*Apokea
wanachama kutoka CUF, CHADEMA na ACT
*Yumo aliyekuwa
Katibu Mwenezi wa kata wa CHADEMA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea wanachama saba kutoka vyama vitatu
vya upinzani ambao wameamua kurejea Chama cha Mapinduzi (CCM) na wengine 82
kutoka Chama cha Wananchi (CUF) ambao walikuwa wapiga debe.
Wanachama hao
wamepokelewa leo mchana (Ijumaa, Mei 25,
2018) wakati akizungumza na
wananchi mara baada ya kukagua uwanja mpya wa michezo unaojengwa katika kijiji
cha Dodoma, kata ya Nachingwea, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
Waziri Mkuu ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, alipokea kadi
nne za CUF, moja ya ACT na mbili za CHADEMA kutoka kwa wanachama hao saba kabla
hajawakabidhi kadi za CCM. Wanachama hao saba waliokabidhiwa kadi mpya za CCM
pamoja na wenzao 82, walikula kiapo cha uaminifu mbele ya Waziri Mkuu.
Shangwe
zililipuka uwanjani hapo wakati aliyekuwa Katibu Mwenezi wa CHADEMA kata ya
Nachingwea, Bw. Ismail Hamisi alipokabidhi kadi yake kwa Waziri Mkuu.
Akisoma risala
kwa niaba ya wanachama wenzake walioamua kujiunga na CCM, mkazi wa Ruangwa
mjini, Bw. Fred Mnimbo alisema wameamua kurudi kwa sababu yale waliyotarajia
yafanyike upinzani hayaonekani.
“Tumegundua
upinzani wa sasa ni maslahi binafsi na si wa kuwatumikia wananchi; kinachosemwa
sicho kinachotendwa na wapinzani na pia tumeamua kuunga mkono juhudi anazofanya
Rais John Pombe Magufuli,” alisema Bw. Mnimbo katika risala hiyo.
Alisema wameamua
kuhamia CCM kwa sababu Serikali iliyopo madarakani kwa sasa inatekeleza
mahitaji ya Watanzania kwa asilimia 90 na pia wanataka kumuunga mkono mbunge
wao wakiwa katika chombo kimoja ili waijenge vizuri Ruangwa na Tanzania kwa
ujumla.
“Tunataka
kuunga mkono usimamizi mzuri wa rasilmali zetu hasa mazao ya korosho na ufuta
kutokana na jinsi unavyoyasimamia kikamilifu hasa mikoa ya Kusini. Kaulimbiu ya
Ruangwa kwa maendeleo inawezekana,
imedhihirika kwa vitendo kwa sababu kila mmoja anaona kwamba Ruangwa ya jana si
Ruangwa ya leo, maendeleo yanaonekana kwa mafanikio makubwa,” alisema huku
akishangiliwa.
Akitoa utambulisho
wa wanachama hao wapya, Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Bw. Barnabas Essau alisema
wanachama hao wameamua kujiunga na CCM kwa sababu wameridhishwa na utendaji wa
Serikali ya awamu ya tano.
Novemba 5, mwaka jana, Waziri Mkuu alipokea
wanachama 37 kutoka vyama vya CUF na CHADEMA kwenye mkutano wa hadhara
uliofanyika kijiji cha Mbekenyera, wilayani Ruangwa. Pia Desemba 29, 2017,
alipokea wanachama 60 kutoka CUF kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji
cha Nkowe kata ya Nkowe, wilayani Ruangwa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI
MKUU,
IJUMAA, MEI 25,
2018.
No comments:
Post a Comment