September 19, 2017

Safari ya kilometa 5,500 kwa mguu kusaka elimu

 Victoria Julius akitembea kuelekea Shule ya Msingi Abainano.
 Wanafunzi wakitembea kutoka shule kuelekea nyumbani.
Wanafunzi wakitembea wakati wa kutoka Shule.

NA HAPPINESS MNALE

NI jambo la kawaida kwa wanafunzi wanaosoma katika shule kadhaa za kutwa katika wilaya ya Tarime, mkoani Mara kuamka usiku wa manane ili waweze kufika shuleni kabla ya vipindi kuanza.

Miongoni mwa wanafunzi hawa ni Dotto Samson (15) anayeishi Mtaa wa Mtana. Kila siku Dotto huamka saa 09:00 alfajiri kisha kutembea kilometa 14 hadi Shule ya Sekondari ya Manga anakosoma.

“Ninaamka saa 9:00 usiku kujiandaa kwa ajili ya kwenda shule, nyumba ninatoka saa 10:00 lakini shule ninafika saa 2:0,”anasema. Hii inamaanisha kuwa, binti huyu anayesoma kidato cha pili hutembea kilomita 28 kwenda na kurudi shuleni kila siku.

Hesabu zinaonyesha kuwa kwa umbali wa Kilometa 28 kwa siku, Dotto na baadhi ya wanafunzi wenzake katika shule ya Manga, wanatembea kilometa 5,432 kwa siku 194 za masomo kwa mwaka. Ubali huu ni sawa na kilometa 21,728 kwa miaka minne (kidato cha kwanza hadi cha nne).

Urefu wa safari za wanafunzi hao kwa mwaka ni sawa kusafiri mara tano kati ya Kibaha mkoani Pwani hadi Njombe (kilometa 1089) au kati ya Kigoma na Arusha (kilometa 1090), Arusha na Vwawa mkoani Mbeya (kilometa 1091) au kati ya Bariadi Simiyu na Kibaha Pwani (kilometa 1092).

Kwa viwango hivyo vilivyoko kwenye jedwali (chati) la Wakala wa Barabara Nchini (TanRoads) toleo la Machi 2017, kwa miaka minne ya masomo wanafunzi hao hutembea kwa miguu zaidi ya mara 20 kwenda katika maeneo ya mikoa iliyotajwa.

Kadhalika Dotto na wanafunzi wenzake hutembea kilometa 140 kwa siku tano za masomo kwa wiki, karibu sawa na kutoka mjini Shinyanga hadi Bariadi (kilometa 138) wakati kwa siku 22 za masomo kwa mwezi, hutembea kilometa 616 karibu sawa na umbali kati ya Mwanza na Babati mkoani Manyara (kilometa 619) kwa takwimu za TanRoad.

Dotto anasema kuna wakati anatamani kuacha shule kutokana na kutembea umbali mrefu lakini anajikaza ili amalize. “Najikaza tu ili nimalize shule, maana nikisema niache nitaozwa na umri wangu bado mdogo, hivyo najitahidi lakini suala la kutembea kwakweli linatuchosha,”anasema.

Dotto anasema licha mbali na mwendo mrefu, pia hulazimika kufanya kazi za nyumbani kabla hajaelekea shule. “Nikiamka nafagia na kuosha vyombo, maji huwa nachota jioni baada ya kurudi shule,”anasema.
 
kadhalika hukutana na changamoto mbalimbali akiwa barabarani. “Ingawa hakuna pikipiki mara kwa mara za kuja huku, ila madereva bodaboda wanaopita wanatusumbua sana,”anasimulia. Anasema anatamani shule yao ujengewe mabweni ili wapate mahali pa kukaa na kujisomea.

“Wanaokaa kwenye mabweni ni wasichana wa kidato cha tano na sita pekee, lakini kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne tunarudi nyumbani, tunatembea umbali mrefu sana,” anasisitiza Dotto na kuongeza:

“…tunachoka, yaani mtu ukifika shule umechoka huna hamu ya kumsikiliza mwalimu, lakini pia tunaamka mapema, hivyo ikifika saa 4:00 asubuhi yaani nakuwa hoi kwa usingizi”.


Mkuu wa Shule ya Manga, Victoria Yonas anasema kutokana na uhaba wa mabweni wanachukua wanafunzi wa kike wa kidato cha tano na sita pekee.

Anasema shule yake inahitaji majengo matatu na vitanda 160 ili kuweza kuwahifadhi wanafunzi wote wa kike shule hapo.

“Changamoto ziko kwa wazazi, unaita kikao hawaji, wakija ukiwambia sula la kuchangia ili tujenge mabweni wanasema ilishatangazwa elimu bure, hivyo hawapaswi kuchanga chochote,”anasema na kuongeza:

“Lakini mila nazo, wanafunzi wengi tunawasukuma kuja shule, wanasoma ili mradi tu,tena wakishakeketwa ndio kabisa, na hivi wanatemeba umbali mrefu wa hadi kilomita 15 basi mnasukumana tu, mwalimu unasimama kidete ili waje shule, ni changamoto lakini tunapambana”.

