May 23, 2018

VYUO VIKUU NCHINI VYASHAURIWA KUFUNDISHA UJASIRIAMALI KWA VITENDO KUWAWEZESHA WAHITIMU KUJIAJIRI

Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania ( TPSF), Bwana Godfrey Simbeye ameshauri Vyuo Vikuu kutoa kipaumbele katika kufundisha ujasiriamali wakati huu ambapo Serikali ya awamu ya tano imejikita katika kuhakikisha nchi yetu inaingia katika nchi za uchumi wa kati kwa kuimarisha Uchumi wa  Viwanda. 

  Ameshauri pia Wakuu wa Vyuo Vikuu nchini washirikiane kuweka programu za ujasiriamali  ili kuwaandaa wahitimu kwa kushirikiana kwa kuwa hao ndiyo tegemeo katika kuelekea uchumi wa viwanda na hatimae kuingia uchumi wa kati ifikapo 2025. 

Simbeye ameyasema hayo katika kambi maalum ya Ujasiriamali iliyoandaliwa na Chuo kikuu Mzumbe  kwa  lengo la kutoa fursa ya kupeana mbinu na stadi  za ujasiriamali kwa Wanafunzi,Wafanyakazi na Wanajamii wanaokizunguka Chuo hicho.  Simbeye amepongeza Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuanzisha utaratibu huo na kushauri  Vyuo Vikuu vingine nchini kushirikiana na Chuo Kikuu Mzumbe ili kambi hizi ziweze kushirikisha wanafunzi toka vyuo vyote. “ Natambua kuwa kambi kama hizi zinafanyika katika vyuo vingi pia , lakini nishauri tu muungane ili kuongeza ubora na kufikisha elimu hii kwa wanafunzi wengi zaidi na ninashauri Mzumbe muwe chachu ya kuanzisha mpango huu.”
 Simbeye ameeleza kufurahishwa na kasi ya serikali ya awamu ya Tano katika kuhamasisha uanzishwaji wa Viwanda  na kueleza kuwa wao kama sekta Binafsi wanaunga mkono juhudi hizo.   Simbeye amesema amefurahishwa kuona ubunifu na uanzishwaji wa viwanda vidogo unaofanywa na wanafunzi na kuwataka kuhakikisha juhudi zao zinaendelea na viwanda vyao vinakuwa kufikia viwanda vya kati.
Ameongeza kuwa idadi ya viwanda nchini bado ni ndogo kwa mujibu wa shirika la Viwango, taarifa ya 2018 inaonesha kuwa Tanzania ina jumla ya viwanda 53,876 vikiwemo vikubwa ambavyo ni tegemeo 256,viwanda vya kati 173, wakati viwanda vidogo ni 6,957  huku vile vidogo kabisa  vikiwa 46, 495, ukilinganisha na nchi jirani ya Kenya yenye viwanda zaidi 500,000, aliyasema haya akisisitiza kuwa fursa zipo na lengo ni kuhakikisha viwanda vinakua kufikia viwanda vya kati. Ameeleza kuwa TPSF ina jukumu kuu la kuhakikisha inashirikiana na serikali katika kuhakikisha uendeshaji biashara nchini unakuwa na mazingira rafiki na rahisi na wezeshi kupitia majadiliano kati ya Sekta Binafsi na Serikali.
Simbeye aliekuwa mzungumzaji mkuu katika Kambi hii, alishukuru Chuo Kikuu Mzumbe kwa Kuwa tayari kufungua milango ya ushirikiano kwa kutoa ujuzi na uzoefu wa kitaaluma kwa vijana na wananchi  wengine wakiwemo waajiriwa na wajasiriamali ili kuwajengea uwezo.  Akitoa shukrani hizi Simbeye aliahidi kushirikiana na Chuo kikuu Mzumbe kuanzisha Mfuko maalum utakao saidia kukuza elimu ya Ujasiriamali kwa vijana na kukutanisha vyuo vikuu na wafanyabiashara wakubwa kwa ajili ya kushiriki katika kulea wajasiriamali na wabunifu wanaoanza.
Awali akizungumza kabla ya ufunguzi wa kambi hiyo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof.Lughano Kusiluka  alisema wameamua kuanzisha kambi ya ujasiriamali  kwa lengo la kushiriki kwa vitendo katika azma ya Serikali kuelekea uchumi wa viwanda kwa kuwaandaa wahitimu hao ili waweze kuleta tija na kuongeza uzalishaji kupitia Sekta ya ujasiriamali na viwanda. Prof Kusiluka alisistiza kuwa wakati umefika wa wahitimu kutumia elimu wanayoipata kujiajiri  zaidi kuliko kutegemea ajira.
Aidha Prof.Kusiluka aliongeza kuwa uanzishaji wa kambi hiyo ni utekelezaji wa mpango mkakati wa   maendeleo wa Chuo ambao miongoni mwa mikakati yake ni kuhakikisha Chuo kinahamasisha shughuli za ujasiriamali na biashara kwa kuanzisha mafunzo maalum kwa Wanachuo na kuwaandaa kujiajiri kwa kutumia elimu waliyoipata Chuoni hapo. Prof Kusiluka aliongeza kuwa Kambi hizi zitaendelea kufanyika kila Mwaka na kwa ukubwa zaidi. 
