WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amewataka viongozi wa taasisi zilizopewa dhamana ya kusimamia mazao makuu matano ya biashara
ambayo ni ya pamba, tumbaku, korosho, chai na kahawa kutekeleza majukumu yao
ipasavyo.
Amesema
mazao hayo ni muhimu
sana katika kuwezesha mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kufikia uchumi wa
viwanda kwani ndiyo mhimili wa kutoa malighafi za kuendesha viwanda husika na
yana mnyororo mpana wa uzalishaji ambao una fursa ya kutoa ajira nyingi.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo
(Ijumaa, Septemba 15, 2017) Bungeni mjini Dodoma alipowasilisha hotuba yake ya
kuahirisha Mkutano wa Nane wa Bunge. Amesema Serikali imejipanga kuimarisha
usimamizi katika uzalishaji na uuzaji wa mazao hayo.
Amesema Serikali itahakikisha kuwa
kila taasisi iliyopewa dhamana ya kusimamia mazao hayo, inatekeleza majukumu
yake ipasavyo sambamba na kuhakikisha kwamba Watendaji wake wanafanya kazi hiyo
kwa uadilifu na ufanisi mkubwa.
Amesema jitihada hizo zinalenga kuwawezesha
wakulima wengi hususan wa vijijini ambao ni takriban asilimia 75 ya Watanzania wote,
kulima kilimo cha kisasa, chenye tija na cha kibiashara, hivyo kuondokana na
umaskini wa kipato.
“Vilevile,
kuwawezesha wakulima kupata mbinu za kisasa za kuyafikia masoko ya uhakika ya
mazao yao ili kupata bei nzuri ambayo itawakwamua kiuchumi. Mazao mengine ya kibiashara yatakayotiliwa
mkazo ni katani, ufuta, alizeti, mbaazi na ngano.”
Amesema kwa kipindi kirefu uzalishaji wa
mazao hayo ulishuka kulitokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya baadhi ya viongozi
wa vyama vya Ushirika kushindwa kutekeleza vyema wajibu wao, wizi, dhuluma kwa
wakulima na pia ushiriki mdogo wa Maofisa Kilimo katika kusimamia kilimo cha kitaalam.
Wakati huo huo,
Waziri Mkuu amesema jumla ya vijana 1,000,000 wamelengwa kupata urasimishaji ujuzi kati ya mwaka 2017 na 2021 kupitia
Mpango wa Kutathmini na Kurasimisha Ujuzi uliopatikana nje ya Mfumo Rasmi wa
Mafunzo.
Amesea Serikali
imeamua kuchukua hatua hiyo ili kuwawezesha vijana ambao ndiyo nguvu kazi wachangie
kikamilifu katika kujenga uchumi wa Taifa. “Hadi sasa tayari vijana wengi
wanaendelea kunufaika na mpango huu kutoka mikoa mbalimbali.”
Miongoni mwa faida za mpango huo ni
pamoja na kuwasaidia mafundi waliojifunza kupitia sehemu za kazi kupata kazi
zenye staha na kuwajengea uwezo wa kushiriki na kushindana kikamilifu katika
soko la ajira. Pia kuinua tija mahali pa kazi na kusaidia waajiri/wenye
makampuni kukidhi viwango katika eneo la rasilimali watu.
Waziri Mkuu
amesema mpango huu unafadhiliwa kwa asilimia 100 na Serikali na unatekelezwa
kwa pamoja na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi ( VETA)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
40480 - DODOMA.
IJUMAA, SEPTEMBA 15, 2017
No comments:
Post a Comment