Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akisalimiana na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Fadhili Nkulru wakati alipowasili kwenye viwanja vya ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kahama kuzungumza na watumishi wa Umma. Hii ilikuwa jana Julai 14 na leo Julai 15 Rais John Magufuli ametengua uteuzi wake. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekemea mahusiano
mabaya baina ya watumishi wa wilaya ya Kahama na kusema wanapaswa kubadilika
mara moja.
Ametoa onyo hilo leo (Jumapili,
Julai 15, 2018) wakati akizungumza na watumishi
na viongozi wa Halmashauri za Wilaya za Ushetu, Msalala na Kahama Mji, wilayani
Kahama mkoani Shinyanga.
“Hali ya mahusiano hapa Kahama ni mbaya kuliko
Kishapu na Shinyanga. Mnachapa kazi vizuri lakini tatizo kubwa kila mmoja
anaenda kivyake, hakuna anayemsikiliza Mkurugenzi wa Halmashauri wala Mkuu wake
wa idara,” amesema.
Waziri Mkuu ambaye yuko kwenye ziara ya siku tano ya
kikazi mkoani humo, amewaeleza watumishi na viongozi hao kwamba Serikali
haitavumilia kuona watumishi wa aina hiyo wanaendelea kufanya kazi.
“Serikali haitavumilia kuona watumishi wakifanya
mambo ya hovyo. Kahama ni wilaya yenye majaribu na Shinyanga nayo ni wilaya
yenye majaribu makubwa. Kwa hiyo watumishi inabidi muwe makini, kuweni
waangalifu msije mkaingia kichwakichwa kwenye majaribu haya.”
“Migogoro niliyoisikia ambayo iko hapa ni kwa sababu
ninyi mmeingia kwenye biashara na kutake
sides. Hapa Kahama, Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Wilaya hamuelewani,
Mkurugenzi na wakuu wa idara hamuelewani, wakuu wa idara na wasaidizi wao nao
pia hawaelewani,” alisema.
“Napenda kusisitiza kwamba ninyio ni viongozi wa
umma, kwa hiyo ni lazima mzingatie itifaki za kiuongozi, mzingatie mahusiano
mema mahali pa kazi. Hatupendi viongozi muwe chanzo cha matatizo hapa Kahama,”
aliwaasa.
Alisema Kahama ina fursa kubwa na nzuri kwenye
kilimo, madini, mifugo na biashara na akawataka viongozi wanaoletwa kwenye
wilaya hiyo wawe makini. “Kiongozi ukiletwa hapa inabidi uwe na kichwa
kilichotulia. Inabidi uwe mwaminifu sana ili uweze kudumu kwenye wilaya kama
hii,” alisisitiza.
“Kama kiongozi ulizoea kwenda disco inabidi uache,
kama ulizoea kwenda baa inabidi ununue kreti uweke ndani kwako. Kama ulizoea
kushabikia mpira kwa kujichora chaki, sasa basi. Kaa sebuleni kwako, angalia
mpira kwenye luninga yako, ndiyo dhamana ya uongozi hiyo,” alisema.
Aliwataka watumishi wa umma wawasaidie wananchi
kuboresha utendaji wao kwenye kilimo, uvuvi na ufugaji ili kila kuleta tija
kwenye kila sekta.
Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake wilayani Kahama
kwa kukagua shughuli za maendeleo na kuzungumza na wananchi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JULAI 15, 2018.
No comments:
Post a Comment