Naye Mkuu wa Idara ya Rasilimali na Ulezi katika shule ya biashara, Dkt Emmanuel Chao alisema maamuzi ya kufanya kambi hiyo yametokana na kuwepo kwa mitazamo tofauti miongoni mwa Wahitimu wa Vyuo vikuu nchini kuwa wanapaswa kuajiriwa moja kwa moja pindi wanapomaliza masomo yao, mtazamo ambao hauendani na hali halisi na hivyo wengi wao kujikuta wakikosa ajira kutokana na kukosa mbinu za kujiajiri na hivyo Chuo kikuu Mzumbe kimeona umuhimu wa kuanza kutoa stadi hizo bure kwa wahitimu wote wanaotaka kujiajiri na kuwasaidia katika kukuza ubunifu na mawazo yao ya kibiashara.
Mgeni rasmi katika kambi hiyo Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Ndugu Clifford Tandari, alipongeza  hatua ya Chuo Kikuu Mzumbe kkuwa na kambi hiyo  huku akiwataka wanaosimamia pamoja na chuo kusaidia wajasiriamali na wabunifu walipo katika chuo kuhakikisha wanasaidiwa kurasimisha biashara zao pamoja na kuzisajili.  Tandari amekitaka  Chuo Kikuu Mzumbe kusaidia pia kutoa elimu kwa wajasiamali wengine katika mkoa wa Morogoro ambapo alisema mpaka sasa unaongoza katika kuwa na viwanda vingi nchini.
Katika kambi hiyo wadau mbalimbali walipata fursa ya kutoa mafunzo na kutoa uzoefu wao katika biashara akiwemo Prof Ngowi kutoka , Chuo Kikuu Mzumbe, mjasiriamali mzoefu Kutoka Kishaga na wengine. Vile vile bidhaa za wabunifu wajasiriamli wanafunzi na baadhi waliohitimu kutoka Mzumbe zilizinduliwa.
Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Lughano Kusiluka, akifurahi pamoja na Wanafunzi Wajasiriamali walioshiriki kambi ya Ujasiriamali na kuzindua bidhaa zao.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF),  Godfrey Simbeye,  akizindua bidhaa ya mvinyo iliyotengenezwa na wafanyakazi wajasiriamali wa Chuo Kikuu Mzumbe, mjini Morogoro mwishoni mwa wiki, wakati wa Kambi ya Ujasiriamali iliyoandaliwa kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuwapa mbinu na stadi za ujasiriamali wanafunzi, wafanyakazi na jamii inayokizunguka chuo hicho.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Lughano Kusiluka, akizindua moja ya bidhaa za Wananchuo walioshiriki kambi ya Ujasiriamali.
Mjasiriamali akinadi bidhaa zake  kwa Washiriki.
Baaadhi ya washiriki wa kambi ya ujasiriamali wakiangalia bidhaa zilizoletwa katika kambi hiyo.
Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro (mwenyesuti nyeusi) akiendelea kupokea maelezo kuhusu bidhaa kwa wajasiriamali walioshiriki kambi hiyo. Kushoto kwake ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Lughano Kusiluka.
Mkamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo SUA, Prof. Raphael Chibunda, akijadiliana jambo na Rais wa Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu Mzumbe (mwenye shati jeupe) mbele ya mgeni rasmi,mwenyekiti wa TPSF na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe
Mjasiriamali akitoa maelezo ya bidhaa zake kwa Mgeni Rasmi Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro ndg.Cliford Tandari (katikati), kulia kwake ni Mkurugenzi wa Sekta Binafsi Tanzania TPSF na kushoto ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda.
 Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu  cha Kilimo SUA, Prof. Raphael Chibunda, akimpongeza Mwanafunzi wa Sheria wa Chuo Kikuu Mzumbe Talib Mlilima aliyejikita katika ujasiriamali wa kubuni na kushona suti baada ya kuzindua bidhaa yake.
Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Clifor Tandari akifurahi pamoja na Wanafunzi  wakati akizindua bidhaa za Wanachuo hao.Anayeshuhudia pembeni ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof.Lughano Kusiluka.

Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro akipata maelezo kutoka kwa Mjasiriamali (hayupo pichani)

No comments:

Post a Comment

Pages