Mkuu wa Mkoa wa Chiku
Gallawa akizungumza katika kikao cha wadua wa Afya kilichofanyika katika chuo
cha Uuguzi Mwambani Mkwajuni-Songwe, Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Songwe
Samwel Jeremia na Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Ileje Joseph Mkude.
Na Mwandishi Wetu, Songwe
Waganga wote wa jadi
wanaopiga ramli chonganishi maarufu kama Lambalamba wamepigwa marufuku kufanya
shughuli hizo mkoani Songwe huku wenyeviti wa vijiji ambavyo lambalamba
watabainika kuendelea na shughuli hizo, hatua kali dhidi yao zitachukuliwa.
Marufuku hiyo
imetolewa mapema leo na Mkuu wa Mkoa wa Songwe Chiku Gallawa katika kikao cha
wadau wa Afya mkoani hapa ambapo ameeleza kuwa changamoto mojawapo ya sekta ya
afya ni uwepo wa waganga wa jadi ambao huwapotosha wananchi kwa imani zisizo za
kweli.
Gallawa amesema, “Hatutaki
kuona wala kusikia hivi vikundi vya vya lambalamba, kazi yao kubwa ni ulaghai
na kuwaibia fedha wananchi, na ninaagiza, mwenyekiti yeyote wa kijiji
atakayebainika kuwaendekeza hawa watu tunaanza naye kumchukulia hatua kali za
kisheria”.
Ameongeza kwa
kuwaagiza wakuu wa wilaya zote mkoani hapa wasimamie kuhakikisha wananchi
hawatapeliwi na lambalamba hususani wilaya za Mbozi na Ileje ambako lambalamba
wameonekana mara kwa mara.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Waganga wa Jadi na Machifu Mkoa wa Songwe Mwenenzunda Mteleshwa
amesema kuwa yeye hawatambui lambalamba hivyo serikali iwachukulie hatua za
kisheria kwakuwa wanaenda kinyume na taratibu za utoaji wa huduma za jadi.
Wakati huo huo Gallawa
amezitaja changamoto nyingine katika sekta ya afya mkoani hapa ni uwepo wa
ugonjwa wa ebola nchi jirani ya Congo, upungufu wa vituo vya kutolea huduma za
afya pamoja na uwepo wa magonjwa yanayosababishwa na uchafu kama vile
kipindupindu.
Gallawa amefafanua
kuwa serikali imeweka mikakati ya kuboresha sekta ya Afya Mkoa wa Songwe kwa
kutoa shilingi bilioni 2.7 kwa ajili ya uboreshaji wa vituo vya kutolea huduma
za afya pamoja na Kuimarisha huduma za kitabibu kwa kuipandisha hadhi Hospitali
ya Wilaya ya Mbozi ili itumike kama Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe.
Ameongeza kuwa mkoa
unatarajia kuzindua mkakati wa usafi na mazingira ukiwa na kauli mbiu ya “Kataa
uchafu Songwe” lengo likiwa ni kupambana na magonjwa yanayosababishwa na uchafu
na kutunza mazingira.
No comments:
Post a Comment