Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
ameiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani kwa
kushirikiana na Jeshi la Polisi waangalie umuhimu wa kutumia mifumo ya ulinzi
wa miji ya kieletroniki (City Surveillance System) ili kupunguza uhalifu na
kuongeza usalama wa wananchi na mali zao.
Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Mei 24, 2018) wakati akizungumza na
mamia ya wananchi na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam na viongozi wa Jeshi la
Polisi kwenye viwanja vya Mbweni, wilayani Kinondoni, mkoani Dar es Salaam baada ya kuzindua vituo
vya polisi vya kisasa vya Mburahati, Kiluvya-Gogoni na Mbweni.
“Katika suala zima la
kuimarisha usalama, napenda niwape changamoto Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
na Jeshi la Polisi ili zitoe kipaumbele kwenye matumizi ya City Surveilance System (CCTV). Usimikaji wa mifumo hiyo utasaidia
kupunguza uhalifu na kuongeza usalama wa wananchi na mali zao,” amesema.
Waziri Mkuu amesema tayari
Jiji kama Nairobi la nchini Kenya linatumia mifumo ya aina hiyo na kwamba uwepo
wa mifumo hiyo, na haoni ni kwa nini Tanzania bado haijawa na mifumo kama hiyo.
Amesema uwepo wa mifumo
hiyo, utasaidia si tu kutambua kwa wepesi wahusika wa matukio ya uhalifu kama
vile ukwapuaji, wizi wa magari na uharibifu wa mali, bali pia utaongeza
shughuli za kibiashara na utalii.
"Tanzania hatujaanza
kutumia mifumo hii lakini ifike mahali, tuanze kubadilika. Tafuteni wataalamu
wenye ujuzi watufungie mifumo hii ili iwe rahisi kufuatilia matukio
mbalimbali. Naibu Waziri wa Mambo ya
Ndani fuatilia mifumo hii ili tuanze na majiji yetu na tuweze kufuatilia matukio
ya kihalifu barabarani na mitaani", amesema Waziri Mkuu.
"Nitoe rai kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Polisi
wachukue hatua za haraka kurahisisha upatikanaji wa matumizi ya mifumo hiyo
hususan katika majiji yetu kwa ajili ya kuimarisha usalama wa watu na mali
zao," amesema.
Mapema, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Yusuf Masauni
alimshukuru Rais Dkt, John Pombe Magufuli kwa kukubali kutoa kiasi cha
sh.bilioni 10 kwaajili ya ujenzi wa nyumba za polisi.
Alisema kutokana na fedha hizo, nyumba takriban 400 za askari polisi,
zinatarajiwa kujengwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa vituo hivyo vitatu, Inspekta Jenerali wa
Polisi, Simon Sirro alisema ujenzi wa kituo cha Mburahati umegharimu sh.
bilioni 1.2, Kiluvya (sh. milioni 227) na Mbweni (sh. milioni 667).
Alisema ujenzi wa vituo hivyo umeshirikisha wananchi wa maeneo husika,
Jeshi la Polisi na wadau werevu ambao ni walipakodi wazuri na wazalendo
zikiwemo taasisi na watu binafsi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI
MKUU,
ALHAMISI, MEI 24,
2018.
No comments:
Post a Comment