May 19, 2018

KILELE CHA MAADHIMISHO YA JUMA LA ELIMU KITAIFA MKOA WA SINGIDA

Mkuu wa Mkoa wa Singida. Dk Rehema Nchimbi  akizungumza na wadau wa elimu, walimu pamoja na wanafunzi wakati wa  kufunga maadhimisho ya Juma la Elimu kitaifa iliyofanyika katika wilaya ya Mkalama mkoani Singida.
Mwenyekiti Wa Bodi ya Mtandao wa Elimu Tanzania Dk John Kallage akitoa risala ya majumuisho ya uhamasishaji ya Juma la Elimu Kitaifa yaliyofanyika katika wilayani Mkalama mkoani Singida.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mh Dk Rehema Nchimbi akigawa mipira ya Miguu kwa baadhi ya wakuu wa shule za Msingi na Sekondari katika wilaya ya Mkalama ambayo iliyotolewa na Mtandao wa Elimu Tanzania wakati wa kilele cha Maadhimisho ya juma la elimu Kitaifa.
Mkuu wa Mkoa wa Singida. Dk Rehema Nchimbi akiendesha harambee ya kuchangia maboresho ya Elimu wilayani Mkalama wakati wa kilele cha juma la elimu yaliyofanyika wilayani humo.
Baadhi ya wanafunzi wakimuonyesha mabango yenye ujumbe wa Kuhamasisha Uwajibikaji wa Pamoja kwa Elimu Bora  wakati wa kilele cha juma la maadhimisho ya Elimu yaliyofanyika Wilayani Mkalama.
Wanafunzi wakiwa kwenye maandamano wakati wa kilele cha juma la elimu kitaifa

Kampeni ya Juma ya Elimu Duniani huadhimishwa duniani kote kati ya mwezi wa nne na wa tano. Nchini Tanzania Maadhimisho haya huratibiwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET) Ikishirikiana na wadau mbalimbali wa elimu, serikali na taasisi binafsi.

Kwa  Mwaka 2018 maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa yamefanyika Wilaya ya Mkalama, Mkoa wa Singida kuanzia tarehe Mei 14 hadi Mei 18 2018 ambapo Mgeni rasmi katika sherehe za Kilele cha Maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa alikua Mkuu wa Mkoa wa Singida Mh. Dk Rehema Nchimbi.

Akisoma majumuisho ya uhamasishaji wa juma la Elimu wilayani Mkalama Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Elimu Tanzania Dk. John Kallage alielezea mada ya Mwaka huu Kitaifa ni “Uwajibikaji wa pamoja kwa Elimu Bora kwa wote” na kwa wilaya ya Mkalama uhamasishaji ulifanyika katika Shule za Msingi sita na Shule za Sekondari tatu  ambapo ni katika vijiji sita ambavyo ni Mbigigi, Kikhonda, Ikolo, Mwangeza, Malaja na Nyahaa. 

Wadau wa elimu walifanikiwa kufanya mikutano ya kijamii ikijumuisha wazazi, wanajamii na viongozi wa serikali ya kijiji, dini na watu mashuhuri ili kubaini na kuzitafutia ufumbuzi changamoto za Elimu kwa pamoja.

Wadau wa Elimu katika Ziara ya uhamasishaji wa Juma la Elimu katika wilaya ya Mkalama walibaini Changamoto mbalimbali ikiwemo Bajeti finyu ya Serikali isiyokidhi mahitaji ya Sekta ya Elimu, Upungufu Mkubwa wa  walimu  na hasa waalimu wa masomo ya Sayansi na walimu wa Kike, Upungufu wa madawati, Upungufu wa vitabu vya kiada na ziada, Miundombinu isiyokidhi mahitaji mfano Vyumba vya madarasa, Vyoo, Maji na Nyumba za walimu pamoja na uhaba wa miundombinu rafiki kwa watu wenye mahitaji maalumu.

Katika Risala ya Majumuisho ya uhamasishaji wa Juma la Elimu Kitaifa wilayani Mkalama Mwenyekiti wa Mtandao wa Elimu Tanzania Dk John Kallage alisema “Mtandao wa Elimu Tanzania unatambua na kupongeza juhudi mbalimbali za Serikali katika kuboresha Kiwango cha Elimu nchini ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu bila malipo ya ada”

Mtandao wa Elimu Tanzania na waadau wa Elimu waliishauri Serikali kuongeza jitihada za kuinua ubora wa Elimu nchini ili kufikia malengo ya Kitaifa na Kimataifa kwa Kuongeza Bajeti ya elimu, kuajiri walimu wa kutosha na kuboresha mazingira yao ya kufanyia kazi, kuimarisha miundombinu ikiwemo vyumba vya madarasa, vyoo, upatikanaji wa maji na nyumba za walimu, Kuboresha mitaala ili iweze kuendana na wakati pamoja na kuongeza mapambano ya kupinga mila kandamizi zinarudisha nyuma jitihada za maendeleo ya elimu.

Mtandao wa Elimu Tanzania katika kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha Elimu imechangia vifaa mbalimbali ikiwemo Mabati na milango kwa ajili ya kuisaidia Shule ya Msingi Mbigigi vyenye Thamani ya Tshs 12,000,000/= pamoja na Mipira ya miguu katika shule zote zilizptembelewa na wadau wa Elimu.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mh. Dk Rehema Nchimbi akifunga Maadhimisho wa Juma la Elimu Kitaifa, Alipongeza juhudi na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Mtandao wa Elimu Tanzania pamoja na wanachama wake katika kuinua na kuboresha Elimu Nchini. Akiongea katika Sherehe hizo Mh. Dk Rehema Nchimbi alisema “Elimu ni kipaumbele cha serikali ya awamu ya Tano na Utoaji wa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari ni kiashiria tosha na hivi karibuni tu Serikali imetangaza Ajira mpya kwa waalimu wa masomo ya Sayansi na natumai hata wilaya ya Mkalama itafaidika”. 

Katika Sherehe hizo pia Mkuu wa Singida aliendesha harambee kwa ajili ya Kuchangia maboresho ya Elimu na inakadiriwa kiasi cha Milioni Tatu zitakusanywa.

No comments:

Post a Comment

Pages