WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema shida ya umeme iliyokuwa inaikabili
mikoa ya Lindi na Mtwara hivi sasa imekwisha.
"Kuunganishwa
kwa mikoa ya Lindi na Mtwara kwenye gridi ya Taifa, kumeondoa tatizo la umeme
lililokuwa likiikabili mikoa hii, na mitambo ya jenerata iliyokuwepo, itabakia
kuwa ya akiba endapo dharura yoyote itatokea," alisema.
Ametoa kauli
hiyo jana jioni (Jumatatu, Mei 21, 2018) wakati akizungumza na wakazi wa mji wa
Mtwara kwenye viwanja vya bandarini mjini humo.
Alisema
pengo lililokuwepo la kukatikakatika kwa umeme, limezibwa kwa kupata umeme wa
kutoka Somanga hadi Lindi. “Umeme huu umeanzia kituo chetu cha Mbagala, umekuja
Mkuranga, Muhoro, Lindi na hatimaye umefika pale Mahumbika. Na mchana wakati
nikiwa Mahumbika, niliwasha kwa kompyuta kuashiria umeme wa gridi kuingia mikoa
yetu ya Lindi na Mtwara,” alisema.
Akiwa Mtwara
mjini, Waziri Mkuu alikagua na kisha kuzindua mradi wa upanuzi wa kituo cha
kufua umeme wa gesi asilia wenye uwezo wa kuzalisha megawati nne.
Kabla ya
kuzindua mradi huo, alipita bandarini kukagua ukarabati
wa mitambo ya kupokelea mafuta ya dizeli na petroli ambako alielezwa kuwa
kampuni mbili za GM na OILCOM zimeanza ukarabati na kwamba mwezi ujao, bandari
hiyo itaanza kupokea meli za kubeba mafuta.
“Bandari ya Mtwara hivi sasa
itaanza kupokea meli kubwa za mafuta, jambo ambalo halijafanyika tangu mwaka
2014. Mwezi ujao, wakati wowote, wataanza kupakua mafuta. Kwa hiyo mji utaanza
kuchangamka.”
“Kuanza kupakuliwa kwa
mafuta katika bandari hii, kutasaidia kushusha bei ya mafuta kwenye mikoa hii
na pia kiasi kitakachobakia, tutakipeleka nchi za jirani za Msumbiji na
Malawi,” alisema.
Alisema matengenezo hayo
yakikamilika yatafanya bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga zote ziwe na
uwezo wa kupokea mafuta. Pia aliitaka Mamlaka ya Bandari (TPA) iondoe urasimu
na Mkurugenzi Mkuu wake awatumie vizuri watendaji waliopo chini yake.
Mapema, walipopewa nafasi ya kusalimia wananchi, wabunge wa Chama cha Wananchi
(CUF) walitumia fursa hiyo kuelezea kufurahishwa kwao na hatua za maendeleo
zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kilwa Kusini, Bw. Selemani Said Bungara alisema
aliamua kutoka Chama cha Mapinduzi kwa sababu aliamini kwamba mtu hawezi
kusukuma gari akiwa ndani, ni lazima atoke.
“Tumetoka ndani ya gari ya gari na sasa tunalisukuma na linakwenda kwa
kasi. Hebu angalia, ndani ya miaka miwili tu, mambo yanavyokwenda kwa kasi. Kama
tungebakia ndani, gari lingeenda?” alihoji.
Hoja yake ilijibiwa na Mbunge wa Nanyamba, Bw. Abdallah Dadi Chikota
ambaye alisema gari analolizungumzia mbunge huyo liko imara na wala halihitaji
kusukumwa. “Gari letu halihitaji kusukumwa hata kidogo, liko imara, matairi
yako imara, na dereva wetu yuko makini. Tena gari letu hata muda wake wa service haujafika,” alisema na kuamsha
shangwe kwa wananchi waliokuwa wakimsikiliza Waziri Mkuu.
Naye Bw. Zuberi Mohammed Kuchauka (Liwale) aliwataka wananchi wa mikoa ya
Kusini wachangamkie fursa zinazopatikana kutokana na maendeleo yanayofanywa na Serikali
ya awamu ya tano. “Kusini hivi sasa imeamka na imetoka gizani, sasa wananchi
tuchangamkie fursa,” alisema.
Naye Mbunge wa Nachingwea, Bw. Hassan Elias Masala, alitumia fursa hiyo
kuomba barabara ya kutoka Nachingwea iwekewe lami ili wakazi wake waweze
kutumia fursa ya kusafirisha korosho zao hadi kwenye bandari ya Mtwara.
Naye Bw. Maftaha Abdallah Nachuma (Mtwara Mjini) pia aliomba barabara ya
kutoka Mtwara hadi Mingoyo ikamilishwe matengenezo yake kwani kwa hali ya sasa
siyo rahisi kusafirisha mizigo. Pia aliomba apelekewe umeme maeneo ya Mbawalachini
na Mkunjanguo. “Maendeleo hayana chama, kabila wala itikadi,” alisema.
Wabunge wengine waliofuatana na Waziri Mkuu kwenye ziara hiyo ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na Mbunge wa Mtwara Vijijini,
Bibi Hawa Ghasia na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Bi.
Hamida Mohammed Abdallah (Viti Maalum).
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI
MKUU,
JUMANNE, MEI 22,
2018.
No comments:
Post a Comment