Kuhusu ufaulu kwa wanafunzi wa kike anasema kwamba wengi wanapata daraja la nne na hakuna aliyewahi kupata daraja la kwanza ama la pili.

Safari ya shule usiku

Niliamua kujaribu kutembea kwenda Mangu. Hivyo nikiwa usingizini, nilisikia mlango ukigongwa. Ilikuwa alfajiri ya saa 10 kasoro dakika kadhaa. Nilihoji nani aliyekuwa akibisha hodi wakati huo.

Najibiwa; Ulisema nikuamshe saa 10:00 alfajiri unataka kwenda sehemu. Akili inarejea kauli niliyoitoa siku moja kabla, nikimwambia muhudumu wa Hotel ya Blue Sky iliyoko Tarime kwamba ahakikishe ananihamsha muda huo.

Moyo unajuta, kisha namwambia sawa, asante na pole kwa usumbufu. Haraka najiandaa, kisha natoka. Baada ya kufika kwenye geti la hoteli, nashikwa woga kwani kuna giza nene!. Naamua kuita pikipiki ambayo inanipeleka hadi kitongoji cha Mtana.

Hapo naanza kutembea kuelekea Manga. Nimejawa na hofu na woga kwani sehemu ninazopita ni pori na giza totoro. Baada ya kutembea hatua kama 20 hivi, moyo unatulia maana nimekutana na mwanafunzi ambaye tulipanga twende wote katika shule anakosoma. Huyu ni Dotto Samson.

Ananiuliza; Utaweza kutembea?Namjibu nitaweza, mbona we we unaweza! Akanijibu; nalazimika tu kutembea lakini sipendi. Tunaanza safari na tukiwa njiani anasema wala siku hiyo amepata mtu wa kuongozana naye kwani mara zote huwa peke yake.

Baada ya kutembea umbali mrefu, najisikia kuchoka hivyo namuuliza ikiwa tunaweza kupumzika. Dotto anasema haiwezekani kwani tukifanya hivyo, atachelewa vipindi.

Safari inaendelea na kunaanza kupambazuka, ni saa 12 sasa lakini bado tuko safarini. Hapo tunaanza kukutana na wanafunzi wengine wanaotoka vijiji vya Nyambanyasoko, Kembu, Nyamerambaro, Busarwi na vijiji vingine.

Wengi wanatokwa na jasho. Njiani wananisimulia maisha yao ya shule. Saa 2:00 asubuhi tunafika shule, wanafurahi kwamba angalau wamewahi kabla vipindi havijaanza.

Kutokana na kuchoshwa na kutembea kwa miguu kwa saa karibu nne, nashindwa kufanya kazi siku hiyo. Nalazimika kuita pikipiki kutoka Tarime mjini ili inifuate maana hapa hakuna usafiri wowote. Narejea mjini nikiwapa wenyeji wangu ahadi kwamba nitarejea kesho yake. Narudi Tarime nikiwa hoi.

Hali hii ni sawa na ile iliyotajwa na Taasisi ya Kimataifa ya Ufuatiliaji wa Haki za Binadamu (Human Rights Watch) katika taarifa iitwayo Nilikuwa na ndoto za kumaliza Shule, Februari mwaka huu, iikiutaja umbali kama moja ya vikwazo vya elimu kwa wanafunzi nchini.

“Serikali ya Tanzania inabidi iweke mikakati kabambe kuharakisha mipango yake kupambana na vikwazo hivi,”inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.

Kadhalika sera ya elimu na mafunzo ya 2014 inataja umbali kati ya shule na makazi ya wanafunzi kama kichocheo cha utoro na wananfunzi kuacha shule, huku ikiweka misingi ya kujengwa kwa miundombinu katika shule zote kama hatua ya kukabiliana na tatizo hilo.

Vitisho vya ushirikina, fisi

Siku ya pili sikuweza kutembea, hivyo nakodi gari kuelekea Manga sekondari.

Mkuu wa shule ya Manga, Yonas anasema sheria za shule ni kama zimelegezwa kwa wanaooshi mbali. “Wengi wanaishi mbali, nasi kama binadamu tunatambua hilo. Tunawahimiza kuwahi angalau vipindi, lakini kuwahi namba, kusimama msitarini wengi hawawezi,”anasema Yonas na kuongeza:

“Wapo wanafunzi wanaotembea kilomita saba kuja tu shule, wengine 10 na hata kilomita 15”.

Mwanafunzi mwingine wa shule hiyo Grace Julius (15) anasema wanapoamka usiku, wakati mwingine hukutana na vitisho vya ushirikina.

“Tunapita maporini, huwezi amini nakutana na wachawi wananitisha kuna wakati nakimbia, naanguka, mara nyingi kila mmoja anatoka nyumbani kwao peke yake maana tunaishi vijiji tofauti, mimi naishi Burongo,”anasimulia Grace na kuongeza:

“Kuna kipindi kila wakati nilikuwa nakutana na fisi hali ile ilisababisha niwe nasubiri kupambazuke ndio niende shule, nikawa nachelewa kwenye vipindi”.

Agness Juma ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule hiyo akiishia katika Kijiji cha Nyamerambaro, anasema hutumia saa 2:30 kutembea kutoka kwao hadi shule.

