WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amekabidhi zawadi ya gari aina ya carry kwa timu ya mpira wa miguu ya Afisi Kuu
Zanzibar baada ya kuibuka mshindi katika mashindano ya mpira wa miguu ya
Majimbo.
Mashindano hayo
yaliyohusisha majimbo 18 ya kisiwani Unguja yaliandaliwa na Chama Cha Mapinduzi
Zanzibar ambayo yalizinduliwa Machi 23, 2017 na Rais wa Zanzibar Dkt. Mohammed
Shein.
Alikabidhi zawadi hiyo jana
(Jumamosi, Novemba 25, 2017) katika mechi ya fainali iliyozikutanisha timu ya
Afisi Kuu na timu ya Jimbo Kwahani. Katika mechi hiyo ya fainali Afisi Kuu iliibuka
na ushindi wa magoli matatu na Jimbo Kwahani iliambulia goli moja.
Waziri Mkuu aliipongeza CCM
Zanzibar kwa kubuni mashindano hayo ambayo yaliwakutanisha vijana. Alisema
mbali na kuimarisha afya zao pia ni chanzo cha ajira hivyo ameishauri CCM
upande wa Bara kuiga ubunifu huo.
“Ubunifu huu wa kuanzisha
mashindano ya majimbo unapaswa kuigwa na Tanzania Bara, waanzishe mashindano
haya kwa kuyakutanisha majimbo yote. Ni vema jambo hili likawa la Kitaifa ili
kunufaisha vijana wengi.”
Pia Waziri Mkuu alimpongeza Muwakilishi
wa Jimbo la Uzini, Mohammed Raza ambaye ndiye alikuwa mdhamini mkuu wa
mashindano hayo, pia aliwashauri vijana walioshiriki mashindano hayo kuendelea
kufanya mazoezi.
Katika mashindano hayo timu
ya Jimbo Magomeni ilipewa tuzo ya timu iliyoonyesha hamasa kubwa, timu ya Jimbo
Mfenesini iliibuka kidedea kwa kuongoza kwenye nidhamu na golikipa wa timu ya
Afisi Kuu, Vuai Makame Jecha alipewa tuzo ya mchezaji bora.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, NOVEMBA 26, 2017.
No comments:
Post a Comment