WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na Maafisa
Kilimo kutoka mikoa inayolima korosho, washirikiane kupata takwimu mpya za
wakulima wa zao hilo.
Ametoa agizo
hilo leo mchana (Jumapili, Desemba 31, 2017) wakati akizindua kampeni ya
kitaifa ya upandaji mikorosho bora na mipya milioni 10 msimu wa 2017/2018 mjini
Ruangwa, mkoani Lindi.
“Maafisa kilimo na maafisa ushirika mkisimamiwa na Mkuu wa Wilaya na
Mkurugenzi, mshirikiane na kusimamia kwa umakini upatikanaji
wa takwimu za wakulima na maeneo yanayolimwa, haiwezekani kila mwaka takwimu ziwe
ni zilezile tu,” alisema.
“Afisa kilimo wa wilaya lazima ujue una wakulima
wangapi, je hao wakulima wako, kila mmoja analima ekari ngapi? Na katika ekari
hizo, ana miche mingapi, na je ana mahitaji ya pembejeo kiasi gani?” alisema.
“Pia nilikwishawaagiza maafisa ushirika na viongozi
wa vyama vya msingi (AMCOS) mpaka chama kikuu cha ushirika, kuwa kila mmoja anapaswa
atambue ana wanachama wangapi katika chama chake. Hili litawezekana pia kwa
kushirikiana na Afisa Mtendaji wa Kata au Mwenyekiti wa Kijiji, kwa sababu wao
wana idadi kamili za watu wanaowaongoza,” alisema.
“Ninaamini tukifanya
hilo tutamaliza tatizo la takwimu na Serikali itakuwa na uwezo mkubwa wa
kuwahudumia wakulima wake, na tutaweza kuweka bajeti ya kutosha kuhudumia mahitaji
yao,” alisisitiza.
Waziri Mkuu alipanda mche mpya
wa korosho ili kuanzisha zoezi la upandaji miche hiyo na kisha akagawa miche
kwa wakulima 10 kutoka vijiji vya Likunja, Kitandi, Kilimahewa na Nachingwea
ambao waliwawakilisha wenzao.
Mapema, kabla ya kuzungumza na wananchi Waziri Mkuu alikagua vitalu
vya miche ya mikorosho vilivyopandwa na Halmashauri ya Ruangwa na kuelezwa kuwa
miche hiyo ipo ya aina mbili ambapo aina ya kwanza ni ile iliyotokana na mbegu
na ya pili ni ile iliyotokana na vikonyo (grafting).
Waziri Mkuu ambaye pia ni
Mbunge wa Ruangwa, yuko kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka jimboni kwake.
Sherehe hizo
zilihudhuriwa na wakuu wa mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani na wajumbe wa
Bodi ya Korosho Tanzania (CBT). Wakuu wa Wilaya na wataalamu kutoka kituo cha
utafiti cha Naliendele walishiriki zoezi hilo.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI,
DESEMBA 31, 2017.
No comments:
Post a Comment