Tofauti na wenzake yeye analalamikia woga kutokana na kutembea umbali mrefu akipita eneo kubwa lisilo na watu.

“Kutembea kuanzia saa 10:00 za usiku msichana tu kama mimi peke yangu ni hatari, hali hiyo hunijengea wasiwasi, yaani huwa naogopa sana hata nikisikia miti inayumba naanza kukimbia najua ni mtu anataka kunitisha ama kunibaka, inatisha, tunateseka sana lakini hatuna namna,”anasema.

Nikiwa njiani kurejea Tarime mjini nakutana na mtoto Victoria Julius wa darasa la pili akitembea kuelekea shule.

Victoria anatembea taratibu kwenda shule huku akiwa amebeba busala (Togwa ya Kikurya). Anasema kwamba yeye huingia darasani saa 5:00 asubuhi akipisha na wenzake wanaoingia asubuhi.

“Nachoka kutembea, busala ni ya kunywa, shuleni hakuna chakula,nyumbani sipewi chakula cha kuja nacho shule, nakunywa busala tu mpaka nirudi nyumbani,”anasema.

Mwenyekiti wa Chama cha Walimu (CWT) wilayani Tarime, Shirikisho Nyagosaimana, anasema umbali wa shule moja hadi nyumbani huchangia watoto wa kike kupata mimba.

“Wazazi wengi walirudi kwenye mahame (maeneo) yao na kusababisha wanafunzi kukutana na umbali wa shule kutoka kijiji cha Mtana hadi Shule ya sekondari Manga ni umbali wa kilomita 14 kwenda hivyo mtoto wa kike anatembea kilomita 28 kila siku.

“Shule ziwafuate wananchi, serikali isiogope kulipa fidia ya maeneo mwanafunzi anatembea kilomita 28 kwa siku, hapo bado nakabiliwa na kazi za nyumbani, achote maji napo unakuta anatemeba umbali mrefu kilomita mbili, atasoma saa ngapi, akilala anakuwa hoi,”anasema.

Naye mwalimu wa shule ya msingi Magena, Francis Ngeta, anasema kwamba umbali mrefu husababisha wanafunzi kutojisomea.

“Atasoma saa ngapi, mfano huku tuna session (awamu) mbili, wanafunzi wanakuja shule asubuhi ikifika saa 6:20 mchana wanaenda nyumbani kula na kurudi shule saa 7:45 atembee kilomita sita hadi nyumbani, arudi tena sita ataelewa kweli vipindi, natamani chakula kitolewe shule,”anasema.
 
Ngeta anasema kwamba wanafunzi wanaoongoza kwa kuchelewa shule ni wasichana. “Kazi za nyumbani na mazingira ya shule hayamfanyi mtoto wa kike kupenda shule, wana changamoto nyingi sana katika elimu ikiwemo ukeketaji inagwa sasa wanadai wanaufanya kisayansi,”anasema.

Kwa upande wake Mzee Simango Nyarukamu ambaye ni mkazi wa Nyansicha, Tarime, anasema zamani watu walitembea umbali mrefu kusaka shule, hivyo haoni tatizo kwa wanafunzi wa sasa kutembea.

“Sisi tulikuwa tunalima, tunatembea umbali mrefu kwenda shule, wao wa sikuhizi wanashindwa nini, waache kulalamika, wasome,”anasema mzee huyo.

Suluhisho

Kifungu cha 35 (3) cha Sheri ya Elimu ya 1978 kinamtaka kila mtoto aliyeandikishwa katika shule yoyote kuhudhuria masomo mpaka pale atakapokuwa amehitimu masomo husika kama inavyoelekezwa katika vifungu vingine vya sheria hiyo.

Mei 4, 2016, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Stella Manyanya akizungumza bungeni alisema serikali imeweka mikakati ya kuboresha mazingira ya ufundishaji na kujifunzia kwa kujenga na kukarabati miundombinu ya shule zake.

Mkurugenzi wa Shirika la Haki Elimu, John Kalage anasema wasichana wengi huacha shule kwa sababu ya umbali na wengine hushindwa kutulia na kujifunza ipasavyo kwa sababu ya uchovu unaosababishwa na kutembea kwa umbali mrefu kila asubuhi na jioni.

Kalage anasema suluhisho ni Serikali itekeleze kwa vitendo wajibu wake wa kuhakikisha watoto wote wanapata elimu bila ubaguzi wa aina yoyote, ikiwemo kutatua changamoto za mazingira ya kujifunzia na kufundishia na kufanikisha kuwepo kwa elimu jumuishi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Apoo Tindwa, anasema jiografia ya wilaya hiyo inachangia changamoto. Anasema wanakabiliwa na uhaba wa vyumba vya madara na mabweni ya wanafunzi na kwamba mwaka huu halmashauri itatumia Sh. Milioni 450 kukarabati maboma ya madarasa 60.

Wilaya ya Tarime ina shule za sekondari 31 kati ya hizo, 29 ni za Serikali na mbili zinamilikiwa na taasisi za kidini.

No comments:

Post a Comment

Pages