WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amempa mwezi mmoja Ofisa Ardhi wa wilaya ya
Namtumbo Bw. Maurus Yera awe ametafuta ardhi ya kuwafidia wakazi wa
kijiji cha Lwinga wilayani Namtumbo.
Wakazi
hao 21 mwaka 2008 eneo lao lenye ukubwa wa ekari 101 lilitwaliwa na
Serikali kupitia halmashauri ya wilaya hiyo kwa ajili ya kupisha ujenzi
wa shule ya sekondari ya mkoa wa Ruvuma na waliahidiwa kulipwa fidia.
Waziri
Mkuu alitoa agizo hilo jana jioni (Alhamisi, Novemba 23, 2017)
alipozungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye
uwanja wa michezo wa Lwinga akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani
Ruvuma.
Alitoa
agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi hao kupitia
mabango, ambapo walimuomba awatatulie kero hiyo ya madai ya fidia ya
ardhi iliyodumu kwa miaka 10 bila kupatiwa ufumbuzi.
Waziri
Mkuu alisema haoni sababu ya Halmashauri hiyo kushindwa kuwafidia
wananchi hao sehemu ya ardhi kwa muda wote huo ukizingatia wilaya hiyo
ina hifadhi ya ardhi.
“Nataka
wananchi hawa wawe wamelipwa fidia yao ya ardhi kabla ya siku kuu ya
Krismasi ya mwaka huu. Serikali haiko tayari kuona wananchi wake
waliotoa ardhi kupisha maendeleo wakisumbuliwa.”
Waziri
Mkuu alisema Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli
inataka kila mtumishi ahakikishe anatumia taaluma yake vizuri kwa
kuwahudumia wananchi ikiwa ni pamoja na kutatua kero zinazowakabili kwa
wakati.
Pia
Waziri Mkuu alitoa wito kwa wananchi hao kuhakikisha hawakubali kutoa
rushwa pale wanapohitaji kupata huduma mbalimbali kutoka kwa watumishi
kwa kuwa ni haki yao kuhudumiwa.
Aliwataka
wananchi kuwa na imani na Serikali yao na kuiunga mkono katika
mapambano dhidi ya rushwa kwani vitendo hivyo vinakwamisha shughuli za
maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu amewataka watendaji kuhakikisha miradi wanayosimamia
inakuwa na thamani inayolingana na kiasi cha fedha kilichotolewa na
iwapo watabainika kwenda kinyume hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
“Lazima
kiasi cha fedha kinachotolewa kugharamia mradhi kilingane na thamani ya
mradi husika. Mfano tumetoa sh. milioni 70 kugharamia mradi na kukuta
mradi uliojendwa ni wa sh. milioni 30 aliyeshughulikia ujenzi huo nasi
tutamshughulikia hatutamuacha salama.”
Awali,
Waziri Mkuu alifungua ghala la kuhifadhiia mpunga na mchele katika
wilaya ya Namtumbo lililojengwa na MIVARF na kisha alizungumza na
watumishi wa halmashauri hiyo na kuwataka wafanye kazi kwa bidii na
kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Bibi Christine Mndeme alisema mkoa
huo unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa masoko
kwa mazao ya mahindi na mbaazi, ambapo Waziri Waziri Mkuu alisema sula
hilo linashughulikiwa hivyo wananchi waendelee kuwa na subira.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
iJUMAA, NOVEMBA 24, 2017.
No comments:
Post a Comment