WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaomba
Viongozi wa Jumuiya na Taasisi zote za kidini nchini wahakikishe wanawapiga vita
watu wote wanaopanga na kutaka kuvuruga amani na utulivu uliopo nchini kwa
sababu watakwamisha maenendeleo.
Amesema Serikali inaelewa kwamba
dini ni miongoni mwa vyanzo muhimu vya maendeleo ya ustaarabu wa mwanadamu
kwani inatoa elimu ya maadili mema yenye kuwafanya waumini waepukane na maovu
mbalimbali.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo
(Jumapili Oktoka 01, 2017) wakati akifungua mkutano Mkuu wa mwaka wa 48 wa
Jumuiya ya Waislamu Waahmadiyya uliofanyika katika eneo la Kitonga kata ya
Msongola wilayani Ilala, Dar es Salaam.
Amesema kila Mtanzania anatakiwa
ahakikishe anadhibiti matukio yote yenye viashiria vya uvunjifu wa amani kwa
kutoa taarifa katika mamlaka husika.”Tanzania ni nchi salama na yenye utulivu,
hivyo ni lazima wote tushirikiane kuitunza.”
“Napenda niwahakikishieni kuwa Serikali
inaunga mkono juhudi za Jumuiya za kidini katika kupiga vita maovu ya kila aina;
mathalan utumiaji wa dawa za kulevya, wizi, rushwa, uzinzi ambao husababisha
madhara mengi ukiwemo ugonjwa wa UKIMWI.”
Amesema iwapo dini zetu zitatumika
vizuri tutaweza kwa haraka sana kutekeleza agizo la Rais Dkt. John
Magufuli la 'Hapa kazi tu' kwani kila
mtu ataepuka uzembe na kuwajibika ipasavyo.
Waziri Mkuu amesema ana imani kwamba
jumuiya hiyo kama zilivyo taasisi zingine za kidini itaendeleza kazi kubwa ya
kupambana na maovu katika jamii yetu kwa kuwapatia waumini wao na wananchi kwa
ujumla elimu na maarifa ya kuboresha tabia zao na maadili yao kiroho.
Amesema amani na utulivu uliopo
nchini unatokana na mambo mengi ikiwemo na wananchi kupata ustawi, kuweza
kufanya shughuli zao vizuri na kuwa na imani na Serikali yao, ambayo imejiwekea
mikakati ya kuhakikisha wananchi hususan wanyonge wanapata faraja ndani ya nchi
yao.
Waziri Mkuu amesema mambo yameweza
kupatikana baada ya Serikali kupambana na rushwa na ufisadi pamoja na
kuimarisha maadili ya watumishi wa umma, ambayo vimekuwa ni vyanzo vya kupotea
kwa amani na utulivu katika baadhi ya nchi.
“Serikali
imeweka mikakati madhubuti ya kupambana na ufisadi, kupitia mikataba mibovu na
kuimarisha maadili ili kujenga imani kwa wananchi, kuondoa migongano na tofauti
ya kipato, kuwa na matumizi mazuri ya rasilimali za umma, kuleta tija kwa
kuongeza thamani ya huduma na kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato.”
Awali,
Amir na Mbashiri Mkuu wa Jumuiya ya Waislamu Waahmadiyya Tanzania, Sheikh Tahir
Mahmood Chaudhry amesema Jumuiya hiyo
imekuwa ikifanya mikutano kila mwaka kwa lengo la kukumbushana misingi sahihi
ya dini tukufu ya kiislam pamoja na kukuza undugu wao.
Sheikh
Chaudhry amesema mkutano wa mwaka huu umejumisha watu zaidi ya 4,000 kutoka
mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani pamoja na wageni kutoka nchi za
Uingereza, Canada, Rwanda, Uganda, Ujerumani, Kenya, Burundi, Malawi na
Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Amesema
Jumuiya hiyo mbali na masuala ya kidini pia inatoa huduma mbalimbali za kijamii
kama elimu, maji na afya kwenye mikoa tofauti tofauti nchini.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, OKTOBA 01, 2017
No comments:
Post a Comment