June 12, 2018

HAMASA ZA VIONGOZI WAKUU ZIMECHANGIA MAFANIKIO YA PAMBA-MONGELLA

MKUUwa Mkoa wa Mwanza, Bw. John Mongella amesema mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kilimo cha zao la pamba kwa mwaka huu, yametokana na hamasa iliyotolewa na viongozi wakuu wa Serikali.

Amesema kwa mwaka huu wanatarajia kupata mavuno makubwa kutoka katika kilimo cha zao la pamba kwa sababu wakulima wengi wamelima na baadhi tayari wameshaanza kuvuna.

Bw. Mongella amesema Rais Dkt. John Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa walitoa maelekezo na ufuatiliaji wa karibu wa kilimo cha mazao makuu matano ya biashara nchini, likowemo na zao la pamba.

Akizungumza kuhusu maendeleo ya zao hilo jijini Mwanza leo (Jumanne, Juni 12, 2018), Bw. Mongella amesema zao la pamba litasaidia kufufua viwanda vya mafuta ya kula, nguo pamoja na kuongeza ajira.

Amesema baada ya Rais Dkt. Magufuli kuhamasisha kilimo cha zao la pamba, ambacho kilianza kusuasua nchini, viongozi waliitikia na kuwahimiza wakulima wachangamkie fursa hiyo, ambao walikubali.

“Tunashukuru kwa hamasa na miongozo iliyotolewa na viongozi wetu kwa sababu iliongeza ari kwa wakulima kulima zao la pamba kwa wingi, pia hamasa hiyo imeongeza muamko kwa wananchi kulima mazao mengine, ilikiwemo la mpunga,” amesema.

Pia Bw. Mongella ameishukuru Serikali kwa kuagiza pamba itakayovunwa iuzwe kupitia minada itakayosimamiwa na Chama cha Msingi cha Ushirika (AMCOS) katika kila eneo, jambo ambalo limesaidia  kufufuka kwa vyama hivyo.

Amesema wanatarajia kuwahamasisha wakulima wote wa mkoa huo pamoja na wafugaji na wavuvi wajiunge katika AMCOS zilizoko katika maeneo yao, ili kuweza kuirahisishia Serikali kufanyanao kazi.

Hata hivyo, Bw. Mongella ametoa wito kwa wakulima kutumia taasisi za kifedha kwa ajili ya kuhifadhi fedha zao na wajijengee nidhamu ya matumizi, ambayo itawapa fursa ya kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment

Pages