WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea msaada wa vyerehani 25
kutoka katika Taasisi ya African Releaf Organization ya nchini Kuwait.
Amepokea msaada huo leo (Ijumaa, Septemba 9, 2017) kwenye makazi
ya Waziri Mkuu Oysterbay jijini Dar es Salaam kwa niaba ya wananchi wa jimbo la
Ruangwa.
Waziri Mkuu ameishukuru taasisi hiyo kwa msaada huo wa
vyerehani ambavyo vitagawiwa kwenye vikundi mbalimbali vya wajasiriamali
wilayani Ruangwa.
Amesema vyerehani hivyo vitawawezesha wajasiriamali
wanaojishughulisha na ushonaji kupata vitendeakazi vitakavyotumika kama njia ya
kujiongezea kipato.
Waziri Mkuu amesema mbali na kutoa msaada huo wa vyerehani
pia taasisi hiyo inajenga Zahanati katika kijiji cha Mbecha kata ya Nanganga wilayani
Ruangwa.
“Taasisi hii ni rafiki na Halmashauri yetu na Wanaruangwa
wamefarijika kwa kupata zahanati na
vyerehani vitakavyotumika kama njia ya kujiongezea kipato.”
Awali, Mkurugenzi wa Miradi wa Taasisi ya
African Releaf Organization, Bw. Khamis Mkanachi alishukuru kwa ushirikiano
wanaoupa kutoka Halmashauri ya Ruangwa.
Pia Bw. Mkanachi amesema taasisi yao itaendelea kuvisaidia
vikundi mbalimbali vya ujasiriamali katika Halmashauri hiyo kwa lengo la kuvikwamua
kiuchumi.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu alimtembelea na kumpa pole
mbunge wa jimbo la Newala Vijijini, Bw. Rashidi Akbar aliyelazwa katika Taasisi Moyo
ya Jakaya Kikwete.
Kwa upande wake Bw. Akbar alimshukuru Waziri Mkuu kwa
kumtembelea hospitalini hapo na kwamba hali yake kwa sasa inaendelea vizuri
ukilinganisha na alivyofikishwa.
Pia Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kumjulia hali Bw.
Anzigar Kambanga ambaye ni mwananchi wa wilaya ya Ruangwa aliyelazwa katika Taasisi
Moyo ya Jakaya Kikwete.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, SEPTEMBA 9, 2017.
No comments:
Post a Comment