini wa masomo
katika ngazi za uzamili na uzamivu katika fani za maendeleo vijijini pamoja na
kuandaa mafunzo mbalimbali yanayohusu mageuzi ya kilimo kwa maafisa kilimo
pamoja na wakulima wenyewe.
Pamoja na mambo mengine, Taasisi
ya Kimataifa ya Kupunguza Umaskini ya China imekuwa ikisaidia kutoa msaada wa
kitaaalamu ambapo wataalamu wa kilimo kutoka China wamekuwa wakitoa mafuzo kwa wakulima mkoani Morogoro.
No comments:
Post a Comment