Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), Dk Agnes Kijazi
(kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) alipokuwa
akitoa utabiri wa msimu wa mvua za vuli unaoanza mwezi Oktoba hadi
Disemba 2017. Kushoto ni Mkurugenzi Huduma za Utabiri TMA, Dk. Hamza
Kabelwa akishiriki katika mkutano huo.
MAMLAKA
ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa msimu wa mvua za vuli
unaoanza mwezi Oktoba hadi Disemba 2017. Kwa mujibu wa taarifa ya
utabiri iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam na
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi ambapo mvua za Vuli
zinatarajiwa kuanza Septemba, 2017 katika maeneo mengi ya Ziwa Viktoria
na mwezi Oktoba, katika ukanda wa pwani, na baadaye mwezi Novemba katika
maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki.
Alisema
ongezeko la mvua linatarajiwa katika miezi ya Novemba na Disemba, 2017
na hali kadhalika kutakuwa na vipindi virefu vya ukavu kujitokeza zaidi
katika mwezi wa Oktoba, 2017.
Hata hivyo
alisema mvua zinatarajiwa kuwa za wastani katika maeneo mengi ya mikoa
ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga, Dar es Salaam, Tanga,
Pwani, Kilimanjaro, Arusha na Manyara, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro
pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
Dk.
Agnes Kijazi alibainisha kuwa mvua za chini ya wastani na vipindi virefu
vya ukavu vinatarajiwa kujitokeza hususan katika maeneo ya mikoa ya
Kagera, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Pwani, Tanga, kaskazini mwa mkoa wa
Morogoro pamoja na maeneo ya visiwa vya Unguja na Pemba.
"Pamoja
na matarajio hayo ya mvua za wastani katika maeneo mengi ya nchi,
uwezekano wa matukio ya vipindi vya mvua kubwa unatarajiwa hususan
katika mwezi wa Disemba, 2017. Mtawanyiko hafifu wa mvua na vipindi
virefu vya ukavu vinatarajiwa kujitokeza katika baadhi ya maeneo katika
kipindi cha msimu wa mvua wa Oktoba hadi Disemba, 2017 hususan katika
maeneo ya mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Kilimanjaro, Arusha na
Manyara, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja and
Pemba," alisema Mkurugenzi Mkuu.
Pamoja na
hayo, Kijazi aliwashauri wakulima katika maeneo hayo kuandaa mashamba
yao mapema na kupanda mazao yanayokomaa katika muda mfupi, huku
akizitaka mamlaka husika, kama vile wadau wa Afya, menejimenti za maafa,
Mamlaka za miji na wadau wengine kuchukua hatua stahiki katika
kupunguza athari mbaya zinazoweza kutokea katika msimu wa mvua za Vuli
2017.
Aidha alisema kwa ujumala maeneo mengi
yaliyopo kaskazini mwa nchi yanatarajiwa kupata mvua za wastani na
uwezekano wa vipindi vifupi vya mvua kubwa hususan katika mwezi wa
Desemba 2017.
Msimu wa mvua wa Oktoba hadi
Disemba (vuli) ni mahususi kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua
kwa mwaka (Ukanda wa Ziwa Viktoria, nyanda za juu kaskazini mashariki,
Pwani ya kaskazini na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Kigoma). Na TMA
inatarajia kutoa utabiri wa mvua katika maeneo mengine ya nchi
yaliyosalia mwezi wa Oktoba 2017.
Imeandaliwa: wwwthehabari.com
No comments:
Post a Comment