March 22, 2019

TANZANIA YAPIGA HATUA MATUMIZI YA VYANDARUA VYENYE DAWA

 Meneja wa Takwimu Mkoa wa Tabora kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Gabriel Gewe(kulia) akitoa maneno ya utangulizi wakati wa  semina za siku moja kuhusu usambazaji wa matokeo ya Utafiti wa Viashiria vya Malaria Tanzania wa mwaka 2017 kwa Kanda ya Magharibi kwa Waganga Wakuu wa Mikoa, Halmashauri, Waratibu wa Malaria Mkoa, Halamashauri ,Mameneja Takwimu wa Mikoa na  Wawakilishi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS). wengine ni Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Hamis Mkunga(katikati) na Mratibu wa Malaria wa Halmashauri ya Kigoma/Ujiji Dkt. Abigael Kasumani (kushoto) .
Mtakwimu Mwandamizi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Stephano Cosmas akitoa mada leo mjini Tabora wakati wa semina ya usambazaji wa matokeo ya Utafiti wa Viashiria vya Malaria Tanzania wa mwaka 2017 kwa Kanda ya Magharibi kwa Waganga Wakuu wa Mikoa, Halmashauri, Waratibu wa Malaria Mkoa, Halamashauri ,Mameneja Takwimu wa Mikoa na  Wawakilishi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS).  (Picha na Tiganya Vincent).

NA TIGANYA VINCENT
 
MATOKEO ya utafiti uliofanywa mwaka 2017 na Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine umeonyesha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika juhudi za kuzuia na kupambana na ugonjwa wa malaria kupitia matumizi ya vyandarua vyenye dawa katika ngazi ya kaya.

Kauli hiyo imetolewa leo mjini Tabora na Kaimu  Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Hamis Mkunga wakati akifungua semina za siku moja kuhusu usambazaji wa matokeo ya Utafiti wa Viashiria vya Malaria Tanzania wa mwaka 2017 kwa Kanda ya Magharibi kwa Waganga Wakuu wa Mikoa, Halmashauri, Waratibu wa Malaria Mkoa, Halamashauri ,Mameneja Takwimu wa Mikoa na  Wawakilishi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
Alisema utafiti huo umeonyesha jumla ya asilimia 78 ya kaya zote nchini zinamiliki walau chandarua kimoja chenye dawa ambapo  kaya za mjini zina uwezo mkubwa wa kumiliki vyandarua kwa asilimia 81 ukilinganisha wa vijijini ambapo ni asilimia 77.

Mkunga alisema katika utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria wa mwaka 2015/16, ni asilimia 66 tu za kaya zilikuwa zinamiliki angalau chandarua kimoja chenye dawa. 

Aliongeza kuwa kwa upande wa Tanzania Bara, Mkoa wa Pwani ndio unaoongoza kuwa na kiwango kikubwa cha umiliki wa vyandarua vyenye dawa kwa asilimia 89 na Mkoa wa Njombe una kiwango kidogo cha umiliki wa vyandarua vyenye dawa asilimia 58 ikilinganishwa na mikoa mingine. 

Aidha, Mkunga alisema matokeo ya utafiti huu yameonesha kiwango cha malaria kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano nchini kimeshuka kwa zaidi ya nusu kutoka asilimia 14.4 mwaka 2015 hadi asilimia 7.3 mwaka 2017.

Aliitaja miongoni mwa mikoa ya Tanzania Bara ambayo imeonyesha kuwa kiwango kikubwa cha watoto wenye malaria ni Kigoma  kwa asilimia 24.4 ikifuatiwa na Geita yenye asilimia 17.3, Kagera asilimia 15.4 na Mtwara asilimia 14.8 ambapo Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Njombe, Songwe, Dodoma na Mikoa yote 5 ya Zanzibar ina kiwango kidogo cha maambukizi ya malaria ya chini ya asilimia moja.

Mkunga alisema pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kupunguza kiwango cha malaria, bado wanajamii wanatakiwa kutumia vyandarua ipasavyo katika kujikinga na ugonjwa wa malaria, kuondoa mitazamo potofu kama vile viuatilifu vinaleta kunguni na viroboto na kuwa vyandarua vinapunguza nguvu za kiume.
Utafiti huo umefanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Zanzibar kwa kushirikiana na wadau wengine

No comments:

Post a Comment

Pages