May 20, 2018

SERIKALI YAWAASA VIONGOZI WA DINI WAEPUKE MIGOGORO

 SERIKALI imewaasa viongozi wa dini waeuepuke migogoro ya mara kwa mara katika Makanisa yao na badala yake waendelee kuwajenga waumini wao wakue kiroho na kujenga dhana ya umoja na upendo katika Taifa.

Pia imesema inawashukuru viongozi wa dini na madhehebu yote ya dini kwa kuendelea kuiombea nchi amani, mshikamano na utulivu, jambo ambalo linaongeza chachu kubwa kufikia mafanikio ya maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Hayo yamesemwa leo (Jumapili, Mei 20, 2018) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika ibada ya kutawazwa Askofu Dkt. Maimbo Mndolwa wa Dayosisi ya Tanga kuwa Askofu Mkuu wa saba wa Kanisa la Anglikana Tanzania. Ibada hiyo imefanyika katika Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu Dayosisi ya Central Tanganyika Jijini Dodoma.

“Nawaombeni wote kwa ujumla wetu, tuendelee kutumia Makanisa yetu kuombea Taifa hili ili tuendelee kuishi kwa amani, upendo na mshikamano”. Watu wa Mungu ni watu wa Upendo, watu wa Mungu ni watu wa amani, watu wa Mungu ni watu wa kiroho”.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa “haitarajiwi kuona watu wa Mungu wakiwa katika mstari wa mbele kuchochea migogoro, kuvunja amani ya Kanisa na kuongoza makundi yanayopingana katika kazi ya Bwana”.

Amesema jukumu la makanisa ni kuwajenga waumini kukua kiroho, na kazi ya kuwaongoza watu wamjue Mwenyezi Mungu, ambapo amewaomba imani yao iwe moja na matendo yao yafanane na yale ya Kristo Yesu wanayemuamini.

Waziri Mkuu amesema kuwa nchi haiwezi kupata mafanikio ya kiuchumi na kijamii bila kuilinda amani iliyopo, hivyo amewaomba warejee kumbusho la maandiko Matakatifu katika Waebrania 12:14  “Tatufeni kwa bidii kuwa na Amani na watu wote”.

Pia Waziri Mkuu ametoa wito kwa viongozi hao na wananchi kwa ujumla waendelee kuwaombea viongozi wa Tanzania hususani Rais Dkt. John Magufuli, kuendelea kuwa na afya njema, busara, upendo, hekima katika kuiongoza nchi yetu.

Waziri Mkuu ambaye amemuwakilisha Rais Dkt. Magufuli katika ibada hiyo amesema Serikali inatambua ushirikiano uliopo kati ya madhehebu mbalimbali ya dini nchini kwa ujumla wake na kwamba ushirikiano huo ni wa kihistoria.

Amesema mara zote madhehebu ya dini yamekuwa yakisaidiana na Serikali katika kutoa huduma za elimu, afya, maji na makundi maalum kama vile yatima, wazee, walemavu, wajane na huduma hizo zimekuwa zikitolewa kwa Watanzania wote bila ubaguzi wa aina yoyote. “Mambo haya hayawezi kupatikana nchini bila ya kuwa na amani”.

Kwa upande wake Askofu Dkt. Mndolwa baada ya kutawazwa aliahidi kulitumikia kanisa la Anglikana katika kweli, haki na upendo.

“Naahidi kwa makini kwamba nitaistahi na kudumisha na kuilinda Imani, haki na uhuru wa Kanisa la Anglikana Tanzania na kulitumikia katika kweli, haki na upendo, nisijifanye kuwa bwana juu ya urithi wa Mwenyezi Mungu, bali katika mambo yote nioneshe kielelezo kwa kundi la Kristo. Mungu nisaidie,”.

Askofu Dkt. Mndolwa anashika wadhifa huo baada ya aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Askofu Jacob Chimeledya kumaliza muda wake. Askofu Chimeledya alitawazwa mwaka 2013.

Maaskofu wengine waliowahi kuongoza kanisa hilo tangu kuasisiwa kwake nchini ni John Thomas Mhina Sepetu (1970-1978), Askofu Musa Kalemo Kahurananga (1979-1983), Askofu John Auckland Ramadhani (1984-1997), Askofu Donald Leo Mtetemela (1998-2008), Askofu Valentino Leonard Mokiwa (2009-2013).


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
JUMAPILI, Mei 20, 2018.

No comments:

Post a Comment

Pages