May 29, 2018

TAZAMA YATOA GAWIO LA MIL. 681.8 KWA TANZANIA

Mkurugenzi Mkuu wa Tazama, Davison Thawethe, akizungumza katika hafla ya utoaji wa gawio la Sh. Mil. 681.8 kwa serikali ya Tanzania. 



Wafanyakazi wa Tazama wakiwa katika hafla hiyo. 

Katibu Mkuu wa Nishati wa Zambia na Mwenyekiti wa Bodi ya Tazama, Brigedia Emeldah Chola, akizungumza kabla ya kukabidhi gawio la Sh. Mil. 681.8 kwa serikali ya Tanzania.
 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Amina Shabani, akizungumza kabla ya kupokea gawio la Sh. Mil. 681.8 kutoka Tazama.
 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Amina Shabani (kushoto), akipokea mfano wa hundi yenye thamani ya Sh. Mil. 681.8 kutoka kwa Katibu Mkuu wa Nishati wa Zambia na Mwenyekiti wa Bodi ya Tazama, Brigedia Emeldah Chola (wa pili kulia), ikiwa ni gawio kwa Tanzania kutoka Tazama, hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam.


Dar es Salaam, Tanzania
BOMBA la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Dar es Salaam hadi Ndola Zambia, linalomilikiwa na  Tanzania na Zambia (Tazama), limetoa gawio la Sh. milioni 681.8 kwa Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Amina Shabani alisema hii ni mara ya kwanza kwa bomba hilo kutoa gawio kwa wanahisa wake tangu kuanzishwa  miaka 50 iliyopita.
Alisema kutotolewa kwa gawio kulitokana na bomba hilo kufanya kazi kama watoaji huduma jambo lililofanya washindwe kutengeneza faida na badala yake kujiendesha kwa hasara.
“Hili ni tukio la kihistoria tumefanya kazi kwa miaka 50 hatujawahi kupata gawio lolote, awali shirika lilikuwa linafanya kazi kama watoa huduma kwa nchi hizi katika kusafirisha mafuta lakini kuanzia mwaka jana mfumo umebadilika na sasa linafanya kazi kibiashara” alisema Amina.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Nishati wa Zambia na Mwenyekiti wa Bodi ya Tazama, Brigedia Emeldah Chola alisema kwa mwaka jana waliingiza Bilioni 11.4 ambapo wametoa Sh. bilioni 2.0 sawa na asilimia 20 ya mapato yake kwa wanahisa.
Alisema katika gawio hilo Zambia ambayo wanamiliki 2/3 ya hisa wamepata Sh.bilioni 1.2.
“Gawio linaonekana kuwa dogo lakini kwangu naona ni hatua muhimu kwani ni inaashiria kutoka kwenye kupata hasara kutokana na kufanya kazi kwa mazoea” alisema Chola.
Alisema wamedhamiria kuongeza ufanisi katika utendaji kazi  pamoja na kuongeza mikakati itakayosaidia kuongeza thamani kwa wanahisa wao kwa kuzingatia miongozo ya serikali.
Aidha alitaja baadhi ya mikakti waliojiwekea kuwa ni pamoja na kuongeza upana wa bomba hilo lenye ukubwa wa Kilomita 914 kufikia inchi 12 kutoka nane za sasa mradi utakoagharimu Dola za Marekani milioni 350 na kuongeza kuwa baada ya kufanya hivyo bomba hilo litakuwa na uwezo wa kusafirisha Tani milioni 1.5 kwa mwaka.
Jingine ni kujenga bomba jipya kwa ajili ya mafuta yaliyokwishachakatwa ambao unatarajiwa kugharimu  Dola za Marekani Bilioni 1.5  pamoja na kuwa na utaratibu wa kukagua mitambo yao mara kwa mara ili kuweza kufanya maboresho kabla ya kuchakaa na kuhitaji mataengenezo makubwa.

No comments:

Post a Comment

Pages