June 14, 2019

KATIBU MKUU ARDHI AZINDUA MRADI WA UPATIKANAJI TAARIFA ZA ARDHI

Meneja wa Mradi wa Uanzishaji Miundombinu ya Upatikakanaji Taarifa za Ardhi kutoka nchini Korea Hooyoung So akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo katika ofisi za Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi zilizopo eneo la Mtumba Jijini Dodoma tarehe 13 Juni 2019. Katikati ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Dorothy Mwanyika. 

Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dorothy Mwanyika amezindua mradi wa Uanzishaji Miundombinu ya Upatikanaji Taarifa za Ardhi nchini.
Uzinduzi wa mradi huo umefanyika katika ofisi za Wizara eneo la Mtumba jijini Dodoma na kuhusisha Watendaji wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wawakilishi kutoka Korea Eximbank ya nchini Korea ambapo kazi ya Usanifu mradi huo itapitia hatua tofauti na kukamilika Novemba 2019.
Akizungumza wakati wa uzinduzi mradi huo, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Dorothy Mwanyika alisema uzinduzi wa kazi ya kusanifu uanzishaji miundombinu ya upatikanaji taarifa za ardhi nchini Tanzania siyo tu utasaidia wananchi katika masuala ya umiliki wa ardhi bali utawezesha kubuni, kusanifu na kujenga miundombinu kama vile Barabara, Reli, Majengo pamoja na Miradi mikubwa.
Kwa mujibu wa Mwanyika, Mradi wa Uanzishaji Miundombinu ya upatikanaji taarifa za ardhi utasaidia pia katika kukusanya mapato ya serikali kupitia sekta ya ardhi kwa kuwa maeneo ya wamiliki ya ardhi yatakuwa yameainishwa na hivyo kuwa rahisi wamiliki wake kutambulika na kusisitiza kuwa Wizara yake itafanya kila jitihada kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa manufaa ya Taifa.
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi huo, Erick Mwaikambo alisema, uzinduzi wa mradi huo utawezesha upatikanaji ramani za msingi pamoja na taarifa zinazowezesha upimaji ardhi kufanyika kwa haraka na kwa kasi na kwa bei nafuu na kuwezesha maeneo mengi nchi kupimwa pamoja na wananchi kupata miliki kwa urahisi.
Kwa mujibu wa Mwaikambo, mbali na mambo mengine mradi huo pia utasaidia upatikanaji ramani zitakazotumika kuandaa matumizi ya ardhi na hivyo kurahisisha kuwepo kwa miji iliyopangwa pamoja na kuondoa migogoro katika maeneo ya vijijini ikiwemo ile migogoro ya wakulima na wafugaji.
Mratibu huyo wa Mradi wa kuanzisha Miundombinu  ya Upatikanaji Taarifa za Ardhi aliongeza kwa kusema kuwa, mradi huo utasaidia pia shughuli za kubuni, kusanifu na kujenga miundombinu sambamba na kuwezesha kutunza mazingira na maliasili na Sensa ya watu na makazi na hivyo kusaidia zoezi la kupiga kura wakati wa uchaguzi.
Mradi wa Kusanifu Uanzishaji Miundombinu ya Upatikanaji Taarifa za Ardhi nchini Tanzania unafadhiliwa na Serikali ya Korea kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi wa nchi hiyo na Benki ya Exim ya Korea (Korea Eximbank).

No comments:

Post a Comment

Pages